Wednesday, January 10, 2018

KWANINI YESU KRISTO ALIBATIZWA?


Kubatiza katika Kigiriki ni Baptizein maana yake “To immerse, kuzamisha” Ndiyo maana zamani walibatiza kwa kumzamisha mtu katika maji.

Wapendwa Wanafamilia ya Mungu, tunafahamu kuwa Wakristo tuna batizwa kwasababu tunazaliwa katika hali ya dhambi na tunaishi katika hali dhambi. Tunapobatizwa dhambi zetu zinaondolewa nasi tunabaki wasafi. Lakini kumbuka kuwa Mungu pekee ndiye awezaye kutuondolea dhambi zetu tunapomwamini Yesu Kristo na kuziacha dhambi zetu.

Huduma ya Yesu ilianza pale alipobatizwa na Yohana. Hili limeelezwa vizuri katika Mathayo 3:13-17 na katika Luka 3:21-22.

Kwa asili makanisa yanachukulia kubatizwa kuwa ni ishara kuosha na kuondoa dhambi, kama ilivyoandikwa katika Matendo ya Mitume 22:16, ambapo Anania anamwambia Paulo: Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako. Katika makanisa yanayotekeleza ubatizo kwa muumini ishara hii ina nguvu sana: mbatizwaji huzamishwa majini kama ushuhuda wa wazi wa imani.

Kama ubatizo ni hitaji la kukiri dhambi na kuondolewa dhambi, Je, ni kwanini Yesu Kristo alibatizwa?

Kwetu Wakristo, Ubatizo huondoa dhambi ya asili na kutuingiza katika maisha ya Umungu ukitufanya watoto wa Mungu wanajumuiya wa Kanisa. Kristo hakuwa na dhambi. Hivyo, kimsingi Yesu Kristo hakuhitaji ubatizo. Lakini, alikubali kubatizwa. Kwa nini?

YESU KRISTO ALIBATIZWA ILI KUJIDHIHIRISHA KUWA NI MWANA WA MUNGU.

Matukio matatu: Epifania, Ubatizo na Kugeuza maji kuwa divai huko Kana ya Galilaya yanaeleweka kuwa ni matukio matatu ambayo Yesu Kristo aliyafanya ili kujidhihirisha kwa ulimwengu kuwa yeye ni Mungu.

Amebatizwa ili aonyeshe kuwa uaguzi wa Nabii Isaya umetima:
“Kisha utukufu wa Mungu utafunuliwa na watu wote pamoja watauona”.

Isaya ameongeza kusema:
“Paza sauti yako bila kuogopa; iambie miji ya Yuda ‘Mungu wenu anakuja’”

Ili kudhibitisha hayo sauti ya Mungu Baba inasikika ikitwambia
“ Huyu ni mwanangu mpendwa wangu” (Injili)

Kuanzia kesho tutazidi kuona Yesu Kristo akionyesha kuwa ni Mungu kwa kuyatimiza aliyoagua Nabii Isaya.

“Bwana Mungu anakuja kwa nguvu; kwa mkono wake anatawala; atalilisha kundi lake…”

Hivyo, Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu. Yesu Kristo ni Mungu.
YESU KRISTO ALIBATIZWA ILI KUTHIBITISHA UBATIZO WA YOHANA

Ubatizo wa Yohana ulikuwa ni wito kwa watu kubadili maisha yao na kumtafuta Mungu.
“Sauti ya Mtu anaita jangwani: Mtayarishieni Mungu njia”

Wengi hawakumwelewa Yohana hata wengine waliona shaka juu ya Ubatizo wake.

“Watu walipokuwa wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohana, kama labda yeye ndiye Kristo….”

Yesu Kristo anakubali kubatizwa ili kuonyesha kuwa wito wa Yohana na ubatizo wake ni muhimu sana.

“Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa” (Injili).

Anawaonyesha watu kuwa ni lazima kubadilika na kumtafuta Mungu katika maisha yao.

Ndiyo maana Yesu alianza na wito huhuo.

“Ufalme wa Mungu umekaribia tubuni na kuiamini Injili”(Marko 1:15).

Yesu Kristo alibatizwa ili ajiunge na wadhambi na awaokoe.
Mtu anapokubali kubatizwa anakiri kuwa yeye ni mdhambi na anaomba msamaha.

Hivyo, Kristu anapokubali kubatizwa anakubali kujiunga na wadhambi, ili pamoja nao awaombee msamaha na kuwasaidia kuanza maisha mapya.
Nabii Isaya ameagua akisema
“Wafarijini watu wangu, …waambie kwamba wamesamehewa uovu wao”.

Mt. Paulo anaonyesha kuwa Yesu ametimiza uaguzi huo
“Alijitoa yeye mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe”.

Ndiyo maana Mt. Petro anasema
“Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake” (1Petro 2:24).

Kwa hiyo katika Yesu ubinadamu umebatizwa. Ubinadamu unazamishwa katika maji na kuinuliwa tukiwa watu.
“Watu walio na hamu ya kutenda mema.”

Kwa hiyo, Yesu alibatizwa ili ubinadamu ubatizwe.

Kristo alibatizwa ili kuupatia maana ubatizo wetu
Mtu angeuliza.

“Kama katika Yesu ubinadamu wote umebatizwa kama tulivyoona hapo juu ina maana gani sisi kubatizwa tena”


KAMA YESU ASINGE BATIZWA, BASI UBATIZO WETU USINGE KUWA NA MAANA.

Kusema Yesu asingebatizwa ni sawasawa na kusema Yesu asingekufa.

Yesu asingekufa na kufufuka ubatizo wetu usingekuwa na maana yoyote.
“Kama Kristo hakufufuka, Imani yenu ni bure, mgalimo katika dhambi zenu”(1 Wakorintho 15:17).

Ndiyo maana Mt. Paulo anatwambia kuwa kwa ubatizo tunashiriki kifo na ufufuko wa Kristo.
“Tulipobatizwa tuliungana na kifo chake, tukazikwa pamoja naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka wafu, sisi nasi tuweze kuishi maisha mapya”(Rumi 6:4).

Hivyo, lazima tubatizwe mmoja mmoja ili kushiriki binafsi kile Kristu alichofanyia ubinadamu wote alipobatizwa.
Alibatizwa ili kuashiria msalaba na kuanza rasmi kazi ya Ukombozi

Ili kuelewa jambo hili lazima tuelewe maana ya neno “Kubatiza” na ni lini Kristu alibatizwa.

Kubatiza katika Kigiriki ni Baptizein maana yake “To immerse, kuzamisha” Ndiyo maana zamani walibatiza kwa kumzamisha mtu katika maji.

Kwa hiyo, kwa kubatizwa, Kristu amejizamisha (has immersed himself) katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu atakayoikamilisha kwa kufa msalabani.

Hivyo, kwa kubatizwa Yesu anaanza kufa na atakamilisha kifo chake hapo msalabani
Ndiyo maana Kristu aliwauliza wana wa Zebedayo
“Je, mwaweza kubatizwa ubatizo nitakaobatizwa mimi?” (Marko 10:38).

Alitaka kuwaonyesha kuwa kifo chake ni ubatizo ambao ameuanza leo katika mto Yordani.
YESU ALIBATIZWA ILI BABA YAKE AMWIMARISHE KWA KAZI ANAYO IANAZA.

Yesu alibatizwa akiwa na umri takribani miaka 30 alipoanza kazi rasmi na wazi ya ukombozi.
Kama mwanadamu alikuwa anogopa kwa sababu kama Mungu alijua kuwa atakufa Msalabani.

Hivyo, Baba yake anajitokeza
“Wewe ni Mwanangu mpendwa wangu nimependezwa nawe (kwa uamuzi huo). Usiogope mwanangu. Hii njia uliyoichagua ndiyo yenyewe ili uwarudishe kwangu watu waliopotea”

Aidha, Roho Mtakatifu alimtia mafuta, kumtakasa na kumtuma awatangazie maskini habari njema.

“Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili kama hua” (Injili).

Ndiyo maana anapoanza kazi yake anasema:

“Roho wa Bwana yu juu yangu; amenitia mafuta ili niwatangazie maskini habari njema” (Luka 4:18).

Hivyo, leo amebatizwa ili atiwe nguvu na kuimairishwa kwa kazi ya ukombozi anayoianza.

Yesu Kristo alibatizwa ili kuyatakasa maji ya ubatizo wetu.
Tangu sasa maji hayatakuwa tena kitu cha kuwaangamiza watu bali kuwaokoa watu kwa kuwaondolea dhambi zao.

Katika enzi za Noa maji ya gharika (mafuriko) yaliwauwa watu na viumbe vyote katika uso wa nchi isipokuwa Noa na wale tu alioingia nao katika safina.

Hivyo, Kristo aliyatakasa maji yasiwaangamize tena watu bali yawaokoe.

Kwa kufanaya hivyo, alitimiza agano Mungu alilofanya na Noa akisema,

“Ninaweka agano langu nanyi…kwamba kamwe viumbe vyote hai havitaangamizwa kwa gharika, wala haitatokea tena gharika kuiharibu nchi” (Mwanzo 9:9,11).

Kristo alibatizwa ili atutangulie katika safari yetu ya wokovu.
Kwa ubatizo tunaanza safari ya wokovu kuelekea mbinguni.
Mungu aliwaongoza Waisraeli katika safari yao kutoka Misri kuelekea nchi ya ahadi ili awaonyeshe njia.
Walipokaribia bahari ya Shamu Mungu katika ishara ya nguzo ya moto na wingu aliingia kwanza katika maji ya bahari ya Shamu; na Waisraeli kwa kumfuata, waliweza kuvuka bahari kwa usalama na maadui wao wakazamisha katika maji ya bahari.

Leo, Kristo anatutangulia katika maji ya ubatizo ili awe mwanga wetu wa kutuangazia katika bahari hii ya maisha, ili tuweze kusafiri salama na kumshinda adui yetu shetani.

Ndiyo maana Mungu anatualika akisema “msikilizeni yeye.” Ni kana kwamba anasema, “mkitaka kuvuka salama hii bahari ya ulimwengu, ‘msikilizeni mwanangu, atawaelekeza.’”

Basi, Yesu awe wingu letu wakati wa mchana na nguzo ya moto wakati wa usiku ili tuweze kuvuka salama hii bahari ya maisha.

2. Wajibu wetu kama Wabatizwa

a) Tudumu watoto wapendwa wa Mungu

“Wewe ni Mwanangu Mpedwa Wangu”

Tunapobatizwa haya maneno yanasemwa juu yetu
“Wewe ni Mwanangu Mpedwa wangu”

Tunakuwa watoto wa Mungu
“wale waliompokea ndio wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu” (Yohana 1:12).

Je, bado tu wana wa Mungu?
Je, bado tu wana wapendwa wa Mungu?
Je, bado Mungu anapendezwa nasi?

Alipendezwa na Yesu kwa sababu alimtii hata alipomwambia kufa msalabani

Je, sisi ni wana watiifu kwa Mungu?

Basi tudumu kuwa watoto wa Mungu.

Mtoto wa nyoka ni nyoka basi mtoto wa Mungu ni Mungu
Nyoka ana roho ya nyoka mtoto wa Mungu na Roho wa Mungu aliaye Abba yaani Baba. Kwa hiyo, yatubidi tuishi kama watoto wa Mungu
b) Tushike maagano yetu ya Ubatizo

Tuzidi kumkataa shetani na tamaa zake ambazo leo tumezizamisha katika maji ya Yordani.

Mt. Paulo ametwambia

“Maana neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Neema hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi maisha adili nay a kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa, … tuwe watu wake mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda mema” (Somo II).

c) Tutangaze Imani yetu kwa kuishi upendo

“Nenda juu ya mlima mrefu ewe Siyoni, utangaze habari njema. Paza sauti yako bila kuogopa. Wafarijini watu wangu”

Tumsaidie Kristo katika kazi ya ukombozi
Tuishi kama ndugu kwa sababu sisi sote ni watoto wa Mungu
Tudhihirishe ubatizo wetu kwa njia ya maisha yetu.

Watu watutambue kwa matendo yetu kuwa tumebatizwa.

Shalom,

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW