UTANGULIZI.
Imekuwa ni kawaida sasa kwa miaka zaidi ya ishirini hivi, kusikia katika
mihadhara inayoendeshwa na wahadhiri wa dini ya Uislamu, ambayo imeenea sehemu
mbalimbali Duniani na haswa katika nchi za Africa Mashariki na Kati,(East and
Central Africa). Wahadhiri hao hufundisha jamii kupitia Qurani na Biblia kwa
kusema kuwa Mungu ni Mmoja tu. Wasema Mungu kwa Kiebrania anaitwa Yehova , kwa
Kiarabu Allah, kwa Kiingereza God na kwa Kiswahili ni Mungu. Kwa hivyo wasema
Mungu Allah kama Qurani inavyofundisha, ndiye Yehova kama Biblia
inavyofundisha. Mihadhara hiyo inayoendeshwa na Waislamu imeenea sana, mfano
Nchini Tanzania kuna vikundi vingi na kimoja wapo kinaitwa Al-Marid
International Propagation Center. Hawa wameandika katika bango lao kwa kunukuu
katika Biblia maneno aliyoandika Mtume Paulo katika Waefeso 4:4-6. Maneno
waliyoyanukuu yanasema hivi “Bwana mmoja , Imani moja ….., Mungu mmoja , naye
ni Baba wa wote, aliye juu ya yote. Nilipotembelea mkoa wa Morogoro pale mjini,
eneo la kiwanja cha ndege nikaona Msikiti mmoja umeandikwa maneno haya ya
Waefeso 4:4-6. Na nilipotembelea mji wa Nairobi Nchini Kenya pia nikaona kuna
vikundi vingi vinavyoendesha mihadhara na kikundi kimoja wapo kinaitwa Kibera
Islamic Propagation Centre. Hawa nao katika bango lao wameandika ujumbe
unaosema hivi “Acha Biblia Ijisemee na kunukuu injili aya hii” Yohana 8:32 Tena
mtaifahamu kweli nayo hiyo kweli itawaweka huru.
Kwa hivyo utaona kuwa wahadhiri hao wa Dini ya Uislamu hufundisha jamii kwa
kutumia Qurani na Biblia na kusema Allah Sub-Hana Wataala ndiye YEHOVA.
Fundisho hili wanalieneza kwa kupitia Radio, Vijarida, Mihadhara, vitabu na
Kanda (cassettes) za Video na Audio. Na hivyo kuwafanya baadhi ya Wakristo
kuacha Imani yao na kuingia katika Dini ya Uislamu. Na baadhi ya Wakristo wengine
ingawa hawajabadili dini wanaamini hivyo. Swali la muhimu la kujiuliza kwa kila
mkristo, je, ni kweli Mungu Allah kama inavyotuhadithia Qurani ndiye Yehova
kama Biblia inavyotufundisha? Nakusihi fuatilia somo hili kwa makini ili kujua
Ukweli……
SEHEMU KUU ZA SOMO HILI NI HIZI……
1. Hoja za waislamu kusema Allah ndiye Yehova.
2. Je, jina la Mungu kadiri ya Qurani na Biblia ni moja?
3. Je, Malaika mkuu wa Allah ndiye wa Yehova?
4. Je, ni nani muumba,Allah au Yehova?
5. Mji aliochagua Allah je, ni sawa na wa Yehova?
6. Allah anavyofundisha kuhusu kujitakasa nafsi je, ni sawa na Yehova?
7. Je, mbingu ya Yehova ni sawa na ya Allah?
8. Mwisho wa wanaomwabudu Allah ni wapi?
1. Hoja za waislamu kusema Allah ndiye Yehova
Wahadhiri wa Dini ya Uislamu wanasema Mungu Allah ndiye Yehova kwa sababu
Manabii wa Mungu kadiri ya Biblia na Qurani walifundisha kwa kusema Mungu ni
mmoja tu. Na wanasoma aya hizi…
Nabii Musa alivyosema
Kumbukumbu la Torati 6:4
Sikiza ee Israeli; BWANA Mungu wetu BWANA ndiye mmoja.
Nabii Isaya alisema hivi
Isaya 45:18,21
Maana BWANA , aliyeumba mbingu, asema hivi, yeye ni Mungu ,ndiye aliyeumba
Dunia na kuifanya ….. si mimi BWANA? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi. Mungu
mwenye haki , mwokozi hapana mwingine zaidi ya mimi.
Nabii Daudi Alisema
Zaburi 86:10
Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu, wewe ndiwe mfanya miujiza , ndiwe Mungu peke yako.
Yesu alisema hivi
Yohana 17:3
na uzima wa milele ndio huu wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu
Kristo uliye mtuma
Paulo naye Alisema hivi
1 Wakorintho 8:4
Basi kwa habari ya kuvila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya kuwa
sanamu si kitu katika ulimwengu, na yakuwa hakuna Mungu ila mmoja tu.
Hapa wahadhiri wa Dini ya Uislamu wanasema Manabii wote kadiri ya Biblia wanafundisha
kuwa Mungu ni mmoja tu. Je, Muhammad (s.a.w.) alifundisha nini kuhusu Mungu?
Wanasoma aya hizi za Qurani……..
Qurani 41:6 Suratul Haa Mym Sajdah (Kusujudu)
Sema; bila shaka mimi ni mtu kama nyinyi. Nimeletewa Wahyi (inafunuliwa
kwangu)ya kwamba Mungu wenu ni Mungu mmoja tu……
Hapa wahadhiri wanasema kama vile manabii wote walifundisha Mungu mmoja ndivyo
ilivyo fundisha Muhammad.
Qurani 29:46-47 Suratul Al- Ankabuut (Buibui).
Wala mshibishane na watu waliopewa kitabu (kabla yenu) ila kwa yale (majadiliano)
yaliyo mazuri, isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Na semeni :tunaamini
yaliyoteremshwa kwetu, na yaliyoteremshwa kwenu. Na mungu wetu na Mungu wenu ni
mmoja : nasi ni wenye kunyenyekea kwake. Na namna hivi tumekuteremshia kitabu
(hiki cha Qurani) basi wale tuliowapa kitabu (kabla ya hiki kama taurati na
injili) wanakiamini (hiki kitabu ulichoteremshiwa kwani hakipingani na hivyo
walivyoteremshiwa). Na miongoni mwa hawa (Waarabu wasiokuwa na Kitabu
chochote)wako wanaokiamini. Na hawazikatai aya zetu isipokuwa wale wanaotaka
kuficha haki.
Hapa wahadhiri wa kiislamu wakisha soma aya hizi husema vitabu vya Torati na
Injili havipingani na Qurani, na vitabu hivyo walipewa Wayahudi na
Manasara(yaani Wakristo) na Mungu wa Waislamu na Wakristo ni mmoja tu.
Je, hoja hii ni kweli? Nitaijibu huko mbele.