Monday, April 4, 2016

KHALIL GAIDI WA KIISLAM AMPOKEA YESU
Huu ni ushuhuda wa kweli kabisa kutoka kwa kijana wa Kimisri ambaye Bwana Yesu mwenyewe alimtoa kutoka kwenye uasi na kumfanya kuwa mtu mpya kabisa anayempenda Bwana Yesu pamoja na wanadamu wenzake wote.


Khalil alianza kukariri Qur’an angali mdogo sana. Baadaye alianza kusoma vitabu vingine vinavyozungumzia Uislamu na tafsiri ya Qur’an. Kulingana na welewa wake juu ya Quran, alifikia mahali ambapo hata wazazi wake aliwaona ni makafiri. Kwake, kama mwanamke aliacha hata kujifunika ushungi, basi anakuwa si Mwislamu tena. Khalil aliwaona Wakristo kuwa ni maadui zake wakubwa na akaanza kujihusisha na mashambulizi dhidi yao pamoja na makanisa. Kundi la Kiislamu ambalo lilikuwa na mipango ya kuangusha serikali isiyo ya kidini ya Misri na kusimika sheria kali za Kiislamu, walimchukua ili awe mmoja wao, kisha wakamfanya kuwa kiongozi wa eneo lake.


Lakini hatimaye, vyombo vya usalama viligundua njama hizo na kumkamata Khalil pamoja na wanakikundi wenzake wengi. Alikaa gerezani miaka miwili. Alipoachiwa, alikimbilia Yemen pamoja na baadhi ya wenzake. Huko waliendelea na mipango yao ya kujiandaa kuangusha utawala wa Misri.


Kule nako mipango yao iligundulika na wengi wao walikamatwa tena. Matokeo yake kikundi kile kiliamua kuachana na mipango yao ya kuangusha utawala kwa njia ya kijeshi. Aliporudi Misri, siku moja alisoma kwenye gazeti juu ya Wakristo waliokamatwa kwa kuwahubiria watu Injili. Khalil na wenzake waliamua kuwa inabidi wafanye jambo kwa ajili ya Uislamu.


Kwa vile sasa walikuwa wachache, waliamua kuwa vita yao wataifanya kwa kutumia elimu, utafiti na kuandika kitabu ambacho kinaonyesha kuwa Mohammad ni Mtume wa kweli wa Mungu; na kwamba Biblia ya Wakristo na Wayahudi ni maandiko ambayo yamepotoshwa kwa kuingizwa mambo ambayo si ya Mungu. Khalil aliteuliwa na Amir, (yaani kiongozi wa Kundi la Kiislamu), ili afanye huo utafiti na kuandika kitabu hicho. Mwanzoni, Khalil alikataa katakata, maana kulingana na maneno yake, mama yake alishawahi kusema kuwa Wakristo hutumia kitabu hicho kulaani watu na kufanyia mambo ya kimazingara; na kwamba mtu anayekisoma kitabu hicho, anapata laana. Hata hivyo, baadaye alikubali; kazi ambayo anasema aliiona kuwa ni mbaya kuliko zote alizowahi kufanya.


Alipomaliza kusoma Biblia na kulinganisha kile alichosoma na kile kilichoko kwenye vitabu vya Kiislamu, Khalil alishangaa sana kuona kuwa Biblia haina mahali ambako haiko sahihi wala mahali ilikoingizwa maneno yasiyo ya Mungu. Badala yake alishangazwa na mafundisho ya Biblia yanayohusu kusamehe na kuwa na upendo usio na masharti. Alishangazwa zaidi aliposoma jinsi Yesu alivyowaonya wafuasi wake kwamba watateswa; na miaka elfu mbili baadaye, hilo lilikuwa linatendeka kama Yesu alivyosema ingekuwa (huku Khalil akiwa ni mmoja wa wanaosababisha mateso hayo kwa wafuasi wa Yesu). Kusoma kwake Biblia kulimwezesha kuelewa kwa nini Wakristo wa Misri hawajawahi kulipiza kisasi kwa Waislamu; na kwa nini mara zote kwao imekuwa rahisi kusamehe na kusahau. Japokuwa alianza akiwa anaichukia kabisa Biblia, alijikuta amependa ujumbe wake na mafundisho yake.


Hata hivyo, jukumu lake alilokabidhiwa lilikuwa bado paleplale likimngoja. Naye aliendelea nalo kwa nguvu kabisa, ili kuthibitisha kwamba Yesu si Mungu na kwamba hakuwahi kusulubiwa. Angali akisoma Qur’an kwa lengo hili, aliandika sifa zote za Mungu kulingana na Quran; kisha akapekua kwenye Qur’an hiyohiyo juu ya sifa za Yesu. Kulingana na Quran, Mungu ni muumbaji, mponyaji, mtoa mahitaji, ndiye pekee anayeweza kufufua wafu, ndiye pekee anayetenda miujiza, ndiye pekee mwenye kuhukumu kwa haki, na kadhalika. Kwa mshangao mkubwa, Khalil aligundua kwamba hizi ndizo sifa zilezile ambazo Qur’an hiyohiyo inampa Yesu (Isa), jambo ambalo lilimthibitishia Khalil kuwa Yesu na Mungu kumbe ni kitu kimoja.


Lakini hapo sasa mashaka yaliingia moyoni mwa Khalil. Maisha yake yakawa ya mateso. Akawa anawaza afuate kipi. Siku zote aliupenda Uislamu na kuamini kuwa ndiyo njia pekee ya kwenda kwa Mungu kupitia Mohammad. Alianza kujiuliza maswali, “Sasa kama Yesu na Mungu ni kitu kimoja, Mohammad ni nani sasa; na njia ya kwenda mbinguni ni ipi?” 


Siku moja, Amir wake alifika kumtembelea nyumbani kwake ili kuona anavyoendelea na utafiti waliokubaliana. Amir aliweza kuona mambo yote ambayo Khalil alikuwa ameandika (uungu wa Yesu, kwamba Qur’an si neno la Mungu, n.k.).  Amir hakuamini macho yake. Alimwambia Khalil kwamba angemuua kama angesema mawazo yake hayo ya kizushi kwa Mwislamu yeyote, na kwamba kuanzia hapo yeye, Khalil, amekuwa ni kafiri!


Khalil, hata hivyo, hakuachana na mawazo aliyoyapata kwamba Ukristo ndiyo njia ya kweli. Huku akiwa na shauku ya kujifunza zaidi, aliamua kwenda kujiunga na kanisa. Kutokana na historia yake ya ukatili na ghasia, hakuna mtu aliyemwamini. Kila mtu alikataa kukutana naye, hata wachungaji nao waligoma. Hapo alikata tamaa na kuwaza kuwa huenda alikosea kuwaza hivyo; labda Ukristo wala si njia ya kwenda mbinguni. Lakini, sauti ndani yake ilimwambia asiwatazame wanadamu.

Siku moja alikuwa anajaribu kupiga simu kwenye kibanda cha simu huku akiwa ameweka begi lake nje ya kibanda. Alipita kibaka na kuiba lile begi. Ndani yake kulikuwa na nyaraka zote za utafiti wake, Biblia na kitambulisho chake. Aliogopa sana kwa sababu kila kitu alichokuwa ameandikwa kingehesabika kuwa ni kufuru; ilhali kuna na kitambulisho chake ndani humo! Alikimbia nyumbani huku akiwa na mawazo mengi sana.


Akiwa chumbani kwake, alianza kutubu kwa yote aliyofanya. Aliwaza kuwa Mungu alikuwa anamwadhibu kwa kuthubutu kuwaza kuwa Mohammad hakutumwa na Mungu na kwamba Qur’an si neno la Mungu. Alitubu, akatawadha, na kuchukua mkeka ili afanye sala. Lakini magoti yalishindwa kukunjika, na wala kinywa chake hakikufunguka kusema hata neno moja la Qur’an. Khalil alikaa chini na kusema, “Mungu unajua kuwa nakupenda, na ninafahamu kuwa unapenda mimi niwe kwenye njia sahihi. Mungu, siwezi kupingana na hilo tena. Kila nilichofanya, nilikuwa najaribu kukupendeza wewe. Tafadhali, nitoe kwenye giza hili.”


Usiku ule, Khalil alilala kwa namna ambayo hakuwahi kulala kwa miaka mingi. Aliota ndoto. Alimwona mwanamume aliyemjia na kumwambia kuwa alikuwa ndiye yule ambaye Khalil amekuwa akimtafuta. Khalil hakujua huyo alikuwa ni nani. Yule mtu alimwambia Khalil aangalie kwenye Kitabu (yaani Biblia). Khalil akasema kuwa Kitabu pamoja na nyaraka zake zote vilipotea. Yule mtu akasema, “Kitabu huwa hakipotei. Inuka ufungue kabati lako, utakikuta humo. Na nyaraka zako zingine utarudishiwa ifikapo mwisho wa wiki.”  


Khalil aliamka kutoka usingizini na kwenda moja kwa moja kufungua kabati. Cha kushangaza, aliikuta Biblia yake palepale, japokuwa iliibwa pamoja na begi lake! Huku akijua kuwa amemwona Yesu, kwa haraka alienda kwenye chumba cha mama yake, akamwamsha, akaanza kumwomba msamaha kutokana na miaka mingi ya ukali na madhila mbalimbali aliyowafanyia familia yake. Hakuishia hapo kutafuta amani na mapatano. Kulipokucha, Khalil aliingia mitaani, akawa anawasalimu marafiki na wageni. Akawatafuta Wakristo wamiliki wa biashara ambao aliwahi kuwaibia, au kuwafanyia ukatili, akawaomba msamaha pia!


Baada ya miezi kadhaa, Khalil alikua katika imani yake mpya; na kidogo kidogo akaanza kuaminiwa na Wakristo wa mahali hapo na akawa ameingia kanisani. Alibatizwa na sasa anaendelea kupambana na mashambulizi ya kimwili na vitisho dhidi ya maisha yake kutoka kwa wale aliokuwa nao zamani. Lakini Khalil anahisi kuwa yuko tayari kulipa gharama yoyote kwa ajili ya Yule ambaye alitoa kila kitu kwa ajili yake, yaani Yesu Kristo.

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW