Sunday, August 16, 2015

BIBLIA INAWEZA KUAMINIWA NA KUTEGEMEWA
Kimsingi mwanadamu anaweza kumfikiria Mungu kwa njia kuu mbili: Njia ya kwanza ni ile ya kuongozwa na mawazo yake mwenyewe na ya pili, ni ile ya kuongozwa na ufunuo kutoka kwa Mungu. Kujaribu kumfahamu Mungu kupitia njia ya kwanza kwa kiwango kikubwa ndiko kulikochangia kuzaliwa kwa dini nyingi pamoja na vikundi mbalimbali vya imani za uongo. Dini na imani zote hizi zilianza na juhudi za wanadamu kutaka kumjua na kumfikia Mungu kwa nguvu na akili za kibindamu. Hata hivyo kumfikia Mungu kupitia ufunuo kutoka kwa Mungu, ndiyo njia ya pekee iliyo sahihi katika kumjua na kumfikia Mungu. Ukweli huu ndio unaoifanya imani ya Kikristo kutofautiana na dini zingine zilizopo duniani.

Kujaribu kumfikia Mungu kwa kutumia nguvu na akili za kibinadamu kunatukumbusha vitabu viwili vilivyoandikwa na mwanafalsafa mashuhuri wa zamani wa Kiyunani aliyejulikana kama Aristotele. Kimoja kati ya vitabu hivyo alikiandika kwa ajili ya watu wa kawaida na kile cha pili alikiandika kwa wasomi waliofundishwa kupambanua mambo. Hivi ndivyo kazi ya Mungu ilivyo, mwanadamu anaweza kuchagua kumfahamu Mungu kwa kutumia akili na pia anaweza kumfahamu kwa njia ya ufunuo unaopatikana katika Biblia. Watu wanaomtafuta Mungu kwa njia hii ya pili, ndio wanaofanikiwa kumwona na kumwamini.

Kitabu hiki cha zamani ni chenye mvuto wa kushangaza. Kilichukua takribani miaka 1600 kuandikwa hivyo kukifanya kuwa kitabu pekee kilichokuwa muda mrefu kuandikwa kuliko vitabu vyote vilivyopo chini ya jua. Kimeundwa na vitabu 66, vilivyoandikwa na zaidi ya waandishi hamsini. Waandishi hawa waliokuwa wanatofautiana katika umri, kazi, vyeo, hadhi na elimu. Wengi katika waandishi hawa walikuwa hawajuani, walitoka katika nchi tofauti na kuzungumza lugha tofauti. Mawazo ya waandishi hawa yanaweza kuelezewa kwa kutumia wazo kuu moja ambalo ni, “mpango wa Mungu kuhusu ukombozi wa wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo pekee ambaye pia ni Bwana wetu.” Pasipo shaka yoyote kitabu hiki kimebeba sifa za kipekee zinazokifanya kisifananishwe na kitabu kingine chochote. Kimetafsiriwa kwa lugha na lahaja zaidi ya 4000 zikijumuisha lugha ya ‘breli’ inayotumiwa na vipofu. Kila mwaka nakala milioni 60 za Biblia au sehemu ya Biblia zinachapishwa duniani kote, hivyo kukifanya kuwa kitabu kinachoongoza kimauzo. Sambamba na kuongoza kiuchapishaji, kinaongoza duniani kwa kuenea ambapo kimefikia zaidi ya nusu wa wanadamu duniani.

Takwimu za usambazaji wa vitabu zinaonyesha kuwa miongoni mwa vitabu vinavyochapishwa na kusambazwa, asilimia tano tu ya vitabu hivyo ndivyo vinavyouzwa baada ya miaka saba. Hakika Biblia ni Neno la Mungu linalodumu na lisilotikiswa na chochote. Biblia ni msingi wa utamaduni wa kibinadamu na haipingani na sayansi kama baadhi ya watu wanavyofikiria. Ni kitabu kinachogeuza maadili ya jamii kutokana na ukweli kuwa, kinambadilisha mwanadamu. Wakati uliopita mtu mmoja asiyeamini kuwepo kwa Mungu alitembelea visiwa vya Fiji na kumwambia kiongozi mmoja wa kijadi maneno yafuatayo: “Wewe ni ‘chifu’ mkubwa, ila nimesika kuona kuwa wewe na watu wako mmekubali kubadilishwa na wamishenari kuwa Wakristo.” Baada ya kusikia maneno ya mtu huyu, kiongozi huyu wa jamii moja huko Fiji alimwonyesha jiwe kubwa na kumwambia, “Kabla ya kuja kwa wamishenari waliotuletea Biblia, tulitoa kafara za wanadamu kwa miungu kwa kubamiza vichwa vyao hadi kufa juu ya jiwe hili. Walipokufa tulibanika minofu yao juu ya moto na kuila. Kama Biblia isingetufikia na kuondoa ushenzi wetu, wewe usingerudi nyumbani kwako. Kama Injili isingetufikia, ambayo wewe unaidharau na kuikebehi, tungekukata vipande na kuila nyama yako. Biblia ni silaha yenye nguvu dhidi ya maovu ya aina zote.”

Mtu mmoja alimzawadia mtoto wake Biblia na kuandika ndani yake maneno yafuatayo: “Mwanangu, ama Kitabu hiki kitakuzuia kutenda dhambi, au dhambi itakuzuia kukisoma.” Nguvu ya kubadilisha inayopatikana katika kitabu hiki ndiyo inayokifanya kipingwe na kupigwa vita kupita vitabu vyote na wakati huo huo kuongoza kwa kupendwa duniani. Kwa maneno mengine, kitabu hiki kinashambuliwa na wakati huo huo kusifiwa. Biblia ndicho kitabu kipekee kitokacho kwa Mungu, chenye mafundisho yaliyo hai na yasiyo na makosa. Uwezo wake unadhihirisha usahihi wa maudhui yake.

Ndani ya Biblia kuna kweli zinazoeleweka kirahisi, na pia ziko kweli zingine ambazo wanadamu kutokana na ubinadamu wao, wanashindwa kuzielewa. 

Wakati fulani mpinzani mmoja wa Biblia alimweleza mwandishi mmoja wa habari ndugu Mark Twain kuwa, anasumbuka kutokana na kutoelewa mambo mengi yaliyoandikwa katika Biblia. Ndugu Mark Twain naye akamjibu kwa kusema, “ndugu yangu, mimi ninasumbuliwa na mambo ambayo nimekutana nayo katika Biblia na kuyaelewa!”

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW