Thursday, September 19, 2013

Toufik Alikuwa Mwislamu Lakini Alimwita Yesu, Leo Ameokolewa na Hajawahi Kujuta


Ufuatao ni ushuhuda wa Toufik, ambaye alikuwa ni Mwislamu lakini alikutana na injili ya Bwana Yesu na kubadili welekeo ambao hajaujutia; na hata anapoelezea neema hii ya wokovu wa Yesu aliyoipata, machozi yanamtoka. Pia machozi yanamtoka zaidi anapowafikiria ndugu zake Waislamu ambao wanapambana kwa jitihada nyingi wakijaribu kumpendeza Mungu kwa njia ya matendo yao ya kidini. Toufik analia anapotambua kuwa yote hiyo wanayofanya ni kazi bure kwa kuwa hawajagundua ziri ambayo na yeye, miaka mingi iliyopita, alikuwa hakuijua.


......................

Nilikulia kwenye familia ya Kiislamu ambayo ilikuwa inatii imani ya Uislamu. Nilipokuwa na miaka mitano nilienda shuleni. Na wakati huohuo nilihudhuria msikitini na kufundishwa kuhusu Uislamu.

Nilipokuwa nikimtafakari Allah, sikumuona kama Mungu mzuri, Muumba anayependa viumbe wake. Nilimuona kama Mungu mkubwa sana ambaye wakati wowote alikuwa tayari kuniharibu.

Hata mimi mwenyewe sikujiona kama mtu anayekwenda mbinguni. Nilipotazama matendo yangu mazuri na yale mabaya, sikuona uwezekano wa mimi kupona.

Nilijiuliza maswali mengi: Hali yangu ya kiroho ikoje? Mungu yuko wapi sasa? Hivi mimi anaponiangalia ananionaje hasa? Anawaza nini juu yangu? Hivi ndio nimetengwa kabisa naye kutokana na dhambi zote nilizofanya? Je, kuna njia ya kumrejea? Nawezaje kurejea tena kwake?

Wakati fulani nilipewa nafasi ya kuishi na Wakristo fulani. Familia ile ya Kikristo niliyoenda kuishi nao walikuwa na upendo kwa ajili yangu. Mwanzoni niliwaza kuwa labda walikuwa wanajifanyisha tu; wanaigiza tu. Nikasema, si muda mrefu nitajua tu; ukweli utadhihiri tu!

Niligundua kuwa upendo uliokuwamo baina yao kama familia ulifikishwa hata kwangu. Haukuwa ni upendo wa kawaida tu (eros, filios), bali ulikuwa ni upendo ambao walisema kuwa unatoka kwa Mungu. Nikawa siamini kwamba, iweje Mungu awape kitu ambacho hakunipa na mimi? Wao wana nini ambacho mimi sina?

Niliona kujitoa kwao ambako sikuwa nako. Niliona jinsi baba wa familia ile alivyoamka asubuhi, akaenda kazini hadi usiku, na anaporudi wanaungana mezani na kushikana mikono kisha wanaomba. Au anawaambia watoto waimbe wimbo na kubariki chakula. Niliona jinsi ambavyo hakuwahi kuinua sauti yake kwa mkewe au watoto wake. Niliona jinsi walivyoongea. Na kuhusu nafasi ya mke, aliheshimiwa. Alikuwa na sauti katika kuongea. Alikuwa na mambo mazuri ya kuwafunza wale watoto. Na alipoongea, alisema mambo yenye maana. Alikuwa na akili. Alikuwa na elimu.

Nilikutana na mwanamume ambaye alikuwa akikaa na wanawe na kuwasomea Biblia. Kisha aliwauliza maswali mwishoni na walishikana mikono na kuomba.

Nilishangazwa na ugunduzi huu. Ulikuwa ni nuru katika maisha yangu ya kiroho! Kwa hiyo niliuliza maswali. Na nilisikia hawa Wakristo wakiniambia, “Unamhitaji Mwokozi.”
Walisema, “Tuna jibu la shida yako.” 

Na hapondipo nilipoanza kujiuliza maswali. Kwa hiyo nilienda kwenye Quran. Siku moja nilikuwa nasoma nakala nne za mtu anayeitwa Sayid Khotib. Ni mtu aliyetafsiri Quran. Nilipokuwa nasoma, nikakuta kuwa karibu kila rejea aliyotoa ilitoka kwenye Biblia. Alirejea kwa Yohana mtume, kwa Paulo … na maswali yangu yakaanza kuja tena. Nikasema, kwa nini? Sisi Waislamu tunaamini kuwa Biblia imepotoshwa, hivyo hatuamini kuwa ujumbe wake ni wa kutiliwa maanani. Kwa nini sasa bwana huyu anarejea humo kufafanua maelezo yake kuhusu Quran?

Hili nalo lilifungua ufahamu wangu. Nikasema, huyu mtu anaheshimika sana kwenye ulimwengu wa kiislamu. Lakini anarejea kwenye Biblia. Ina maana kuwa Biblia ina ukweli basi!

Kilichofuata, siku moja nilienda porini karibu na nilikoishi saa tano usiku. Nilipiga magoti na kuinua macho yangu juu na kusema, “Mungu, kama kweli uko pale juu, sitaki uje kama ulivyoongea na Musa, na Yesu na manabii wengine; nataka uongee na mimi moja kwa moja. Nataka ujionyeshe kwangu.” Hilo lilikuwa swali langu kutoka moyoni kabisa.

Zilipita siku 30. Siku niliyokuwa naondoka kwenye ile nyumba ya wale Wakristo, maana siku ya jumamosi niliwaambia kuwa, “Siku ya jumatatu nitapata cheki yangu kutoka kwenye kampuni ninayofanyia kazi, hivyo nitarudi kule nilikotokea. Sidhani kama nitawafuata ninyi; sidhani kama nitakuwa Mkristo; si mimi! Mimi ni Mwislamu na Mwarabu. Nitakufa nikiwa Mwislamu na Mwarabu. Hilo ndilo ninalolijali.” Nikaacha hivyo.

Hata hivyo, jumatatu ilifika. Huyu mama nilikokuwa, alikuwa na tabia ya kuacha kaseti kwenye gari langu. Siku hiyo niliendesha gari, na mara kaseti ikaanza kuongea. Kwa kawaida nilikuwa nikiondoa kaseti hizo na kuzitupia kwenye kiti cha nyuma. Japo wakati mwingine nilikuwa nizisikiliza, lakini sikuwa nimewahi kusikia mtu akiongea kama wakati ule – ilikuwa ni kama yule mtu alikuwa akiongea moja kwa moja na mimi! Na kile alichosema ni kuwa: Unataka upendo wa Mungu, siyo? Nilianza kulia. Nikasema, “Ndiyo, nautaka. Upendo wa Mungu ninauhitaji. Kama ningejua ni nini cha kufanya ili kuupata, basi niko tayari hata kutoa maisha yangu. Kama nikijua kuwa huyu Mungu ninayemwamini atanipenda licha ya dhambi zangu; na kwamba ataniosha dhambi zangu zote, basi nitakuwa tayari kuwa mtumishi wake!”

Siku hiyo jioni nilirudi tena kwenye ile nyumba ya ile familia ya Kikristo. Sikuwaambia chochote. Lakini waliniona nilikia, jambo ambalo hawakuwahi kuliona kabla. Siku hiyo walielewa jambo ambalo mimi sikulijua. Walinikumbatia na kulia pamoja na mimi kuanzia saa 4:30 hadi saa 8:00 usiku.

Jumapili ilifika. Nilienda kanisani. Sitasahau siku ile. Mchungaji akasema, “Tuna ndugu hapa ambaye anapenda kutushirikisha jambo.”

Nilisimama. Sikuwaambia kama ninavyokuambia wewe sasa, maana sikuwa naelewa. Nilisema, “Sasa ninamwamini Yesu wenu. Yeye ni Mwokozi wa kweli. Amenipa amani. Amechukua dhambi zangu.”

Nililia. Niliangalia nikakuta kusanyiko lote wanalia pamoja na mimi!

Na siku moja, dada huyu ambaye aliniongoza kwa Kristo alifiwa na kaka yake. Na mimi nilihudhuria kwenye ule msiba. Na baada ya msiba walikusanyika ili kuwapatia chakula wageni waliokuwa wamekuja kutoka mbali. 

Nilienda mapokezi na watu wakaanza kuja na kunipa mikono. Wakawa wanasema, “Wewe utakuwa ni fulani.”
Nikasema, “Ndiyo.”
Wakawa wananinong’oneza kwamba, “Nimekuwa nikikuombea.”

Na karibu watu kumi waliponiambia hivyo, nilijua kuwa Mungu hakuniokoa mimi kwa sababu yangu! Aliniokoa kwa sababu ya sala za wale watu!

Miezi sita baadaye nilikuwa kwenye chuo kikuu cha Biblia. Miaka miwili baadaye nilikuwa namtumikia Bwana, na bado naendelea kumtumikia Bwana.

Nilienda kwenye msikiti ambako nilikuwa nikienda kuswali zamani, na niliwaangalia Waislamu na nikaona kile ambacho wanapambana nacho; wakifanya kile wanachotakiwa kufanya; wanachoambiwa kufanya – matendo baada ya matendo … hakuna kinachotoka moyoni! Hakuna kitu kinachoweza kubadili mioyo yao!

Huwezi kutoa upendo wakati wewe mwenyewe hauna upendo. Huwezi ukatoa amani wakati wewe mwenyewe haujui amani ni nini. Lakini bado unasema, ‘asalaam aleikum – amani iwe juu yako – kila wakati; ilhali hamna amani ndani yako!’

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW