Sunday, September 10, 2017

UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU
Ili tuweze kuwa mashahidi wa Mungu,tunahitajika kubatizwa kwa Roho Mtakatifu baada ya kuokoka na kutakaswa. Ili tumtendee Mungu kazi kikamilifu, ni lazima tupokee nguvu ya Roho Mtakatifu (Matendo 1:8;Luka 24:49). Kwa sababu hili, somo hili, ni la muhimu sana kwa mtu yeyote anayetaka kuwa mtendakazi mzuri wa Mungu. Tutaligawa somo hili katika vipengere vinne:-
A. MAANA YA UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU
B. UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU,UWEZA WA KUTUWEZESHA KUWA MASHAHIDI WA MUNGU
C. ALAMA 9 ZA ROHO MTAKATIFU NA JINSI ZINAVYOTUPA UFAHAMU KUHUSU UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU
D. JINSI YA KUBATIZWA KWA ROHO MTAKATIFU
E. ISHARA YA KWANZA YA KUBATIZWA KWA ROHO MTAKATIFU NA NIDHAMU INAYOAMBATANA
F. UMUHIMU WA KUUCHOCHEA MOTO WA ROHO MTAKATIFU
A. MAANA YA UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU
Baada ya mtu kuokolewa,inambidi kubatizwa kwa maji kwa jina la baba,Mwana na Roho Mtakatifu (Mathayo 28:19). Hata hivyo,huo siyo ubatizo wa mwisho.Baada ya mtu kutakaswa,anahitajika kubatizwa kwa Roho Mtakatifu (Mathayo 3:11) Ubatizo wa maji, unamfanya mtu azamishwe ndani ya maji na kuzungukwa na maji pande zote. Vivyo hivyo, Ubatizo wa Roho Mtakatifu unamfanya mtu aliyeokoka,kuzamishwa ndani ya Roho Mtakatifu na kuzungukwa na Roho Mtakatifu pande zake zote.Roho Mtakatifu,anakuwa msaidizi wake (Yohana 15:26). Ubatizo wa maji,tunabatizwa na wanadamu waliopewa Agizo la Mungu lakini Ubatizo wa Roho Mtakatifu, tunabatizwa na Yesu mwenyewe (Mathayo 3:11).
B. UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU, UWEZA WA KUTUWEZESHA KUWA MASHAHIDI WA MUNGU
Neno “mashahidi” katika (Matendo 1:8), linatokana na neno la lugha ya Kiyunani “Martus” ambalo linatafsiriwa katika Kiingereza" Martyr” ambalo maana yake ni “Mtu anayekuwa tayari kuteswa sana au hata kuuawa kwa sababu ya imani yake,pamoja na hayo, hawezi kuiacha imani yake”.Bila ubatizo wa Roho Mtakatifu, hatuwezi kuwa mashahidi kama walivyokuwa Stefano na Antipa (Matendo 22:20; Ufunuo 2:13). Kabla ya kubatizwa kwa Roho Mtakatifu,Petro alisema asingemkana Yesu hata ikibidi kuuawa, lakini kinyume chake alimkana mara tatu,na yeye pamoja na wanafunzi wenzake walipoyaona mateso yanakuja,walimwacha na
kumkimbia Yesu (Mathayo 26:31-35,56) Lakini baada ya ubatizo walikuwa na ujasiri mkubwa. Matendo 4:13
C. ALAMA 9 ZA ROHO MTAKATIFU NA JINSI ZINAVYOTUPA UFAHAMU KUHUSU UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU
§ Maji (Yohana 7:37-39)Hakuna maisha bila ya maji.Mwanadamu ni asilimia 60%maji.Kuharisha na kutapika sana humfanya mtu kupoteza maji mengi na huweza kusababisha mtu kupoteza uhai. Vilevile sisi tunaosema tumeokoka, hatuwezi kabisakuwa na maisha ya kiroho yaliyo hai yenye nguvu, bila Ubatizo wa Roho Mtakatifu.Ni lazima tunyweshwe Roho (1Wakorintho 12:13).
Jambo jingine, maji ni muhimu katika usafi wa miili yetu hutuondolea kunuka n.k Roho Mtakatifu hutumulikia dhambi au uchafu wowote.
§ Moto (Mathayo 3:11).Kuwepo kwa moto ni alama ya uwepo wa Mungu (Kutoka 3:1-5; Matendo 2:2-3). Moto vilevile,unangarisha madini kama dhahabu na fedha (Malaki 3:2-3). Ubatizo wa Roho Mtakatifu hufanya uwepo wa Mungu uwe dhahiri kwa mtu na pia humng’arisha mtu na kuwa mtumishi wa Mungu anayeng’aa . Siyo hayo tu, moto huleta mwanga.Ubatizo wa Roho Mtakatifu hutupa mwanga mkubwa wa maandiko yaani Biblia na kutupa mwanga wa uzuri wa mbinguni na ubaya wa Jehenam.Ukiwa na mwanga huo hakutakuwa na gharama kubwa yoyote ya kukufanya ushindwe kufanya mapenzi ya Mungu. Moto pia huleta nguvu ya kuendesha, magari, treni, Ndege n.k vifaa vyote hivyo huendeshwa kutokana na moto unaotokea baada ya cheche za umeme kuunguza mafuta.
Kazi ya Mungu inaendeshwa kwa nguvu ya moto, ubatizo wa Roho Mtakatifu na kwa moto. Mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu, moto unawake ndani yake na hawezi kuacha kushuhudia au kuhubiri na kufundisha (Yeremia 20:9; Isaya 62:1; Matendo4:20). Mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu,maneno yake huwa moto unaoteketeza kila ugumu wa mioyo ya watu kwa kuwa Roho Mtakatifu hushuhudia pamoja naye na hivyo matokeo yake ya utumishi wake huwa makubwa. Ni nguvu kwa ajili ya Utumishi (Yeremia 5:14; Yohana 15:26-27;16:6-8;Mika 3:8).
§ Upepo (Yohana 3:8) Upepo wakati wote unatembea, na uko mahali pote. Roho Mtakatifu hakufanya kazi wakati wa mitume tu, hata sasa anatembea na yuko kwetu tayari, ni wajibu wetu kumpokea tu. Upepo huvuma upendako.
Ni vigumu kuubadilisha mkondo wa upepo tunavyotaka sisi,jahazi hufuata mkondo wa upepo. Ni muhimu kutakaswa kwanza kabla ya Ubatizo huu.
Utakaso humfanya mtu kuwa mtii mno katika yote na Roho Mtakatifu ni mshirika wa wale wamtiio(Matendo 5:32) Upepo pia hutuletea hewa safi inayotuburudisha wakati wa joto, moshi n.k Mazingira yoyote magumu tukiyakabili katika utumishi wa Mungu, Roho Mtakatifu huwa hewa safi kwetu inayorekebisha mazingira.
§ Mafuta (Luka 4:16-21) Roho Mtakatifu hututia mafuta au kutuweka katika utumishi wa Mungu (1Samweli 16:13; Kutoka 30:30; 1Wafalme 19:16;Yohana 2:27) Rais kabla hajaapishwa huitwa Rais mteule na hana mamlaka sana wakati huo kisheria.
Kuapishwa kwa leo ndiyo kutiwa mafuta kwa zamani.Bila ubatizo huu,mamlaka yetu huwa hafifu. Mafuta yanalainisha na kuzuia msuguano.Ubatizo wa Roho Mtakatifu hutupa hekima ya kuvuta roho za watu(Mithali 11:30) mafuta huufanya mwili uwe laini.
Ubatizo wa Roho Mtakatifu hulainisha ukavu wa maombi yetu (Warumi 8:26).
§ Mvua (Zaburi 72:6;Hosea 6:3) Nchi haiwezi kutoa matunda bila mvua.Mtu aliyeokoka hawezi kuwa na matunda mengi bila mvua yaani ubatizo wa Roho Mtakatifu (Yohana 15:16).
§ Mvinyo (Waefeso 5:18;Matendo 2:12-13) mvinyo kwa walevi unasahaulisha shida. Ubatizo wa Roho Mtakatifu, humwezesha mtu kudharau majaribu na kuondoa wasiwasi na kubabaishwa na mambo madogo madogo tu. Mvinyo kwa walevi, pia unawapa ujasiri wa kufanya lolote lile, aibu, woga vinatoweka. Ubatizo wa Roho Mtakatifu humfanya mtu kuwa jasiri kama simba na mtu aliye kuwa mwoga kama Petro, kuwa jasiri (Mithali 28:1; Mathayo 26:31-35,56; Matendo 4:13).
§ Hua (njiwa)- (Yohana 1:32) Ubatizo wa Roho Mtakatifu haufanyiki kwa mtu wa ulimwengu huu yaani ambaye
hajaokoka. Njiwa hakutua kwenye ulimwengu,alirudi safinani kwa waliookoka (Mwanzo 8:8-9)Roho Mtakatifu ni mweupe, kama hua.Ni Mtakatifu,huja kwa watakatifu waliotakaswa.
§ Muhuri (Waefeso 1:13) Muhuri ni alama ya mamlaka.Bila muhuri barua hupungua mamlaka yake. Ubatizo wa Roho Mtakatifu humfanya mtu kuwa na mamlaka ya Yesu kwake na shetani husema “ Yesu namjua na Paulo namfahamu (Matendo 19:15) Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni mamlaka au uwezo kutoka juu wa kuzifanya kazi za Yesu.
§ Arabuni (2Wakorintho 1:21-22)Neno arabuni maana yake- Uhakikisho au uthibitisho wa Uimara.Ubatizo wa Roho Mtakatifu, hutufanya kuwa na uthibitisho wa uimara wa Neno la Mungu, hutuongezea imani ya kufanya maajabu.Shetani hawezi kumpeperusha huku na kule mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu.
D. JINSI YA KUBATIZWA KWA ROHO MTAKATIFU
Kuokoka au kuzaliwa mara ya pili.Mafuta haya hayatiwi kwa mtu mgeni ambaye jina lake haliko katika kitabu cha Uzima mbinguni (Kutoka 30:31-33)
Kutakaswa (Yohana 17:17;1Wathesalonike 5:23) Wanafunzi 120 orofani,walitakaswa kabla ya Ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Kuwa na Imani kama Roho Mtakatifu yuko kwetu tayari na kwamba ni ahadi ya Mungu kwetu(Matendo 2:38-39); Luka 11:10-13)
Kuwa na kiu ya kumtumikia Mungu (Isaya 44:3)
Kuomba kwa kufumbua sana kinywa na kutokuruhusu kutumia akili,wala kuwaza kwambatutasema lugha ya mapepo. (Luka 11:10-13; Zaburi 81:10).
E. ISHARA YA KWANZA YA KUBATIZWA KWA ROHO MTAKATIFU NA NIDHAMU INAYOAMBATANA
Mtu akibatizwa kwa Roho Mtakatifu,kutakuwa na mambo ya kusikia kwake na ya kuyaona kwake(Mathayo 3:16-17).
Ishara ya kwanza ni kusikia kutoka kwake kabla ya kuona mengine. Atasema au ananena kwa lugha mpya asiyoifahamu
ambayo siyo ya dunia hii (Matendo 2:4;10:44-46;19:6). Ni muhimu mno kwa mtu aliyeokoka kuomba kwa kunena kwa lugha hii (1Wakorintho 14:2,4-5,15). Hata hivyo hatupaswi kunena kwa lugha mbele ya mataifa wasioelewa kitu. Watadhani sisi ni wendawazimu (1Wakorintho14:18-25)
Kunena kwa lugha mbele ya mataifa wasiojua kitu nikuwapa mbwa kilicho kitakatifu na kutupa lulu zetu mbele ya nguruwe matokeo yake watatudhihaki kwa kuwa hawajui maana (Mathayo 7:6).
F. UMUHIMU WA KUUCHOCHEA MOTO WA ROHO MTAKATIFU
Moto bila kuchochewa huzimika (Mithali 26:20). Hatuna budi kuwa waombaji na kuomba kwa Roho, yaani kunena kwa lugha katika maombi mara kwa mara katika maombi yetu binafsi (1Wakorintho 14:14-15; Yuda 1:20) Vile vile hatuna budi kudumu katika usafi kwa Neno (Zaburi 51:4,11;119:11; Yohana 15:3).
Hatuna budi pia kujihusisha katika kushuhudia na kuwaleta watu kwa Yesu (Mika 3:8).
Shalom,
Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.

No comments:

WAS MUHAMMAD PROPHESIED IN THE BIBLE?

SURAH 61:6 Muslims believe that the coming of Muhammad was foretold in the Bible. For centuries, Muslims have tried to find predictions of t...

TRENDING NOW