Friday, November 4, 2016

NENO LA MUNGU LINASEMA NINI KUHUSU SABATO? (SEHEMU YA KUMI NA TATU)


Baada ya kusoma katika Sehemu ya Kumi na Mbili kwanini Wakristo wanasali Jumapili, basi tuendelee kuona je, sheria inaweza batilishwa?
Maana ya Sheria:
Neno sheria lina maana nyingi.Lina maana kama kama;
.Desturi
.Kanuni,au
.Amri zilizo na lazima kufuatwa.
Vilevile neno sheria lina maana ya utaratibu wa maisha unaowekekewa kanuni zilizopitishwa na bunge; na pamoja na desturi zinazokabiliwa na Taifa zitumike kwa jamii (yaani sheria za mila). Ili kuakikisha kwamba sheria zinaheshimiwa na kufuatwa Taifa (Serikali) hutumia vyombo vya dola kama;
Polisi-kwa kuwakamata na kuwafikisha wahalifu mahakamani;
Mahakama-kwa kuwaadhibu wahalifu; na Magereza -kutekeleza adhabu ya mahakama kwa kuwafunga waalifu.

SASA TUJIFUNZE MAREKEBISHO YA SHERIA KATIKA AGANO JIPYA KUPITIA CHEKECHO LA MSALABA
Mungu habadiliki katika tabia na sifa zake, lakini Yeye mwenyewe amekuwa akiweka amri na kuzibadili kama apendavyo Yeye, katika vizazi mbalimbali. Na pia amekuwa akifanya maagano na vizazi mbalimbali kwa kadiri ya kusudi lake.
ADAM NA HAWA HAWAKUPEWA TORATI:
Adamu na Hawa hawakupewa torati, bali walipewa amri moja tu, yaani kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya kama Biblia inavyosema katika kitabu cha Mwanzo 2:16-17.
Mungu hakumpa Adamu amri ya ‘usizini’ kwa kuwa hakuwapo mwanamke mwingine ila mkewe Hawa. Vivyo hivyo hakumpa amri ya ‘usiibe’ kwa kuwa vitu vyote vilivyo kuwapo katika bustani ya edeni alipewa na Mungu kuwa vyake. Pia Mungu asingeweza kumwambia Adamu aheshimu wazazi wake kwa kuwa hawakuwapo. Katika maandiko hatuoni Mungu akimwagiza Adamu ashike sabato. Kwa hiyo zama za Adamu na Hawa walipewa amri moja tu.
AGANO LA MUNGU NA NUHU:
Tukija zama za Nuhu, tunaona Nuhu naye anafanya agano na Mungu na kupewa sheria zifuatazo katika Mwanzo 9:1-7; sheria ya kwanza Nuhu anaambiwa asile nyama pamoja na uhai wake yaani damu (Mwanzo 9:4-5), na sheria ya pili, Nuhu na kizazi chake wanakatazwa kuua (Mwanzo 9:6).

AGANO LA MUNGU NA IBRAHIMU:
Tukija kwa Ibrahimu tunaona Mungu anafanya agano na Ibrahimu na kumwambia awe mkamilifu (Mwanzo 17:1). Lakini pia anampa sheria mpya ya kutahiri nyama ya magovi yao, kitu ambacho Nuhu hakuamriwa kufanya.

SASA TUONE JINSI TORATI ILIVYO KUJA:

Baada ya kuja uzao wa Yakobo yaani wana wa Israeli, tunaona wanapewa torati na hukumu kupitia Musa. Hivyo basi, Mungu amekuwa akitoa amri na kuzibadili kizazi hadi kizazi. Kubadilika kwa sheria kulingana na nyakati si kitu kigeni, hayo ni mapenzi yake na hakuna mwanadamu wa kuhoji. Kazi yetu wanadamu kama watekelezaji wa amri za Mungu, ni kuwa na akili na kufahamu nyakati tulizo nazo, na amri zipi tunapaswa kuzitenda katika nyakati hizi tulizo nazo.
Maadiko katika kitabu cha 1 Nyakati 12:32 yanasema, “Na wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.” Siyo kwa sababu Ibrahimu aliambiwa na Mungu kutahiri mtoto wa kiume wa siku nane, na sisi katika Agano jipya tufanye hivyo, la hasha.
SISI TUPO KATIKA AGANO JIPYA NA SIO AGANO LA KALE:
Leo sisi hatumo katika maongozi ya Agano la kale likiongozwa na torati, bali tumo katika maongozi ya Agano jipya tukiongozwa na sheria ya Kristo (Wagalatia 6:2) na siyo na torati ya Musa.
MAREKEBISHO YA SHERIA KATIKA AGANO JIPYA
Marekebisho ya sheria katika Agano jipya, inajumuisha vitu vifuatavyo; kwanza, kupitishwa kwa baadhi ya sheria kutoka katika Agano la kale kama zilivyo; pili, kupitishwa kwa sheria za Agano la kale baada ya kufanyiwa maboresho; tatu, kutopitishwa kabisa kwa baadhi ya sheria za Agano la kale, sheria hizo ni kama kushika sabato, makatazo ya baadhi ya vyakula pamoja na kuondolewa kwa hukumu; na nne, kuwekwa kwa sheria mpya.
TORAJI ILIKUWA NI SHERIA SENYE KIVULI:
Katika kutopitishwa kabisa kwa baadhi ya sheria katika Agano la kale, Bwana Yesu, aliziondoa sheria ambazo zilikuwa ni kivuli yaani zilizoashiria kitu fulani kijacho, mfano sabato (pumziko) ilikuwa ni kivuli au ishara iliyomwashiria kuja kwa Bwana Yesu ambaye ndiye pumziko halisi, ni kwa sababu hiyo basi, kushika sabato katika Agano jipya kuliondolewa na chekecho la msalaba, kwa kuwa sheria hii ilimwakilisha Bwana Yesu mwenyewe kama pumziko halisi (sabato). Hivyo kwa vile pumziko (sabato) mwenyewe amekuja, haina haja ya kuendelea kushika kivuli au ishara.
Pia kuna sheria za Agano la kale ambazo zimepita katika Agano jipya lakini baada ya Bwana Yesu, kuzifanyia marekebisho kwa kuziboresha, yaani kuziweka kiroho zaidi. Kwa ujumla sheria kuu katika torati, ambazo ziligoma kupita kwenye chekecho la msalaba ni Kushika sabato, sheria ya makatazo ya vyakula na hukumu za torati.
BWANA YESU HAKUSHIKA SABATO:
Kuhusu sabato, Bwana Yesu hakushika sabato na wala hakuwaruhusu wanafunzi wake kushika sabato kama tulivyokwisha kuona hapo nyuma kwa upana sana (Marko 2:23-28; Yohana 9:16; Yohana 5:16-18);
Pia katika torati walikatazwa kula baadhi ya vyakula yaani wanyama n.k, lakini katika Agano jipya, Bwana Yesu aliwaagiza mitume wake wale chochote watakachowekewa mbele yao, tena wale bila kuuliza, maandiko yafuatayo yanatupa mwongozo wa kula vyakula vyote (Luka 10:8; Marko 7:18-20; Mathayo 15:11; Tito 1:15; Wakolosai 2:16; 1 Timotheo 4:3-5; Warumi 14:14, 20; Matendo 11:6-9);
Kadhalika kuhusu hukumu walizopewa wana wa Israeli nyakati za Musa, Bwana Yesu alipokuja, aliziondoa kwa kusema, “Msihukumu msije mkahukumiwa.” (Mathayo 7:1-2; Luka 6:37).
BWANA YESU ANAREKEBISHA SHERIA:
Katika Mathayo 5:21-43 tunaona Bwana Yesu akifanya marekebisho ya sheria kwa uwazi kabisa tena mbele za watu, Mathayo 5:21-22 “Mmesikia watu wa kale walivyowaambia, Usiue…..Bali mimi nawaambieni…..”
Bwana Yesu hapa anairekebisha sheria kwa kuiboresha. Mathayo 5:27-28, “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini, lakini mimi nawaambia kila amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni…” Mathayo 5:31-32, “Imenenwa pia, mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka; lakini mimi nawaambia kila mtu amwachaya mkewe……..” Kwa ujumla ukisoma Mathayo 5:21-43 yote utaona jinsi Bwana alivyofanya marekebisho ya sheria.
KUHANI MPYA NA SHERIA MPYA
Moja ya utofauti kati ya Agano la kale na Agano jipya ni ukuhani. Katika Agano la kale Kuhani alikuwa ni mwanadamu ambaye ni Haruni na uzao wake (mdhambi).
Lakini katika Agano jipya kuhani ni Mungu mwenyewe yaani Yesu Kristo (Mkamilifu).
UTHIBITISHO:
Na maandiko katika kitabu cha Waebrania 7:12 yanasema, “Maana ukuhani ule ukibadilika, hapana budi sheria nayo ibadilike”
Kuhani wa Agano la kale alikuwa ni kuhani wa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, lakini kuhani wa Agano jipya ambaye ni Yesu Kristo, Yeye ni kuhani wa sheria ya nguvu za uzima usio na ukomo kama Neno la Mungu linavyosema katika Waebrania 7:16, “Asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo.”
Kwa hiyo ni dhahiri kabisa, kwamba kwa kuwa kuhani amebadilika na sheria nayo katika Agano jipya imebadilika.
Tumefika mwisho wa Sehemu ya KUMI NA TATU, na sasa tutaenda SEHEMU YA KUMI NA NNE
ANGALIZO MUHIMU KWA WANAOSHIKA SHERIA YA SABATO
********** USIKOSE SEHEMU YA KUMI NA NNE ***********
Ni mimi Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.
© Copyright 1998-2016 Max Shimba Ministries - All Rights Reserved.
www.maxshimbaministries.org

No comments:

WHY CHRISTIANITY IS BETTER THAN ISLAM?

Has Islam Improved to Become Better Than Christianity? Does Muhammad fulfill and complete the mission and purpose of Christ? Muhammad emphat...

TRENDING NOW