Monday, November 7, 2016

NENO LA MUNGU LINASEMA NINI KUHUSU SABATO? (SEHEMU YA KUMI NA NNE)


Baada ya kujifunza kuwa Adam na Hawa hawakupewa torati au sheria ya kutunza siku ya saba. Sasa tuangalie maana ya kushika Sabato.
JE, AMRI KATIKA TORATI NI ZIPI?
Kushika sabato, makatazo ya vyakula au vinywaji na hukumu, ni miongoni mwa amri katika torati ya Musa. Na amri hizi, Bwana Yesu, hakuzipitisha katika Agano la jipya kama tulivyokwisha kuona katika sura zilizopita. Kwa hiyo, amri hizo, si miongoni mwa sheria za Kristo (Wagalatia 6:2).
Kimsingi, unapofundisha au kuishika torati ya Musa, unawapofusha watu wasione kazi ya msalaba, hivyo watu hao watajiita wakristo, lakini ni watu wenye tabia za mwilini. Kadhalika unapofundisha na kuyashika maagizo ambayo yapo kinyume na mmiliki wa mbingu, ambaye ni Bwana Yesu Kristo, ni wazi kabisa huko ni kujiweka au kuwaweka watu karibu na shimo la jehanamu ya moto.
Kwa kawaida mtu anayeisogelea torati ya Musa (kushika sabato, makatazo ya vyakula na vinywaji), hutafuta tamaa za dhambi na hatimaye mtu huyo huzalia mauti; Warumi 7:5 tunasoma, “Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwapo kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata tukaizalia mauti mazao.”
WASHIKA TORATI KATIKA AGANO JIPYA AU KARNE HII NI WANAFUNZI WA MUSA NA WALA SI WANAFUNZI WA YESU:
Lakini pia, mtu anayeshika torati ya Musa katika nyakati hizi za Agano jipya yaani kushika sabato na makatazo ya vyakula au vinywaji n.k, mtu huyo huitwa mwanafunzi wa Musa na wala si mwanafunzi wa Yesu, kwa kuwa torati ilikuja kwa mkono wa Musa na neema na kweli kwa mkono wa Kristo (Yohana 1:17). Hata kama mtu anamtaja Bwana Yesu, na mtu huyo akawa anashika sheria za Musa yaani kushika sabato makatazo ya vyakula au vinywaji n.k, bado mtu huyo ataendelea kutafunwa na nguvu ya torati. Na zifuatazo ni dalili za mtu anayemtaja Yesu lakini bado nguvu ya torati inamtafuna;
UTHIBITISHO WA KWANZA:
Mtu huyu huwa na tabia ya unafiki (nje huonekana ni mtakatifu lakini rohoni ni mdhambi)-Mathayo 6:2; Mathayo 23:25-28. Mafarisayo walikuwa na tabia hii, hivyo na mtu anayeshika torati atakuwa na tabia hii.
UTHIBITISHO WA PILI:
Mtu huyu huwa na tabia ya kupenda kubishana, kwa kuwa torati inamfanya asiwe rohoni. Hushawishika kwa hekima yenye kushawishi akili na si kwa dalili za roho na nguvu (1 Wakorintho 2:4-5).

UTHIBITISHO WA TATU:
Mtu huyu huwa na tabia ya kujihesabia haki, wakati wote hujiona sahihi, wakati amepotea, nguvu ya torati humpofusha asione ukweli (Mathayo 7:1-2).
UTHIBITISHO WA NNE:
Mtu wa namna hii, huwa na tabia ya kuinadi sheria moja ambayo anaimudu kuishika, mfano, anaweza kuwa mtu huyo anashika sana sheria ya sabato, basi atainadi hiyo sabato kuliko kumnadi Kristo. Hata kama atamwona mtu anafanya uasherati, ili mradi anashika sabato, huyo kwake ni mtakatifu.
UTHIBITISHO WA TANO:
Mtu wa namna hii huwa na tabia ya kuwaudhi walio zaliwa kwa roho yaani waliookoka; Wagalatia 4:29 tunasoma, “Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, NDIVYO ILIVYO NA SASA.”
UTHIBITISHO WA SITA:
Mtu huyu huwa na juhudi ya kumtumikia Mungu lakini si katika Roho na kweli, hivyo huwafanya waongofu wawe wana wa jehanamu mara mbili (Mathayo 23:15).
UTHIBITISHO WA SABA:
Mtu wa namna hii huwa na wema wa kujionesha mbele za watu na si wema halisi (Mathayo 6:1).
UTHIBITISHO WA NANE:
Ni ngumu mtu wa namna hii kushinda dhambi, kwa sababu ya nguvu ya torati inayomkalia kutenda dhambi.
UCHUNGUZI KUHUSU WAANZILISHI WA DINI YA ADVENTIA “SABATO”:
Ukifanya uchunguzi wa kina, utagundua kuwa, waanzilishi wa dhehebu la wanaoshika sabato, hawakuwa wanatheolojia na watu waliojua maandiko; na wala hawakukaa chini ya mafundisho ya wachungaji wao. Mwanzilishi wa Kwanza ni Mmarekani aitwaye William Miller, alizaliwa Pittsfield, Massachusetts, mwaka 1782 na kufariki mwaka 1849. Mtu huyu aliacha ukristo, lakini baadaye aliamua kurudi tena kwenye ukristo mwaka 1816, na ndiye aliyeleta mafunuo ya uongo ya kurudi kwa Bwana Yesu mwaka 1844, hata kusababisha hasara na mtafaruku mkubwa sana miongoni mwa wafuasi wake (Wana majilio-Adventists). Mwanzilishi wa pili ni Hiram Edson, huyu alikuwa ni mfuasi wa Miller, na ndiye aliyechangia mafundisho potofu ya hukumu ya upelelezi kwenye dhehebu hilo, baada ya unabii wao wa kurudi kwa Yesu kutotimia. Mwanzilishi wa tatu ni aliyekuwa baharia zamani, mtu aitwaye John Bates, huyu bwana ndiye aliyetoa mchango mkubwa wa kurudisha sabato ya Agano la kale. Na ndiye wa kwanza kutoa mafundisho ya uongo kwamba, Jumapili ni alama ya mnyama, bali siku ya sabato ndiyo muhuri wa Mungu kwa watu wake walio waaminifu. Mwanzilishi wanne ni Bwana James na mke wake aitwaye Ellen Gould White, hawa ndiyo waliouendeleza usabato kuliko mtu mwingine yeyote. James na mkewe walijiunga na Miller mwaka 1840 na 1842 na hii iliwapelekea kutengwa na kanisa lao la Methodist. Ellen ndiye aliyekuja kuyakazia mafundisho ya kushika sabato, baada ya kudai kuwa alipelekwa mbinguni na kukuta katika amri kumi za Mungu amri ya nne ya kushika sabato, ilikuwa iking’aa kuliko zote.
Mwana mama Ellen White anatia msisitizo kwa kusema amri ya nne kati ya zile kumi ni ya juu zaidi na kuzungukwa na duara linalong’aa na ilitengwa kutunza heshima ya jina la Mungu!
Mwana mama huyu wa Kisabato anaendelea kudai kuwa kama amri ya nne inaweza kuvunjwa au batilishwa basi amri nyngine zote zinaweza kuvunjwa! (Maandishi ya awali ya Ellen G. White, uk .32,35). Labda hii inaweza kukusaidia kuelewa kwa nini Waadventista wengi wanasema kwamba kama tusipotunza sabato ni sawa na kusema tunaweza kufanya dhambi za kuvunja amri nyingine tisa! Hawaelewi kabisa Agano Jipya wanaposema “kama tunaweza kuvunja sabato ni sawa na kusema tunaweza kuzini!” (Haishangazi Waadventista hawawezi kusikia au kuelewa tunayosema wakati akili zao zimepofushwa na roho hii ya udanganyifu). Akili za Waadventista zimepotoshwa na mafundisho ya huyu Mama Ellen G. White, na matokeo kwamba kushika sheria ni sehemu muhimu ya dini yao na ni aina hii ya dini ambayo Paulo alihubiri dhidi yake katika barua yake kwa Wagalatia.
Tunaona kuwa mafundisho ya Wasabato juu ya siku ya saba hayatokani na maandiko Matakatifu bali yanatokana moja kwa moja na maono ya Ellen White ambayo yaliipa sheria nafasi ya kwanza badala ya Yesu Kristo. Nao Waadventista walitafsiri maandiko kufuatana na maono yake, na kwa kufanya hivyo wanapotosha maandiko yote!
Kimsingi, hawa waanzilishi wote hawakuwa watu walioijua Biblia bali walienda kwa nguvu ya upeo mdogo wa kimaandiko waliokuwa nao. Kubwa zaidi ni nguvu ya pesa katika kueneza mafundisho, na hata kufanya kusambaa sehemu kubwa hususani Afrika.
Watoto wa Mungu, ni lazima tutambue kuwa sisi sote tumeokolewa kwa neema, na wala si kwa matendo ya sheria (Waefeso 2:8-9). Kama tutaishi kwa kufuata mambo ya mwili, hapo tunataka kufa, bali kama tutayafisha matendo ya mwili kwa roho, hapo tutaishi, kwa kuwa wanaongozwa na Roho, hao ndiyo wana wa Mungu (Warumi 8:13-14).
Ndugu msomaji, sasa tumefikia mwisho wa nakala hii ya online. Kwenye kitabu chetu “NENO LA MUNGU LINASEMA NINI KUHUSU SABATO” kuna zaidi ya Sehemu 20 ambazo hatujazitoa online. Kitabu kinachapishwa na tutawataarifu kitakapo kuwa tayari.
Mungu akubariki na endelea kujifuza zaidi wewe mwenyewe kwa kusoma Biblia na kupata msaada wa Roho Mtakatifu.
Shalom,
Max Shimba, mtumwa wa Yesu Kristo.
© Copyright 1998-2016 Max Shimba Ministries - All Rights Reserved.
www.maxshimbaministries.org

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW