Baada ya kufahamu kuwa, kushika torati kunaambatana na Torati ya Musa “Sehemu ya Kumi”, sasa tuangalie, Je, Sabato ilikomeshwa?
Je, unafahamu kuwa agizo la kushika siku ya sabato na torati yote kwa ujumla, ilikuwa ni huduma ya mauti au huduma ya adhabu ya kifo?
Siandiki mada hii kuhusu “SABATO” kwa sababu napenda kushindana na watu! La hasha! Kwa upande moja, napenda kuondoa utata juu ya mada hii. Kwa upande mwingine, inanihuzunisha sana na nasikia uchungu kuona watu na au Wakristo wenye nia njema tu ya kufanya mema, lakini wanatumia njia au sheria ambayo haina nguvu na ni kivuli tu, huku tukiwa na Yesu ambaye ndie Bwana wa Sabato.
UTHIBITISHO:
Katika kitabu cha 2 Wakorintho 3:7-8 tunasoma, “Basi, ikiwa huduma ya mauti iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika. Je huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu?”
Kwa hiyo torati yote ikiwemo kushika sabato, ilikuwa ni huduma ya mauti. Pia torati haikuwa huduma ya mauti tu, bali ilikuwa ni nguvu za dhambi, kama maandiko yanavyosema katika kitabu cha 1 Wakorintho 15:56, “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati.”
Kwa kadiri unavyozidi kuifuata torati ndivyo nguvu ya dhambi inavyozidi, kwa kuwa torati kazi yake ni kubaini makosa. Haina tofauti na darubini ya kupima vijidudu vya magonjwa. Kwa vile torati ilikwisha tolewa katika agano la kale na imetufanya kujua dhambi nini; hivyo katika agano jipya, haupaswi tena kuifuata torati, bali tunapaswa kuifuata dawa ya dhambi, ambayo ni Bwana wetu Yesu Kristu.
UTHIBITISHO:
Warumi 8:2 Biblia inasema, “Kwa sababu sheria ya Roho ya uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.”
Kwa ujumla ni kwamba, torati ilikuwa ni huduma ya mauti, kwa kuwa sheria walizoshindwa kuzifuata Wana wa Israeli, iliwalazimu kuuawa. Watu wengi walikufa kwa nguvu ya torati; mfano mtu ambaye hakushika sabato aliuawa (Kutoka 31:14-15; Kutoka 35:2-3).
Mtu aliye jaribu kukusanya kuni siku ya sabato kwa kusudi la kujipikia chakula aliuawa (Hesabu 15:32-36).
Watu wagonjwa hawakutakiwa kutibiwa siku ya sabato hivyo kusababisha watu wengi kufa (Luka 13:14), kitu ambacho si mpango wa Mungu.
KUMBE HATA WAISRAELI WALISHINDWA KUISHIKA TORATI
Hata hivyo, pamoja na torati kuwa ni huduma ya mauti, pia Wana wa Israeli wenyewe, hawakuweza kudumu katika lile agano la kwanza walilofanya na Mungu, hivyo kufanya agano hilo, kutofanikiwa;
UTHIBITISHO:
Yohana 7:19 tunasoma, “Je! Musa hakuwapa torati? Wala hakuna mmoja wenu aitendaye torati.”
KWANINI AGANO HUVUNJWA AU VUNJIKA?