Monday, March 18, 2019

INJILI YA BARNABA

No photo description available.
Beleshi Linalochota Waislamu na Kuwatupia Kwenye Shimo la Kuzimu
Ulimwengu wa Kiislamu, kama kawaida yake, unatia juhudi kubwa sana katika kuuchafua Ukristo ili angalau uweze kuendelea kuwashikilia walio ndani yake; na pale inapowezekana, kuwadanganya Wakristo wasiojua Ukristo wala Uislamu.
Kuna mambo mawili makubwa ambayo huwa yananishangaza sana kuhusiana na masuala ya kiroho. Kwanza ni jinsi ambavyo wakuu wa dini wa Kanisa Katoliki wanavyotumia miaka na miaka kusomea dini na Biblia, kisha wanakuja kuishia kufundisha mambo yaliyo nje ya Biblia!!! Kwa mfano, wanawaambia waumini wao kuwa wafu wanatuombea kule mbinguni au kwamba unaweza kufanya misa huku duniani halafu ndugu yako aliyekufa akiwa na dhambi na, kwa ridhaa yake alikataa wokovu, eti atasamehewa dhambi na Mungu atamuingiza mbinguni!!!
Jambo la pili linalonishangaza sana ni kitendo cha Uislamu na Waislamu kutumia uongo kwa juhudi kubwa sana ili kutetea dini yao na kuwafanya waumini wao waendelee kubakia kwenye Uislamu.
Kama dini yenyewe haiwezi kujitetea kwa njia ya neno inalolihubiri, bali inabidi uisaidie kusimama kwa kutumia uongo, kwa nini basi unaitetea? Na kwa nini hasa unaiamini?
Siwashangai wale wasioelewa, lakini nawashangaa wale wanaojua kuwa, “Hapa ninasema uongo ili kumtetea Allah!” Yaani, wanafanya makusudi kusema uongo kwa lengo la kumtetea Mungu ambaye tunatarajia na tunaamini kuwa ana uwezo wote!!!!
Ama kweli duniani kuna mambo!!!
Nikirudi sasa kwenye mada ya leo, mojawapo ya silaha za uongo inayotumiwa na Waislamu kwa lengo la kuinua dini yao ni kusambaza na kuhubiri kile kinachojulikana kama “Injili ya Barnaba.”
Injili ya Barnaba ni nini?
Hiki ni kitabu kikubwa (karibu sawa na injili zote nne za Biblia zikijumuishwa pamoja - maana kina sura 222). Kitabu hili kinaeleza maisha ya Yesu na kudai kwamba kimeandikwa na mmoja wa mitume wa Yesu aliyeitwa Barnaba.
Nakala za zamani kabisa za kitabu hiki ambazo zinajulikana ni mbili – moja kwa Kiitaliano na nyingine kwa Kihispania. Zote zinaonyesha kuwa ziliandikwa kwenye karne ya 15 au 16 baada ya Kristo.
Kwa nini injili ya Barnaba ni ya bandia?
Unaposoma injili hii, unagundua kuwa ni ‘forgery’ au ni ya bandia kutokana na sababu mbalimbali. Baadhi ya sababu ziko wazi lakini zingine zinahitaji jicho la karibu zaidi ili kuzitambua.
Zifuatazo ni baadhi ya sababu hizo:
1. Mwanzoni tu mwa injili hii, Yesu anaitwa ‘Kristo’ (Christ). Imeandikwa: “Dearly beloved the great and wonderful God hath during these past days visited us by his prophet Jesus Christ …” Lakini unavyoendelea kusoma unakuta kwamba Yesu anakataa kwamba yeye si ‘Masihi’. Kwa mfano, katika sura ya 42 imaendikwa: Jesus confessed, and said the truth: "I am not the Messiah."
Neno ‘Kristo’ (Christ) ni tafsiri ya Kigiriki ya neno la Kiebrania ‘masihi’ (Messiah). Kwa hiyo, Kristo na Masihi ni neno lilelile. Licha ya hivyo, katika maisha yao yote, Wayahudi walikuwa wakimtarajia Masihi. Hivyo, hili lisingekuwa ni neno geni kwao kiasi cha kumfanya mwandishi ashindwe kulielewa.
Mbali na hayo, Barnaba halisi anayejulikana kwenye Biblia aliishi kwenye kisiwa cha Kipro (Cyprus) ambako wenyeji wake walizungumza Kigiriki. Na Barnaba mwenyewe alikuwa ni Mwebrania. Kwa hiyo, asingeweza kamwe kushindwa kuelewa kuwa maneno haya yanabeba maana ileile katika lugha mbili tofauti ambazo alizizungumza zote.
Kwa hiyo, huu ni ushahidi kwamba mwandishi wa Injili ya Barnaba ni mtu ambaye hakujua Kigiriki ndiyo maana mwanzoni tu mwa injili yake hii anamwita Yesu ni Christ, ilhali ndani anamfanya Yesu aseme kuwa yeye si Messiah!
2. Quran inasema kwamba Yesu ni Masihi. (Tazama Sura 3:45). Na Biblia nayo inasema kuwa Yesu ni Masihi. Kama wewe Mwislamu unaamini kuwa Quran ni kitabu cha kweli; na kwamba kile inachokisema ni kweli, iweje basi uamini injili ya Barnaba inayosema kuwa Yesu si Masihi na usiamini Biblia inayosema kuwa Yesu ni Masihi kama ambavyo Quran yako inasema?
3. Katika sura ya 3, ‘barnaba’ huyu anatuambia kuwa Herode na Pilato walitawala Yudea wakati Yesu alipozaliwa. There reigned at that time in Judaea Herod, by decree of Caesar Augustus, and Pilate was governor in the priesthood of Annas and Caiaphas. Wherefore, by decree of Augustus, all the world was enrolled; wherefore each one went to his own country, and they presented themselves by their own tribes to be enrolled. Joseph accordingly departed from Nazareth, a city of Galilee, with Mary his wife, great with child, to go to Bethlehem (for that it was his city, he being of the lineage of David), in order that he might be enrolled according to the decree of Caesar…….. While Joseph abode there the days were fulfilled for Mary to bring forth.
Herode alitawala Israeli kati ya mwaka 37-4 kabla ya Kristo. Unaweza kusoma HAPA au kwingineko kokote. Lakini Pilato alitawala miaka zaidi ya ishirini baadaye, yaani kati ya 26-36 baada ya Kristo. Unaweza kusoma HAPA. Sasa, kwa kuwa Barnaba aliishi pamoja na Yesu, wakati ambapo Pilato alikuwa mtawala, inawezekanaje akafanya kosa lililo wazi kama hili? Hili ni kosa linaloweza tu kufanywa na mwandishi ambaye hakuishi nyakati za Yesu au nyakati za Pilato.
4. Katika sura ya 20 tunaambiwa na ‘barnaba’ kwamba Yesu alisafiri baharini kutoka Galilaya hadi Nazareti. Imeandikwa: Jesus went to the sea of Galilee, and having embarked in a ship sailed to his city of Nazareth. Hebu tafuta Nazarethi kwenye ramani HAPA, kisha uangalie kama mtu anaweza kusafiri kwa chombo cha majini kutoka kwenye Bahari ya Galilaya hadi Nazarethi.
Nazarethi iko kilometa takriban 14 kutoka Bahari ya Galilaya. Ni mtume gani wa Yesu angeweza kusema jambo kama hili – ukichukulia kwamba Yesu na mitume wake walikuwa wakitembea sana kwenye maeneo haya? Hii inaonyesha tu kwamba mwandishi wa injili ya Barnaba hajui jiografia ya Nazarethi au Galilaya.
5. Yehova aliagiza kwenye Biblia kwamba watu washerehekee mwaka wa Yubile kila baada ya miaka 50. Imeandikwa: Na mwaka wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa mahuru katika nchi yote kwa watu wote wanayokaa; itakuwa ni yubile. Mwaka huo wa hamsini utakuwa ni yubile kwenu; msipande mbegu, wala msivune kitu hicho kimeacho chenyewe, wala msizitunde zabibu za mizabibu isiyopelewa (Walawi 25:10-11).
Mwaka 1300 B.K, papa Boniface VIII alitangaza kimakosa kuwa Wakristo wanatakiwa washerehekee siku hiyo kila baada ya miaka 100. Lakini, mwaka 1350 B.K, papa aliyefuata, yaani Clement VI, alirudisha utaratibu wa kawaida wa kusherehekea yubile kila baada ya miaka 50. Kwa hiyo, kwa kipindi cha miaka 50, yaani kuanzia 1300 hadi 1350, watu walikuwa wakijua kwamba yubile inasherehekewa kila baada ya miaka 100. Soma HAPA.
Na huyu mwandishi wa Injili ya Barnaba kwenye sura ya 82, anamwekea Yesu maneno mdomoni kwamba eti alisema: “insomuch that the year of jubilee, which now comes every hundred years, shall by the Messiah be reduced to every year in every place."
Hivi, kama ukiona sinema ambayo mtu anakwambia hii ni ya mwaka 1910, na inaonyesha watu wamevaa mavazi ya zamani na nyumba ni za zamani, lakini humo ndani kwa nyuma ukaona bendera ya taifa la Tanzania inapepea utawaza nini?
Kihistoria inajulikana kabisa kwamba bendera hiyo haikuwapo mwaka 1910. Maana ya kuwapo kwake kwenye sinema hiyo ni moja tu – kwamba hiyo ni sinema ya uongo!
Sasa, suala la yubile ya kila miaka 100, kwa mara ya kwanza, lilikuja mwaka 1300. Halafu waislamu mnataka kuwaambia watu kuwa injili ya Barnaba iliandikwa na mtume aliyeishi na Yesu kwenye karne ya Kwanza, yaani miaka 1300 kabla ya jambo hili linalohusiana na yubile ya kila miaka 100 kutokea. Au huyu mheshimiwa 'barnaba' alikuwa anaongea kinabii?
Kwa msomaji unayependa KWELI, hili linakuonyesha kitu gani? Bila shaka jibu liko wazi kwamba mwandishi wa injili hii aliishii baada ya mwaka 1300. Amka!!!
Barnaba wa karne ya 1 asingeweza kamwe kuandika au kusema jambo kama hili; na zaidi ya yote Yesu…?!
6. Katika sura ya 178, injili ya Barnaba inatuambia kuwa ili ufike paradiso ni lazima uvuke mbingu 9. Ikimaanisha kuwa, paradiso ni ya kumi. Imeandikwa: Truly I say to you that the heavens are nine, ……. And truly I say to you that paradise is greater than all the earth and all the heavens together.
Katika karne ya 14 kule Italia kulikuwa na mshairi maarufu aliyeitwa Dante Alighieri. Katika mojawapo ya vitabu vyake, Dante anazungumzia jambo hilihili. Yaani anasema kuwa ili kufika paradiso unatakiwa kuvuka mbingu tisa!!! Unaweza kusoma HAPA.
Na inajulikana, kama nilivyosema mwanzo wa makala haya kuwa, nakala za zamani kabisa zinazojulikana za injili ya Barnaba ni mbili – moja ya Kiitaliano na nyingine ya Kihispania. Na hizi zinajulikana kuwa ni za kwenye takriban karne ileile ya Dante. Waswahili wanasema, mwenye macho haambiwi tazama!!
7. Sura ya 193 ya Injili ya Barnaba inaongelea juu ya kifo cha Lazaro ambaye alifufuliwa na Yesu. Kisha Yesu anasema kuwa saa yake (ya kufa) ikifika naye atalala vilevile kama Lazaro na atafufuliwa mara moja. Imeandikwa: 'My hour is not yet come; but when it shall come I shall sleep in like manner, and shall be speedily awakened.'
Lakini unapofika kwenye sura ya 216 na 217, wakati ambapo Yesu amekamatwa ili auawe, tunaambiwa kuwa Mungu alimwondoa kimiujiza (kama Quran inavyosema) na badala yake mungu huyu (anayeonekana kuwa ni mwongo) akamvika Yuda sura ya Yesu na Yuda akauawa kwa kuwa watu waliomjia Yesu walidhani kuwa Yuda ndiye Yesu.
Swali ni kuwa, je, si Yesu katika sura ya 193 ndiye aliyesema kwamba angekufa na kufufuliwa? Mbona basi Mungu anamkimbiza na kumficha badala ya kutimiza lile ambalo Yesu alilisema?
Mwenye macho haambiwi tazama!!
8. Sura ya 54 inasema kuwa mafarisayo walikuwapo wakati wa nabii Eliya. Lakini historia inaonyesha kuwa Mafarisayo walitokea kuanzia karne ya pili kabla ya Kristo. Soma HAPA au kwingineko.
Lakini nabii Eliya aliishi kwenye karne ya 9 kabla ya Kristo. Soma HAPA. Hiyo ina maana kuwa aliishi takriban karne 7 kabla mafarisayo hawajatoke. Sasa iweje huyu barnaba atuambie kuwa mafarisayo walikuwapo nyakati za Eliya?
9. Sura ya 80 inatumbia kwamba Danieli alichukuliwa na Nebukadreza kupelekwa Babeli akiwa na miaka miwili. Imeandikwa: Daniel as a child, with Ananias, Azarias, and Misael, were taken captive by Nebuchadnezzar in such wise that they were but two years old when they were taken; and they were nurtured among the multitude of idolatrous servants.
Unaposoma Biblia inatuambia kwamba: Hata katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadreza, Nebukadreza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, usingizi wake ukamwacha. (Dan. 2:1).
Matokeo yake Nebukadreza alitaka waganga na wataalamu wa kutafsiri ndoto wamwambie maana ya ndoto ile. Kila mmoja alishindwa lakini Danieli alitafsiri ndoto ile baada ya kumwomba Yehova.
Matokeo yake, Biblia inasema: Ndipo Nebukadreza, mfalme, akaanguka kifudifudi, akamsujudia Danieli, akatoa amri wamtolee Danieli sadaka na uvumba. Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, Hakika Mungu wenu ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, awezaye kufumbua siri, kwa kuwa wewe uliweza kuifumbua siri hii. Basi mfalme akamtukuza Danieli, akampa zawadi kubwa nyingi sana, akamfanya kuwa mkubwa juu ya uliwali wote wa Babeli, na kuwa liwali mkuu juu ya wote wenye hekima wa Babeli. (Dan. 2:46-48).
Sasa, Nebukadreza aliota ndoto hii akiwa katika mwaka wa pili wa kutawala kwake. Kama alimchukua Danieli kutoka Israeli katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake, hiyo ina maana kwamba, Danieli alitafsiri ndoto ile akiwa na miaka mitatu; na pia alifanywa kuwa liwali (mbunge) akiwa na miaka hiyohiyo mitatu!
10. Jambo jingine ambalo ni kichekesho kikubwa kuhusiana na hii injili ya Barnaba ni kuwa Yesu hakuwahi kuwa na mtume aliyeitwa Barnaba. Mitume wa Yesu wanajulikana. Unaweza kusoma Mathayo 10:2-4; Luka 6:13-14.
Sasa, Barnaba ni nani?
Huyu alikuwa ni mwanafunzi aliyemwamini Yesu baadaye wakati Yesu tayari alishafufuka na kupaa kurudi mbinguni. Wakati mitume alioacha Yesu walipohubiri injili ya Yesu, mmoja wa watu waliosikia na kuiamini na kuokolewa alikuwa ni Yusufu (Joseph), mwenyeji wa Kipro (Cyprus).
Huyu aliuza shamba lake akaleta fedha kwa mitume ili wenye uhitaji waweze kugawiwa. Mitume walimpa jina la Barnaba likiwa na maana ya ‘mwana wa faraja.’
Imeandikwa: Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji. Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro, alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume. (Matendo ya Mitume 4:33-37).
Kwa hiyo, Barnaba hakuwa mmoja wa mitume wa Yesu!
Je, unadhani baada ya ushahidi huu kidogo (maana upo zaidi) bado utashikilia kuwa Injili ya Barnaba ni ya kweli? Unafikiri ni nani aliiandika? Kama umewahi kuisoma injili hii, ni kitu gani kitakachokufanya upinge hoja kwamba injili hii iliandikwa na mwislamu aliyeishi Italia katika karne ya 14, 15 au 16 ambaye alikuwa anajaribu kumhalalisha Muhammad kama ambavyo ninyi Waislamu mmeendelea kufanya hadi hivi leo – maana injili yenyewe 'inamfagilia' Muhammad?
Waswahili husema: Mwenye macho haambiwi tazama na pia sikio la kufa halisikii dawa. Je, wewe ni mwenye macho au ni sikio la kufa?
Jiponye mwenyewe.
Utadanganywa hadi lini?
Tafakari.
Hoji mambo.
Chukua hatua.

No comments:

WHY CHRISTIANITY IS BETTER THAN ISLAM?

Has Islam Improved to Become Better Than Christianity? Does Muhammad fulfill and complete the mission and purpose of Christ? Muhammad emphat...

TRENDING NOW