Biblia Takatifu inatuambia kwamba:
“...tuliumbwa katika Kristo Yesu...” (Waefeso 2:10)
Ni jambo lililo wazi kabisa kuwa sisi wanadamu wote pamoja na viumbe vyote ni kazi ya mikono ya Yesu. Yesu ameumba vitu vyote; tendo la mtu kuukana Uungu wa Yesu ni jambo la kumkosea heshima Mungu aliyekuumba. Ndio maana Yesu aliwaambia Wayahudi kwamba: “...ninyi mwanivunjia heshima Yangu...” (Yohana 8:49).
Tusomapo Biblia Takatifu katika kitabu cha YOHANA sura ya kwanza, tunaona pameandikwa:
“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu... Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo Yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika... Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu Wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” (Yohana 1:1,3,14)
Huyo “Neno” anayetajwa hapo ndiye Yesu Kristo. Mwandishi wa kitabu hicho cha YOHANA ametumia usemi wa: “...Neno alikuwako kwa Mungu...” akiwa anawafahamisha hususani Wayahudi waliokuwa wanajua kuwa YEHOVA ndiye Mungu wao. Kwa hiyo Yohana anasema “...Neno alikuako kwa Mungu...” kwa maana ya kwamba; huyu “...Yesu alikuwako kwa YEHOVA...” ambaye wao Wayahudi walimtambua kuwa ndiye Mungu wao.
Pia zaidi tunaona Yohana anafafanua kwa kusema kuwa; huyu “...Yesu alikuwa Mungu...” Ufafanuzi zaidi tunauona katika YOHANA 1:14 ambapo Yohana amefafanua kwa kusema; “...Yesu alifanyika mwili; akakaa kwetu...” Biblia Takatifu inamtaja kwa wazi kabisa kuwa Yesu ni Mungu na ameumba vitu vyote “...Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo Yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika...” (Yohana 1:3).
No comments:
Post a Comment