Thursday, April 8, 2021

JE, KUNA SABATO KATIKA AGANO JIPYA?

 *SABATO KATIKA AGANO JIPYA*

Na Askofu Mkuu Zakaria Kakobe.

Biblia inasema kwamba, siku hizi za mwisho, kutakuwako nyakati za hatari.


Wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo na mafundisho yaliyo kinyume na kweli [2 TIMOTHEO 3:1; 1 TIMOTHEO 4:1]. Siku hizi tulizo nazo tunazungukwa na “WANAFUNZI WA MUSA” [YOHANA 8:28-29], ambao kwa kutaka kuwawekea watu msisitizo mkubwa wa kuabudu Jumamosi na kushika Sabato; wanafundisha kwamba watu wote wanaoabudu Jumapili wamepotea, na tena wana alama ya mnyama “666”.

Wanafundisha kwamba kuiacha Sabato na kuabudu Jumapili kulianzishwa na Costantine pamoja na Kanisa Katoliki. 

Ni muhimu basi kama wanafunzi wa Yesu, kujifunza yote kuhusu jambo hili, ili tuweze kuishindania imani tuliyokabidhiwa watakatifu MARA MOJA TU [YUDA 1:3].


Tutaligawa somo hili katika vipengele vitano:-


 ( 1 ).  UTANGULIZI KUHUSU SABATO.

 ( 2 ).  KUKOMESHWA KWA SABATO.

 ( 3 ).  SABATO, KIVULI CHA YESU KRISTO

 ( 4 ).  SABABU ZA WAKRISTO KUABUDU JUMAPILI

  ( 5 ).  KUSHIKA SIKU, SIYO NJIA YA KUOKOKA.


*1) UTANGULIZI KUHUSU SABATO*

*1. MAANA YA NENO SABATO.*

Neno “Sabato”, linatokana na neno la Kiebrania, “SHABBATH” ambalo maana yake ni PUMZIKO au KUSTAREHE NA KUACHA KAZI.

Pumziko hili siyo lazima liwe siku ya saba. Katika mazingira fulani watu waliagizwa kuwa na Sabato siku ya Kwanza na siku ya nane [MAMBO YA WALAWI 23:39], na pia walikuwa na Sabato siku ya saba kila wiki [KUTOKA 20:8-11].

Kulikuwa pia na Sabato ya mwaka mzima wa saba kwa ajili ya nchi. Haikuruhusiwa kulima nchi mwaka huo, ilitakiwa nchi istarehe au ipumzike [MAMBO YA WALAWI 25:2-5]. Awaye yote ambaye anadai leo kwamba anazingatia sheria kwa kushika sabato, imempasa kutokulima au kuvuna kila mwaka wa saba , au sivyo amekosa juu ya yote [YAKOBO 2:10]

*2. MWANZO MWA AGIZO LA KUSHIKA SABATO NA MAKUSUDI YAKE*

Agizo la kwanza kwa watu kuishika Sabato, lilitolewa na Mungu kwa Wanaisraeli, kwa mkono wa Musa,katika AGANO LA KALE. Agizo hili halikutolewa kwa Adam, Nuhu, Ibrahim, Isaka, Yakobo na Wengine kabla ya Musa [KUMBUKUMBU 5:1-3,12-14]. 

*Agizo hili pia, lilikuwa kwa TAIFA la Wanaisraeli tu!* Siyo mataifa mengine ambayo hayakupewa sheria [WARUMI 2:14; KUMBUKUMBU 4:7-10]. WANAISRAELI waliagizwa kushika sabato kwa makusudi yafuatayo:-  

( a ). Ili wapate kukumbuka jinsi walivyokuwa watumwa katika nchi ya Misri na ya kuwa BWANA Mungu aliwatoa utumwani na kuwapa PUMZIKO kutoka katika kazi hizo za utumwa [KUMBUKUMBU 5:15].

( b ). Ili ipate kuwa ISHARA ya Agano lao na Mungu, Agano la kale [KUTOKA 31:12-13,16-17; EZEKIELI 20:20]. *Agano hili linatajwa kuwa ni la “MILELE” siyo kwa maana kwamba lisilo na mwisho*. Siyo kila mahali katika Biblia “MILELE” ilipotumika, ina maana isiyo na mwisho. 

AGANO LA MILELE hapa lina maana Agano la muda mrefu sana ujao.[mifano: Nyumba ya kukaa itakayothibitishwa “milele” [WALAWI 25:29-30]; Mtu, kuwa mtumishi wa mtu “milele” [KUMBUKUMBU 15:12-17]; Ukoma wa “milele” [2WAFALME5:25-27].

*3. HUDUMA YA MAUTI ILIYOAMBATANANA       KUTOKUISHIKA SABATO.*

Agizo la kushika sabato,lilikuwa ni KONGWA zito. Mtu ambaye hakuishika sabato, alipewa huduma ya mauti, ALIUAWA {KUTOKA31:14-15, 35:2-3}. Hata mama aliyejaribu kukusanya kuni ili kuwapikia chakula wanawe siku ya sabato, alipigwa kwa mawe hata akafa [HESABU 15:32-36]. 

Mtu hakuruhusiwa kutembea kwa mwendo wa maili moja siku ya sabato. “Mwendo wa sabato” ulioruhusiwa ili mtu asihesabike amefanya kazi, ilikuwa chini kidogo ya maili MOJA kama mwendo wa kutoka Yerusaremu kwenda Mlima Mizeituni [MATENDO1:12]. 

Hata kujitwika godoro ilikuwa ni kuvunja sheria ya kushika Sabato [YOHANA 5:8-10]. 

Hata kuponya siku ya sabato ilikuwa ni kuivunja sheria ya kushika Sabato [LUKA 13:14]. 

Ilikuwa ni huduma ya adhabu, huduma ya mauti! [2WAKORINTHO 3:7-9]. 

*Wanafunzi wa Musa leo,* wanaojidai kwamba wanashika sabato, haiwapasi kwenda hospitali siku ya sabato, wala kutafuta kuponywa kwa njia yoyote siku ya sabato, tena miongoni mwao, asiyeishika sabato, wanatakiwa wamwue! Mbona hawayafanyi haya?

*( 2 ).  KUKOMESHWA KWA SABATO.*

Mwanadamu hakuumbwa kwa ajili ya sabato, bali kwa ajili ya Mungu aliye BWANA wa Sabato au mwanzilishi wa Sabato. Mungu ambaye ndiye aliyeleta agizo la kuishika Sabato, ana haki pia ya kuikomesha au kuiondoa agizo hilo na hakuna mwenye haki ya kumlaumu [MARKO 2:27-28]. 

Mapema katika unabii, kabla ya kuja Yesu Kristo, ilitabiriwa kwamba Mungu ataikomesha Sabato [HOSEA 2:11]. Yesu Kristo , alikuja kuitimiliza torati kwa kuikomesha Sabato.

Kiongozi wetu mkuu wa wokovu Yesu kristo, kwa wazi kabisa, alishindana na kila wazo la Wayahudi la kushika sabato. Alikuja kuikomesha Sabato kwa kuivunja. 

Ikiwa Yesu ni Bwana wetu ,sisi nasi tutakuwa mstari wa mbele kwa kumfuata yeye kama kielelezo na kuivunja Sabato [MARKO 2:23-28; LUKA 6:6-11; 13:10-16; 14:1-6; YOHANA 5:8,18; 9:13-16]. Yesu Kristo, aliigongomelea msalabani hati yakutushtaki kwa kutokuishika sabato, akaiondoa, isiwepo tena! [WAKOLOSAI 2:13-14]. 

*Kushika siku na miezi na nyakati na miaka, ni kuyarejea MAFUNDISHO YALIYO MANYONGE YENYE UPUNGUFU [WAGALATIA 4:9-11].*

Hatupaswi tena kuhukumiwa na mtu YEYOTE kwa sababu ya SABATO! [WAKOLOSAI 2:13-16]. Ili kupata tafsiri nzuri ya neno “Sabato” katika andiko hilo, soma Biblia ya Kiingereza, ya tafsiri ya King James Version inataja neon “SIKU ZA SABATO” au “SABBATH DAYS”. Nanukuu (COLOSIANS 2:16 ) “Let no man therefore judge you in meat, or in drink, or in respect of an holyday, or of the new moon, or of the Sabbath days”. Kwa hiyo, mtu awayeyote asituhukumu sisi kwa habari ya sabato za siku au siku ya sabato. 

Amri ya nne ya sabato katika zile Amri kumi, haipo katika Agano Jipya, Yesu wala mitume hawakutuagiza kushika Sabato [MATHAYO 19:16-19; MATENDO 15:1-29]. Kama wakati uliokuwapo kabla ya Musa, sisi nasi kama uzao wa Ibrahimu kwa imani, hatukuagizwa kushika sabato kama jinsi ambavyo hakuagizwa Ibrahimu!

Agizo Jipya, limekuwa badala ya Agano la Kale lenye upungufu, lililokuwa na huduma ya adhabu au ya mauti. *Huduma hiyo IMEBATILIWA [2WAKORINTHO 3:6-11; WAEBRANIA 8:6-9,13].*

*(3) SABATO , KIVULI CHA YESU KRISTO.*

Sabato, ilikuwa ni kivuli cha mambo yajayo [WAKOLOSAI 2:16-17].

Sabato, ilikuwa ni kivuli tu cha PUMZIKO ambalo wanadamu wasumbukao na kulemewa na mizigo wangelilipata kwa kumwendea, Yesu kristo [MATHAYO 11:28]. Baada ya kuja mwenyewe aliye PUMZIKO, Yesu kristo; hatuna haja tena ya kushika kivuli. Tukimshika Yesu kristo , YEYE Pia, atatupa SABATO ya milele huko mbinguni [WAEBRANIA 4:8-11]. Sabato hii siyo ya Jumamosi maana ni wale watakaofanya bidii kuingia raha hiyo na kuwa mbali na kumwasi Yesu watakaoingia [WAEBRANIA 4:1-11; UFUNUO 14:13]

*( 4 ). SABABU ZA WAKRISTO KUABUDU      JUMAPILI*

Hakuna andiko lolote katika agano jipya linalotupa kumbukumbu ya kusanyiko la Wakristo siku ya Sabato kwa ajili ya kumuabudu Mungu. 

Neno “Sabato” linaonekana mara 60 katika Agano Jipya. Mara 50 katika hizo, linatumika KABLA ya Agano Jipya lenyewe kufanywa kwa damu ya Yesu.Katika mara kumi zilizosalia, mara sita (6) linazungumzia Paulo akiwawahubiri WAYAHUDI kwenye makusanyiko YASIYO YA KIKRISTO kwenye sabato zao za kiyahudi [MATENDO 13:14, 42, 44; 17:1 ,2;18:4]. Mara mbili, neno hilo linaelezea juu ya sheria ya Musa isomwapo na Wayahudi katika masinagogi [MATENDO 13:27; 15:21]; Mara moja inaeleza jinsi tusivyopaswa kuhukumiwa katika Sabato [WAKOLOSAI 2:16]; Mara moja iliyosalia inataja juu ya mwendo wa sabato [MATENDO 1:12]. 

Siku ya JUMAPILI , ambayo ndiyo siku ya kwanza ya juma ,SIKU YA BWANA aliyoshinda mauti na kufufuka [UFUNUO 1:10], Tunaitenga maalum kumwabudu Bwana kwa sababu:-

( a ). Ni sikukuu ya malimbuko ya mavuno ambayo ilifanywa katika Agano la Kale, SIKU YA PILI baada ya Sabato; Ikiwa ni utabiri wa Kristo ambao ni LIMBUKO lao waliolala [WALAWI 23:9-14; 1WAKORINTHO 15:20].

( b ). Ni siku ya ushindi ya Bwana wetu Yesu aliyofufuka, na kujidhihirisha kwa wanafunzi wake baada ya kufufuka kwa Yesu [YOHANA 20:1,19,26 WARUMI 10:9].

( c ). Siku ya kuja Roho mtakatifu, Mwangalizi mkuu wa kazi yote ya Mungu katika kanisa, ilikuwa siku ya pentekoste ambayo ni Jumapili, siku ya pili baada ya sabato [MATENDO 2:1]

( d ) Siku ya Pentekoste Jumapili ndiyo siku ya kwanza ambayo kanisa la kwanza lilianza mahubiri na watu 3,000 wakaokoka na kuanza kusanyiko la kwanza la Ibada kanisani [MATENDO 2].

( e ). Wakristo wa kanisa la kwanza walikusanyika Jumapili [MATENDO 20:6-12;1WAKORINTHO 16:1-2].

*Sababu hizi zinadhihirisha pia wazi wazi kwamba kuabudu Jumapili hakukuanzishwa na mfalme CONSTANTINE wala kanisa Katoliki.*

Hakuna andiko lolote linalosema mtu yeyote anayeabudu Jumapili ana alama ya 666 ya mnyama. Huo ni uzushi. Biblia inatupa uhuru wote katika kuchagua siku ya kumwadhimisha Bwana [WARUMI14:5-6]. Vilevile ni muhimu kufahamu kuwa siku zote ni siku za kujifunza Neno [MATENDO 17:11;2:46].

*( 5 ). KUSHIKA SIKU, SIYO NJIA YA KUOKOKA*

Kushika siku yoyote hata iwe Jumapili, sio njia ya kuokoka.Tunaokolewa kwa kumuamini Yesu kuwa ni BWANA na MWOKOZI na sio kwa kushika siku yoyote [WARUMI 10:9-10,13].

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa.  Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Shalom

No comments:

WHY CHRISTIANITY IS BETTER THAN ISLAM?

Has Islam Improved to Become Better Than Christianity? Does Muhammad fulfill and complete the mission and purpose of Christ? Muhammad emphat...

TRENDING NOW