Sunday, August 6, 2017

UTHIBITISHO KWAMBA MUNGU YUPO (SEHEMU YA KUMI)

Image may contain: text
Naam, tumefikia sehemu yetu ya Mwisho:
Uzoefu wa wengi ni ushuhuda wa nguvu:
Historia na anthropolojia hushuhudia kuwa uzoefu wa dini ni wa kiulimwengu. Watu wa kila zama na tamaduni wamedai kuwa na uzoefu na "Uungu." Wamemkaribia “Mungu” kwa kusujudu, kuheshimu, kusifu, na kushukuru. Je! Yawezekana waabudu wote hao wanainama kiti kilicho tupu? Kwamba uzoefu wanaoujua sio halisia? Kweli, hapo kale walimwengu wengi walijua kimakosa kuwa jua linaizunguka dunia. Lakini uzoefu wao ulikuwa sahii. Kwa uzoefu walijua bila kukosea kuwa jua lipo, dunia ipo na mzunguko upo. Huenda waabudu wakakosea kujua Mungu yukoje, lakini haiwezekani wakakosea kujua yupo. Ikiwa wengine hawajui uzoefu unaojulikana sana, huenda shida ni mishipa ya fahamu, mishipa iliyopoteza uwezo wake wa kuhisi na kujua. “Kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.” (Warumi 1:21)
NYAKATI TULIZO NAZO
Ingawa unabii tuliouzingatia mpaka sasa umeendelea kutimia hadi hivi leo, ulihusu zaidi matukio ya siku nyingi za nyuma (ukiacha urudishwaji upya wa Waisraeli hivi karibuni katika ardhi yao ya kale). Je, kuna kinachosemwa na unabii wa Biblia juu ya nyakati tulizo nazo kuweza kutuongoza katika siku hizi?
Kipo hasa! Tena ni ajabu kinavyotofautiana sana na matazamio na fikra za kibinadamu. Karne ya 19 ilikuwa kipindi cha matumaini. Maendeleo makubwa yalikuwa yakipigwa. Ujuzi wa Kisayansi ulivyoongezeka ulileta maendeleo haraka kiufundi na uzalishaji mkubwa viwandani. Hili lilikuwa lilete neema (ingawa sio kwa walio maskini sana). Elimu ilipanuliwa kuwafikia wengi, na matumaini ya maana yalipatikana. Watu walioelimika zaidi, ilidaiwa, wangejishughulisha na sanaa kama fasihi, muziki na uchoraji. Maadili ya jamii kwa ujumla yengeboreka. Wanasiasa waliahidi kuleta mpango mpya wa kijamii wa haki na usawa kwa wote. Vile ambavyo watu wangetajirika, ndivyo ambavyo wasingeoneana kijicho. "Tokomeza umaskini, na ndivyo utakavyotokomeza uovu, lilikuwa ndilo bango. Wakati uwezo wa juu wa akili ya mwanadamu ukitumiwa, ilikuwa amani ijengeke kati ya mataifa. Viongozi wa kanisa nao wakatazamia kwa dhati kueneza Injili dunia nzima. Kujiendeleza mwanadamu na kuboresha maisha, kwa mtu binafsi na kwa jamii, vilichukuliwa juu juu tu. Hali ya baadaye ikaonekana nzuri.
Amani na maendeleo?
Kinyume cha matazamio hayo, matukio ya karne ya 20 yamekuwa mfadhaiko. Ndoto za maendeleo na amani zimefifia. Vita viwili vibaya sana vya dunia, vikiwa vimechinja mamilioni na kuleta uharibifu usiosemekana wa mali na mateso, vimefuatiwa na uundaji wa silaha kali za maangamizi ambazo hazijawahi kutengenezwa. Mawazo ya utatuzi ya aina mbalimbali ya 'wenye busara' wa karne ya 19 yamekuwa bure. Kupanuliwa elimu hakujafuatiwa na maadili zaidi, badala yake na kukua kwa dhuluma, choyo, vurugu na uvunjaji sheria. Dini ya Kikristo, mbali na kuwabadili mataifa, imekuwa katika kurudi nyuma duniani pote. Demokrasia katika siasa haijajidhihirisha kuwa muarobaini wa maovu katika jamii kama ilivyotarajiwa. Mwishowe pigo baya zaidi - sayansi imethibitika kuwa silaha ya kutisha ya makali kuwili. Mbali na kuwa enzi ya amani, karne ya 20, ya ustaarabu, imekuwa wakati wa migogoro na mapambano. Ndio maana mtizamo wa wengi umekuwa ule wa kukata tamaa. Inaonekana kama hakuna anayeweza kufanya kitu.
Sasa unabii wa Biblia unasemeaje hali hizi?
Biblia ina utabiri wa kueleweka kabisa juu ya siku za mwisho, 'nyakati za mwisho,' wakati harakati za mwanadamu katika nchi zitakapofikia hatua mbaya. Sio picha ya maendeleo endelevu na amani, bali ya matatizo duniani na hofu. Mfano wa wazi sana na unaotugusa upo katika yale Yesu aliyowaambia wanafunzi wake walipomuuliza nini ingekuwa ishara ya kurudi kwake duniani na ya 'mwisho wa dunia.' Anawaambia kwanza juu ya hatima ya Wayahudi.
" Wataanguka (Wayahudi) kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa (wasio Wayahudi), hata majira ya Mataifa yatakapotimia." (Luka 21:24)
Sasa haya ni maelezo mafupi juu ya yale tuliyoyaangalia yahusuyo unabii kwa Israeli. Wayahudi wangeng'olewa kuwa mateka kati ya mataifa yote; Yerusalemu ingekaliwa na mamlaka za kimataifa. Gundua kwamba Yesu anasemea mwisho wa hili 'hata majira ya Mataifa yatakapotimia.' Tumeona mwanzo wa jambo hili katika wakati wetu. Yerusalemu haikaliwi tena na watu wa nje - unakaliwa na Israeli yenyewe.
Mashaka na hofu duniani:
Kwa hiyo yale anayoendelea kusema lazima yahusiane na siku hizo - siku za Israeli kurudishwa katika nchi yao wenyewe. Hivi ndivyo anavyotabiri.
"Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya Mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika." (Ms. 25 - 26)
Hii sio picha ya amani na maendeleo. Ni dunia ya hekaheka na
kuchanganyikiwa, hofu ikiikumba mioyo ya watu wanapofikiria mambo yanayotokea katika 'makao ya watu duniani' kama neno alilotumia Yesu linavyomaanisha.
Mtume Paulo, akiwa anaandika kama miaka 35 baada ya unabii huo wa Yesu, anasema hivi juu ya hali ya siku za mwisho.
"...siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, na wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiopenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake;.."
Hii ni sura ya ajabu ya ustaarabu; mtu anatupilia mbali vizuizi vyote na kuzifuata tamaa zake mwenyewe bila kujali matokeo yake. Hakuna asiyeona uwiano wa hali hiyo na mambo yalivyo katika dunia yetu ya sasa.
Kwa hiyo hali ni hiyo; wakati wajuzi wa mambo miaka 100 tu iliyopita walitazamia kwa dhati sana, kipindi cha maendeleo na amani kwa mataifa ya dunia, Biblia, katika maneno ya Yesu na Paulo ilitabiria dunia ya fujo, hofu na kuchanganyikiwa, nyakati za migogoro, kujifanyia mtu atakacho, na chuki. Wanafalsafa wetu wa kibinadamu walikosea; Yesu na Paulo walikuwa sawa! Lakini waliongea na kuandika zaidi ya miaka 1900 iliyopita. Waliwezaje kujua? Sababu pekee ni kwamba hawakusema maneno yao wenyewe, bali maneno ya Mungu Mwenyewe. Ni Mungu aliyejua, akampa uwezo Mwanawe na mtume wake kutufunulia hali ya siku za mwisho.
HITIMISHO
Kuna majumuisho kadhaa muhimu tunayoweza kuyafikia kutokana na kuchunguza kwetu unabii wa Biblia.
Kama Biblia imejithibitisha kuwa sahihi kiasi hiki katika utabiri wake wa matukio katika historia ya mwanadamu - hatima ya Babeli, Misri na Israeli, na pia katika kukua na kuanguka dola, na hali ya dunia kwa wakati huu - itakosa kuwa sawa katika utabiri wake wa matukio yaliyobaki?
Chukulia yale maono katika sanamu katika Daniel, kwa mfano.
Hatujatolea maoni bado juu ya ile hatua ya mwisho: Jiwe, " lililokatwa kutoka mlimani bila kazi ya mikono," liliipiga ile sanamu chini ya miguu, likaivunjavunja, na lenyewe "likawa mlima mkubwa, na kuijaza dunia yote (Dan. 2:35).
Sasa maana ya jumla ya hili iko wazi: kitu kigeni, kisichokuwa sehemu ya dola za sanamu na falme, kinaziharibu na kuchukua nafasi zake duniani. Kwa kuwa 'bila mikono,' maana yake ni 'bila mikono ya mwanadamu', lile jiwe lazima litakuwa linasimama badala ya nguvu isiyokuwa ya kawaida ya kibinadamu.
Lakini Daniel anatuambia mwenyewe maana yake:
" Katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele... utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele. " (Mstari. 44)
Serikali za sasa na mamlaka za dunia zitaondolewa, katika tukio moja la aina yake, Mungu atakapoingilia kati na kusimamisha Serikali yake Mwenyewe. Kuondoa utata ieleweke kwamba, sio umati wa watu unaoangamizwa: ni nguvu na mamlaka za falme za kibinadamu, zitakazong'olewa na ufalme mpya wa Mungu.
Unabii mwingi mwingine unatueleza jinsi ufalme huo utakavyokuwa; maongozi yake timamu, mafundisho yake yenye kweli, na amani utakayoleta hatimaye duniani kwa watu wote kutokana na kumtambua kwao 'Mungu wa mbinguni!' Soma kwa mfano Isaya 2:1-4 kupata picha kamili na ya kusisimua juu ya mataifa katika enzi hiyo ijayo.
Lakini ni kwa namna gani mageuzi hayo makubwa yanaweza
kufanikishwa duniani? Agano jipya linatupa jibu. Na hasa ni Yesu mwenyewe anayetuambia katika unabii ule wa nyakati za taabu na hofu kwa mataifa yote. Maneno yake yaliyofuata ni haya
"Hapo ndipo watakapomwona mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi" (Luka 21:27)
Anasema atarudi tena mwenyewe. Kurudi kwa Kristo duniani ni wazo mojawapo kuu katika mafundisho ya Yesu na mitume katika Agano Jipya na linakubaliana kabisa na manabii. Soma zaburi 72 kupata kinachosemwa juu ya utawala wake.
Sasa, kwa hakika, hili ndilo linalopaswa kutushughulisha sana: Kama unabii wa Biblia kuhusu mataifa na dola umekuwa kweli kama ilivyo kwa zaidi ya miaka 2000, hayo mengine yaliyotabiriwa yatakosa kutimia? Sio kukosa busara kusema: "sawa nakubali manabii walikuwa sahihi katika utabiri wao katika mambo haya ya kihistoria, lakini siamini wanayosema juu ya yajayo kutuhusu sisi." Kwa nini? Wametoa uthibitisho kwamba hawakuwa wakitoa mawazo yao wenyewe, bali makusudio hasa ya Mungu. Yote yale wanayosema yanapaswa kutufanya tujali sana.
Kitu cha muhimu
Lakini bila shaka kuna zaidi. Unabii huu wa ajabu unapatikana katika Biblia, na sio mahali pengine popote duniani. Hakuna maandiko mengine, hakuna vitabu, hakuna matamko mengine yoyote ya mwanadamu yanayoweza hata kwa mbali kulinganishwa na Biblia. Lakini Biblia inatuambia kwamba Yesu alikuwa mwana wa Mungu; mambo aliyosema yamehifadhiwa kwa ajili yetu katika Injili za Agano Jipya. Pamoja na mafundisho ya mitume wake Petro, Yohana na Paulo, wanatufunulia ukweli ambao hatuwezi vinginevyo kuujua. Wanatuonya juu ya ukweli kuhusu kifo; wanaeleza kwa nini Injili ni 'habari njema,' 'uweza wa Mungu uuletao wokovu' (Warumi 1:16). Wanatutia moyo na ahadi ya uzima wa milele katika mpango mpya atakaouanzisha Kristo atakapokuja. Ndio maana inatupasa kuisoma Bilia. Inaweza kutupa utofauti wa muhimu kati ya utupu wa kifo, na tumaini la nguvu la maisha yasiyo na mwisho.
Usomaji wa makini wa Biblia utatuhakikishia kuwa Mungu yupo,
anatawala, na kwamba anatuita tuwe wafuasi wa mwanawe. Biblia ipo kwa ajili yetu. Tunafanya vizuri kujali inachosema.
Hauko mwenyewe kama ungali unasita kuamini Mungu yupo. Lakini ikiwa yupo, Mungu aliye na uwezo wote na wema wote, basi utajiumiza mwenyewe usipomwamini. Ukimkataa, utakuwa unakataa uzima na upendo.
Wapo waliotafuta kumjua Mungu na kumpata; wakawa na hekima na furaha. Wapo waliotafuta kumjua na kumkosa; wakaonekana wana “hekima” lakini hawana furaha. Na wapo wasiomtafuta na wamepungukiwa hekima na furaha. Kuamini ni kuchagua. Ikiwa utachagua kuamini Mungu yupo, uwezekano wa kupata maana ya maisha upo. Yesu Kristo amekwisha sema, “tafuteni, nanyi mtaona” (Mathayo 7:7).
​Kama unataka kumjua Mungu binafsi, lakini unaona woga, waweza kuomba ombi hili: “Mungu, sijui kama unaishi au la, lakini kama upo, tafadhali jifunue kwangu jinsi ulivyo.”
Hongera, ombi lako limesikiwa! Mungu amekwisha anza kujifunua kwako!
Shalom,
Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.

No comments:

THE SEVEN PROPOSALS OF MUHAMMAD THAT WERE REJECTED

  1. Why did some women reject Muhammad's proposals? 2. Why did Muhammad continue to propose despite the rejections? Dear reader, Today ...

TRENDING NOW