Sunday, September 10, 2017

ROHO MTAKATIFU, ROHO ATUSAIDIAYE KUOMBA.

Image may contain: cloud, sky, bird and text
Kila Mkristo au mtu aliyeokoka, hana budi kuwa na lengo la kufikia kimo na cheo cha utimilifu wa Kristo katika tabia na Utumishi wa Mungu (Waefeso 4:11-15 ). Kufikia kiwango cha Yesu Kristo katika tabia ni jambo linalowezekana, Kama siyo, tusingetakiwa kuwa wakamilifu na watakatifu kama Baba wa mbinguni alivyo Mtakatifu (Mathayo 5:48;1`Petro 1:15-16) Neno la Mungu pia, linatufundisha uwezekano wa kuwa na viwango vya utumishi vya Yesu alipokuwa duniani, na hata kuzidi (Yohana 14:12).
Hata hivyo haya yote hayawezekani kama sisi siyo waombaji kama Yesu alikuwa mwombaji namba moja. Alifanya maombi alfajiri na mapema (Marko 1:35). Alijitenga na shughuli mchana na kufanya maombi (Luka 5:15-16) Aliomba jioni (Mathayo 14:23) Wakati mwingine alifanya maombi usiku kucha (Luka 6:12).
Je,sisi tunaweza kuwa waombaji kiasi hiki? Kwa nguvu na jitihada zetu hatuwezi.
Tunaweza tu, tukisaidiwa na Roho Mtakatifu. Ndiyo maana tunajifunza somo hili muhimu leo katika mfululizo wa masomo haya ya Roho Mtakatifu, na kichwa cha somo la sasa ni
”ROHO MTAKATIFU, ATUSAIDIAYE KUOMBA”, NA TUTAJIFUNZA SOMO HILI KATIKA VIPENGERE VINNE:-
A. UMUHIMU WA MAOMBI KATIKA MAISHA YA KIROHO
B. KUSHUKA KWA MUNGU BAADA YA MAOMBI YA KUUGUA NA KULIA
C. MAFUNDISHO TUNAYOYAPATA KUTOKANA NA MAOMBI YA YESU
D. ROHO MTAKATIFU,MSAIDIZI ATUSAIDIAYE KUOMBA
A. UMUHIMU WA MAOMBI KATIKA MAISHA YA KIROHO
Shetani ndiye adui yetu mkuu. Kazi yake ni kuiba chochote kizuri cha kiroho tulicho nacho, na tena kuchinja au kuua na kuharibu yote mema kwetu kiroho na kimwili.Tukiwa peke yetu, kamwe hatuwezi kupambana na shetani na kumshinda. Hatuna budi kuwa na Mungu katika maisha yetu ili tumshinde ibilisi. Daudi alimshinda Goliathi kwa Jina la Bwana.
Hakumshinda kwa nguvu zake. Kwa maana nyingine hatuwezi kuzaa matunda yoyote mema ya kiroho kama hatuko ndani ya Yesu. Usalama wetu na ushindi wetu wa kiroho, unategemeana sana na sisis kukaa ndani yake Yesu, yaani sisi kuwa na uhusiano au ushirika na Kristo. Pasipo yeye, sisi hatuwezi kufanya neno lolote. (Yohana 15:4-5). Kukaa ndani ya Yesu, kunafananishwa na tawi lililounganishwa na shina.
Kuunganishwa huko ndiyo uhai wa tawi.
Tawi likijitenga na shina, linanyauka na kufa. Sasa basi, tunaunganisha na Mungu na Mungu tunapokuwa tunawasiliana naye katika maombi. Tukiwa hatuna maisha ya maombi, kimsingi ni kwamba tunakuwa ni tawi lililojenga na shina, na hivyo tunanyauka na hatimaye kufa kiroho. Hatuwezi kuwa na kitu tusipoomba (Yakobo 4:2)
Tutaingia majaribuni tusipoomba (Mathayo 26:41).
Tutapepetwa kama ngano na ibilisi na mazuri yote ya kiroho yataondoshwa, na imani yetu itatoweka (Luka 22:31-32).
Shetani atatumeza na kuturudisha katika ufalme wake (1Petro 5:8).
Hatuwezi kuwaleta watu kwa Yesu, tusipokuwa waombaji, maana Shetani hatawaachia (Zaburi 2:8).
Hatuwezi kuona watu wakifunguliwa katika vifungo vya shetani vya kimwili (Luka 13:16) na vile vinavyotokana na mambo ya rohoni (Matendo 12:5-17). Kwa ufupi tutachukuliwa na mafuriko ya Shetani (Zaburi 32:6).
B. KUSHUKA KWA MUNGU BAADA YA MAOMBI YA KUUGUA NA KULIA
Maandiko yanatufahamisha kwamba makao ya Mungu mbinguni, ni Mahali palipoinuka, na Mlimani kwenye kiti cha enzi cha Mungu (Isaya 57:15; Kutoka 24:12-13 ; Ufunuo 7:9-10). Ingawa Mungu wetu yuko mlimani, maandiko yanasema tukimwomba, yeye husikia huko mbinguni na kutujibu maombi yetu kwa kuyatenda tunayoyataka (1Wafalme 8:32; Zaburi 76:8;1 02:19).
Hata hivyo, hatuna budi kufahamu pia kwamba katika mazingira fulani Mungu hushuka kutoka mlimani na kuja duniani katika hali isiyo ya kawaida. Mungu anaposhuka kwa jinsi hii, hutenda mambo ya kutisha, na ya kushangaza, yasiyo ya kawaida na hivyo kuwavuta wengi mno kwake (Waamuzi 4:12-16,5:13; Isaya 31:4; Hesabu 11:23-25,31-32).
Uamsho hutokea Mungu anaposhuka, na watu wagumu wa mioyo huvutwa kwa Yesu, walio vuguvugu huwa moto, mambo mengine makubwa ya kuitikisa jamii kama mamia ya wenye ukimwi kupona kwa mpigo, hutokea, Mungu akishuka.
Hata hivyo kushuka kwa Mungu hutokea baada ya maombi ya kuugua na kulia kwa uchungu mkubwa (Kutoka 2:23-24;3:7-8;
Matendo 7:32-34). Wakati wote Yesu Kristo alimfanya Mungu kushuka katika huduma yake kwa kuwa aliomba kwa kulia sana
na machozi (Waebrania 5:7), na wengine walimuombolezea kwa kilio na uchungu mkubwa (Luka 23:27).
Kulia kwa kuugua katika maombi hushusha majibu ya maombi namna ya kipekee (2Nyakati 34:27; Zaburi 34:17;39:12;51:1-2,17;72:12;12;88:1-2; Isaya 58:9; Yeremia 31:9; Luka 18:7).
Sasa basi ni rahisi kuomba maombi kwa kulia na kuugua?
Jibu ni la ,bila msaada wa Roho Mtakatifu, itakuwa kama tunaigiza tu.
C. MAFUNDISHO TUNAYOYAPATA KUTOKANA NA MAOMBI YA YESU.
Tunajifunza mambo mengi zaidi kuhusiana na maombi kwa kuyaangalia maisha ya maombi ya Yesu, na mafundisho yake kuhusu maombi:-
§ Yesu Kristo alikuwa na wakati wa kuomba pamoja na wanafunzi wake (Luka 9:18), Lakini pia alikuwa na muda mrefu wa maombi ya peke yake (Luka 5:16; Marko 6:45-46). Ni muhimu kujiunga na kikosi cha maombi cha Kanisa na kushiriki maombi ya pamoja na wengine, lakini ni lazima kila mmoja kuwa na muda wa kuomba mwenyewe.
§ Yesu hakukubali kuchukuliwa na huduma za kushauri watu, kuwaombea watu n.k na kuziruhusu zimkoseshe kuomba.
Alijua bila maombi, huduma hizo zitakuwa hazina nguvu. Aliziacha huduma, akafanya maombi (Luka 5:15-16). Kabla ya kuzungumza na watu, alizungumza na Mungu KWANZA. Alifanya maombi ya alfajiri na mapema sana na baadaye alipokutana na watu ilikuwa rahisi mno kwake kuponya ukoma na kutoa pepo. (Marko 1:35-42).
§ Kabla ya Yesu kutembea juu ya maji, na kukomesha upepo, alikuwa na kipindi kirefu cha maombi (Marko 6:46-51). Vipindi virefu vya maombi vinaweza kutupa uwezo wa kuona yasiyowezekana yakiwezekana!
§ Utukufu wa Yesu ulitokana na maombi! (Luka 9:28-29) Hatuna utukufu wa Mungu kwa kuwa siyo waombaji! Mwombaji, utukufu wake humwogopesha shetani
§ Alipokuwa na huzuni aliomba hakunung'unika tu na kulalamika, na ghafla alipata ujasiri wa kukabili lolote lile (Mathayo 26:36-39; 47-49). Hatuna ujasiri na tumejaa woga kwa kuwa hatuombi
§ Maombi yake yalikuwa ni vita hasa. Alipokuwa akiomba, alitoka jasho (hari) kama matone ya damu (Luka 22:44).
Maombi ni mapambano dhidi ya shetani anayezuia majibu yetu (Danieli 10:12-13). Ni lazima iwe ni vita. Mwili ni lazima tuushughulishe kama wapiganaji hasa, tukiwa katika roho Maombi yenye matokeo makubwa, ni yale ya kutoka jasho! Ni lazima tumkabili shetani katika vita ya maombi kabla hata hajatushambulia.Katika vita ya siku sita kati ya waisraeli na wamisri, miaka kadha iliyopita; Waisraeli walishinda Wamisri ingawa walikuwa na ndege nyingi zaidi za kivita kuliko wao,kwa kuwa walizipiga KABLA hazijaondoka katika vituo vyao.
Tusingoje matatizo ndio tuombe!
§ Imani yetu na ya ndugu zetu,inaweza kutokutindika,ikiwa tu tutakuwa waombaji;kinyume cha hapo ni rahisi kumezwa na
shetani (Luka 22:31-32;1Petro 5:8-9)
§ Maombi ndiyo yanafanya tuutunze utakatifu wetu,na kuwa mbali na dunia. Bila maombi ni rahisi kuvutwa na masumbufu
ya dunia (Luka 21:34-36).
§ Yesu aliliombea Kanisa (Yohana 17:14-15). Ni muhimu kuliombea kanisa na siyo kujiombea wenyewe tu wakati wote.
Je tunaweza kuyatendea kazi yote haya kwa nguvu zetu? Jibu ni la kwa nguvu zetu hatuwezi ,bila msaada wa Roho Mtakatifu.
D. ROHO MTAKATIFU MSAIDIZI ATUSAIDIAYE KUOMBA
Shetani anafahamu sana umuhimu wa maombi, na hivyo atatuzuia sana kufanya maombi kuliko yote mengine, ili tubaki kama matawi ambayo hayajaunganishwa na shina. Anajua pasipo Mungu, sisi hatuwezi neon lolote. Kwa kujifunza tu juu ya maombi,bado hatuwezi kuwa na maisha ya maombi. Tunaweza kuomba sisi hatuwezi neno lolote. Kwa kujifunza tu juu ya maombi, bado hatuwezi kuwa na maisha ya maombi. Tunaweza kuomba siku mbili, tatu, halafu basi. Pamoja na wanafunzi wa Yesu kuhimizwa kuomba na Yesu mwenyewe, bado walishindwa kuwa waombaji (Mathayo 26:37-43).
Ndipo hatimaye akawaambia atakuja Msaidizi ambaye kazi yake mojawapo, ni kutusaidia kuomba (Yohana 16:7; Warumi 8:26-28). Yeye Roho, kwa kuwa hutuombea kwa kuugua, na tena ni Roho ya neema na kuomba, huweza kutupa msaada wa kutuwezesha kuomba kwa kuugua na kulia (Zakaria 12:10) Baada ya Roho Mtakatifu kuja na kuwasaidia wanafunzi wa
Yesu, maisha yao ya maombi yalibadilika (Matendo 10:9). Siri ni hii, usitumie nguvu zako kuomba. Kabla ya kuingia katika maombi, mwombe Msaidizi akusaidie kuomba.
Shalom,
Max Shimba Mtumwa wa Yesu Kristo, Mungu Mkuu na Mwokozi wetu.

No comments:

WHY CHRISTIANITY IS BETTER THAN ISLAM?

Has Islam Improved to Become Better Than Christianity? Does Muhammad fulfill and complete the mission and purpose of Christ? Muhammad emphat...

TRENDING NOW