Ukristo barani Afrika una historia ndefu inayokaribia miaka elfu mbili.
Wakati mwingine tunaweza kusikia kuwa Ukristo uliingizwa Afrika juzijuzi tu, na asili yake ni Ulaya. Hili si kweli. Ukristo ni imani ya kale sana katika Afrika. Tangu mwanzo wa Kanisa walikuwepo Wakristo Waafrika.
Ukristo uko Afrika katika wingi wa madhehebu yaliyopatikana katika historia ya Kanisa, baadhi katika bara hilo, baadhi katika mabara mengine.
Kwa sasa ndiyo dini kubwa zaidi barani, hasa Kusini kwa Sahara, pamoja na Uislamu ambao unaongoza Kaskazini kwa jangwa hilo.
Leo karibu nusu ya Waafrika wote ni Wakristo. Lakini asilimia ya Wakristo inaweza kuwa ndogo katika nchi kadhaa na kubwa katika nchi nyingine. Katika Afrika Kaskazini Wakristo ni wachache. Kumbe ni wengi kwa theluthi mbili za bara kusini kwa Sahara.
Kwa jumla Wakristo wanaishi kati ya wafuasi wa dini nyingine, hasa Uislamu na dini za jadi.
Idadi yao inaongezeka haraka sana. Kila baada ya nukta nne Mwafrika mmoja anaingia Ukristo. Wengine huzaliwa katika familia ikiwa mzazi mmoja au wote wawili ni Wakristo tayari. Katika madhehebu mengi iko desturi ya kuwabatiza watoto wadogo. Ubatizo huo unawafanya kuwa wanakanisa. Wakikua watafundishwa na pengine kukaribishwa kwenye Kipaimara. Katika ibada hiyo kijana atarudia ahadi ya ubatizo wake na kuwekewa mikono na askofu au mchungaji mwingine na kuombewa ili Roho Mtakatifu amsaidie katika maisha yake ya Kikristo. Madhehebu mengine hayabatizi watoto wadogo. Yanaweza kuwapokea katika Kanisa kwa ibada maalumu lakini yanasubiri mpaka mtoto atakapokuwa mtu mzima, halafu apokee ubatizo na kuwa Mkristo rasmi.
Njia nyingine ya kukua kwa Kanisa ni kuongoka. Maana yake mtu asiye Mkristo anasikia habari za imani na kuvutiwa moyoni. Halafu anafika kwa kiongozi wa Kanisa na kupata mafundisho juu ya imani na maisha ya Kikristo. Halafu anaweza kubatizwa. Atakuwa mwanakanisa katika dhehebu fulani lakini ni vilevile Mkristo katika Kanisa moja takatifu la Bwana Yesu lililopo popote duniani. Wakristo Waafrika wengi kidogo ni watu walioongoka: waliwahi kuwa wafuasi wa dini nyingine (hasa dini za jadi, lakini wengine Uislamu), wakasikia Habari Njema wakaamua kumfuata Yesu.
Ukristo nchini Tanzania ulianzishwa na wamisionari wa Shirika la Mt. Agostino kutoka Ureno walioongozana na Vasco da Gama mwaka 1499 hadi Zanzibar.
Huko walijenga konventi ya shirika lao ili kuhudumia kiroho Wakristo toka Ulaya tu.
Misheni ilipingwa na Waarabu Waislamu na e kukoma mwaka 1698, kisiwa hicho kilipotekwa na Waarabu wa Oman.
Uinjilishaji ulifanikiwa zaidi katika sehemu ya pili ya karne ya 19 hasa ulipofanyika katika maeneo ya bara.
Kati ya Waprotestanti, waliotangulia walikuwa wamisionari Krapf na Rebmann waliotumwa na chama cha C.M.S.; kutoka kwa kituo chao karibu na Mombasa walifika mpaka eneo la Tanzania ya leo. Kituo cha kwanza cha C.M.S. katika Tanganyika kilikuwa Mpwapwa mwaka 1876.
Mapadri Wakatoliki wa kwanza pamoja na masista walitokea Reunion wakakaa Unguja tangu tarehe 12 Desemba 1860 hadi mwaka 1863, walipokabidhi misheni kwa shirika la mapadri wa Roho Mtakatifu. Halafu hao mwaka 1868 wakafungua huko Bagamoyo kituo cha kukalisha watumwa waliowanunua na kuwapa uhuru. Walifuatwa na Mapadri Weupe (1878) walioanza mwaka 1879 kwenye Ziwa Tanganyika.
Katika mazingira ya Kanisa la Anglikana chama cha Misheni ya Vyuo Vikuu kwa Afrika ya Kati U.M.C.A. (Universities` Mission to Central Africa) kiliundwa kutekeleza wito kutoka David Livingstone kuhubiri Injili na kukomesha utumwa katika Afrika. Waliingia kule Zanzibar mwaka 1864, wakajenga kanisa kuu mahali pa soko la watumwa lililofungwa, altari ikiwa imejengwa juu ya nafasi ya mti wa kuwafunga watumwa walioadhibiwa kwa viboko, na batizio kuwa mahali walipotupwa watoto watumwa ambao hawakuuzwa pamoja na mama zao.
Baada ya kwanza ukoloni wa Kijerumani serikali iliomba makanisa ya Ujerumani kuchukua wajibu badala ya kuwaachia watu wa mataifa wengine.
Walutheri wa kwanza walifika Dar-es-Salaam mwaka 1887.
Mwaka 1888 walifika watawa Wajerumani wa kwanza wa shirika la Mt. Benedikto waliounda baadaye monasteri za Peramiho na Ndanda na kushughulikia uinjilisti kote Kusini.
Mwaka 1891 walifika wamisionari Walutheri (misheni ya Berlin) na Wamoravia kupitia Ziwa Nyasa wakiwa wamepatana kugawa kati yao maeneo ya kazi kama walivyogawana wachungaji wa Ibrahimu na Lutu; walijenga vituo katika Unyakyusa kule Rungwe na Manow.
Ni kwamba Walutheri waliomba Wamoravia kuanza kazi pamoja katika Tanganyika Kusini-Magharibi. Baadaye walichapisha hata kitabu cha pamoja cha nyimbo za Kikristo.
Walutheri wengine yena (misheni ya Leipzig) walianza kule Uchagga kituo cha Moshi.
Wajerumani wengine waliofika mapema walikuwa Waadventista Wasabato.
Kutoka Kenya ilianzishwa kazi ya A.I.M. (Africa Inland Mission) katika mkoa wa Mwanza - chama hicho kiliundwa Marekani kama misheni ya kimadhehebu yenye athari kubwa ya Kibatisti.
Karne ya 20 iliona wamisionari wengi kutoka madhehebu mbalimbali ya Ulaya na Marekani. Baada ya vita vya pili vya dunia Wamarekani walianzisha Kanisa la Kibatisti Kusini-Magharibi mwa Tanzania. Walifika pia wamisionari mbalimbali wa Kipentekoste. Tofauti na nchi za Afrika Kusini na Magharibi, wamisionari wa makanisa ya Wamarekani Weusi hawakuwa na athari kubwa.
Tofauti na Kenya, ambako Kanisa la Kiorthodoksi la Kiafrika (linaloshirikiana na Patriarki wa Kigiriki wa Aleksandria-Misri) ni kubwa, nchini Tanzania halikuenea mapema, isipokuwa wahamiaji Wagiriki walijenga makanisa machache ya Kiorthodoksi kule Dar es Salaam, Iringa, Arusha n.k.
Hasa karne ya 20 imekuwa ya kurudisha umoja. Wakristo wa madhehebu mbalimbali yanashirikiana kirahisi katika shughuli mbalimbali.
Mwaka 1936 viongozi wa madhehebu kama Walutheri, Waanglikana, Wabatisti na Wamoravia waliunda "Baraza la Misheni Tanzania". Baraza hilo lilikuwa mtangulizi wa CCT (Jumuiya ya Kikristo Tanzania / Christian Council of Tanzania).
Katika miaka ya 1960 viongozi wa makanisa ya Kiprotestanti waliongea juu ya kuunda Kanisa la Muungano katika Afrika Mashariki. Kwa bahati mbaya wafadhili wengine kutoka ng'ambo waliona hawawezi kusaidia kanisa la muungano kama si tena la madhehebu yao. Ilionekana hiyo ni hatari kwa kazi kama hospitali na shule zilizotegemea msaada kutoka ng'ambo, hivyo muungano ulisimamishwa.
Lakini madhehebu yaliyoongea hivyo wakati ule yanaendelea kushirikiana katika vyombo vya pamoja kama vile CCT. Wanachama wa CCT ni kama wafuatao: Walutheri, Waanglikana, Wamoravia, African Inland Church, Wabatisti, Wapresbiteri, Jeshi la Wokovu, Kanisa la Uinjilisti (Mbalizi), pia vyama kama TCRS/Huduma ya Kikristo ya wakimbizi Tanzania.
Ushirikiano umejengwa pia kati ya Waprotestanti na Kanisa Katoliki. Zamani za wamisionari uhusiano huo ulikuwa mgumu mara nyingi. Lakini mabadiliko mengi yamejenga msingi wa uelewano na hali ya kuheshimiana.
Hatua muhimu sana ilikuwa mkutano mkuu wa Kanisa Katoliki duniani ulioitwa Mtaguso wa Pili wa Vatikano miaka 1962-1965. Hapo maaskofu wote chini ya uongozi wa Papa (kwanza Papa Yohane XXIII, halafu Papa Paulo VI) walitamka kwamba Wakristo wote ni ndugu na kwamba kujenga umoja wa Kanisa ni wajibu wa kila mmojawao.
Leo hii makanisa ya CCT na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hushirikiana katika shughuli mbalimbali kama vile Baraza la Kikristo la Afya Tanzania (Tanzania Christian Medical Board) au katika kuandaa mafundisho ya pamoja katika elimu ya Kikristo mashuleni.
Chama cha Biblia ni chombo kingine cha ushirikiano wa kimadhehebu. Chama hicho kina kazi ya kutoa Biblia kwa bei nafuu kwa watu wengi. Kinasimamia tafsiri ya Biblia katika Kiswahili cha kisasa na lugha nyingine za kikabila. Kinaandaa matoleo mapya ya Biblia na misaada ya kuielewa kama "Itifaki ya Biblia".