Na. Mwl. Daniel Mwankemwa
Utangulizi:
Majini ni viumbe visivyoonekana kwa macho ya kawaida ya wanadamu. Hii ni kwa sababu viumbe hivi viko katika asili kutoonekana. Majini huitwa pia Ibilisi, shetani, pepo mchafu au joka la zamani.
ASILI YAO:
Kwa mujibu wa Biblia majini yalikuwa ni malaika kabla ya kuungana na yule muasi mkuu wa Mungu, yaani Lucifer aliyemuasi Mungu mbinguni na kutaka ukubwa wa kufanana na Mungu, na ndipo akatupwa huku duniani yeye pamoja na malaika zake, na huku wakiwa wamenyanganywa utukufu waliokuwa nao hapo awali. Vita hivyo viliongozwa na malaika mkuu wa Mungu wa Mbinguni yaani Yahweh(Yehova) kumtupa chini huyo malaika muasi pamoja na malaika zake. Viumbe hivyo vilivyotupwa ndivyo leo vinaitwa MAJINI au MASHETANI au PEPO WACHAFU au IBILISI au JOKA LA ZAMANI.
Uf. 12:7-12 “Kulikuwa na vita mbinguni, Mikael na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake, nao hawakushinda wala mahala pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa yule mkubwa nyoka wa zamani aitwaye ibilisi na shetani audanganyaye ulimwengu wote, akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni ikisema sasa kumekuwa wokovu na nguvu na ufalme wa Mungu wetu kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu yeye awashtakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya mwanakondoo na kwa neno la ushuhuda wao ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. Kwa hiyo shangilieni enyi mbingu, nanyi mkaaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”
Hivyo kwa mistari au aya hizo unaanza kupata taswira ya kile tunachojifundiza kuusiana na majini.
Ki-Biblia malaika ni viumbe walio katika hali ya roho ila wanaweza kuonekana kwa umbile la mwanadamu. Mw. 18:1-18, Lk 1:26-28, Kut 3:1-6
Katika Ebr 1:13-14 “Yuko malaika aliyemwambia wakati wowote uketi mkono wangu wa kuume hata nitakapowaweka adui zako chini ya nyayo zako? Je, hao si ROHO watumikao wakitumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?”
Biblia inazidi kubainisha namna ya kuubwa kwao
Mw.2:1 “Basi mbingu na nchi zikamalizika na JESHI LAKE LOTE”
Ni katika jeshi hilo ambapo tunapata hawa viumbe vya kiroho.
Na katika Kol 1:1-16 “Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa vilivyoko mninguni na vilivyo juu ya nchi. Vinavyoonekana na visivyoonekana……….”
Jeshi hilo ni huru linaweza kujiamulia lolote na ndiyo maana 1/3 ya hao hao roho yaani malaika waliasi na kufanya machukizo mbele za Mungu na wakafukuzwa (Uf 12:7-12) na wengine wamefungwa.
Katika Yuda 6 “Na malaika wasiolinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu”
Kwa hiyo majini ndiyo mashetani na mashetani ndiyo majini. Katika kitabu cha
Lawi 17:7
“Wala hawatatoa tena sadaka zao Kwa wale MAJINI ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao, sheria hii itakuwa sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao kizazi baada ya kizazi.”
Kwa sababu majini hayo tangu yalipotupwa toka mbinguni wana wa Israeli hawakuwa na ufahamu kwa kutosha kuyahusu, baadhi yao walijikuta wakiyatolea sadaka huku wakiamini kuwa wanamtolea Mungu sadaka. Na kumbuka kuwa mara nyingi wana wa Israeli walipotoa sadaka zao nyingi zilikuwa za wanyama na hivyo kutakiwa kujinja na kutoa damu ambayo ni sehemu kubwa ya chakula cha majini.
Katika Zaburi 106:34-40.
“ hawakuwaharibu watu wa nchi kama BWANA alivyowaambia, bali walijichanganya na mataifa wakajifunza matendo yao, bwakazitumia sanamu zao nazo zikawa mtego kwao naam walitoa wana wao na binti zao kuwadhabihu kwa MASHETANI wakamwaga damu isiyo na hatia, damu ya wana wao na binti zao walio watoa dhabihu kwa sanamu za kaanani. Nchi ikatiwa unajisi kwa damu.”
Ndivyo walivyotiwa uchafu kwa kazi zao, wakafanya uasharati kwa matendo yao. Hasira ya Bwana ikiwa juu ya watu wake akauchukia urithi wake.
Hivyo kutokokamana na kutokuonekana kwao hayo majini yaliwahujumu wana wa Israel hata yakawasababishia wamwasi Mungu kwa kuyatolea sadaka kinyume cha Mungu wa mbinguni aliyehai.