Natanguliza maswali kwa waislam:
(a)Aya gani ya quran au hadithi gani inawaagiza kufanya sikukuu au sherehe ya Maulid ya Mtume?
(b)Nini adhabu ya watu wanaotunga kitu kama Maulid na kukiingiza katika dini?
UTANGULIZIUpagani wa maulid unadhihirika kwa kuangalia maeneo makubwa matatu:
(a) Historia ya Maulid.
(b) Kutokuwepo kwa uhakika wa tarehe aliyozaliwa mtume Muhammad kutoka kwenye quran au hadithi
(c) Ushahidi wa wanazuoni juu ya upagani wa maulid.
(a) HISTORIA YA MAULID Historia hii inatuonesha vitu vitatu vya msingi:
(i) Si Muhammad wala maswahaba walisherekea Maulid
(ii) Maulid ilianza miaka zaidi ya mia tatu baada ya mtume.
(iii) Waanzilishi wa Maulid wana nasibishwa na kizazi cha wakanaji Mungu (Wapagani na makafiri).
Yeyote mwenye kutazama maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na historia ya Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum), Taabi‘iyna na waliowafuata kwa wema mpaka kufikia zaidi ya mwaka wa 350 Hijri hatumuoni hata mwanachuoni mmoja wala mahakimu (viongozi) na wala watu wa kawaida waliokuwa wakifanya mawlid au wakaamrisha au wakahimiza au wakazungumza juu yake. Amesema al-Haafidh as-Sakhawiy: “Shughuli za kufanya Mawlid matukufu hayakupokelewa na watangu wema (Salafus Swaalih) wa karne tatu bora za mwanzo. Kwa hakika jambo hili lilizuliwa baada yake” (Imenukuliwa kutoka kwa Subulul Hudaa war Rashaad cha As-Salihiy, Mj. 1, uk. 439).
Suala la sisi kujiuliza ni kuwa; Je, haya Mawlid yalianza lini? Jawabu ya suala hili kwa mwanachuoni wa Ki-Sunnah, Al-Imaam al-Maqriiziyni:
“Katika kipindi cha uongozi wa Faatwimiyyuun (hawa walikuwa ni Rawaafidh (Mashia) katika kipote cha Ismailiyyah [Makoja] katika nchi ya Misri) walikuwa wanachukuwa hii ni misimu ya sherehe ambapo walikuwa wakiwakunjulia hali za raia zao na kuwakithirishia neema. Na walikuwa hawa watawala wa Faatwimiyyuun katika mwaka mzima wana misimu ya sherehe na Idi zao nazo ni kama zifuatazo: Msimu wa kichwa cha mwaka, Msimu wa mwanzo wa mwaka, Sherehe za ‘Aashuraa, na Mawlid ya Nabii (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Mawlid ya ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu), na Mawlid ya Hasan na Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhuma), na Mawlid ya Faatwimah az-Zahraa (Radhiya Allaahu ‘anha), na Mawlid ya kiongozi wao aliye hai kwa wakati ule, usiku wa kwanza wa Rajab, na usiku wa kati ya Rajab, na Mawlid ya usiku wa Ramadhaan na mwisho wa Ramadhaan na Msimu wa ‘Iydul Fitwr na Msimu wa ‘Iydul Adh-ha na Idi ya Ghaadir, Msimu wa ufunguzi wa Ghuba na Siku ya Nairuuz na Siku ya Ghatas na Siku ya Mazazi, na Siku ya Vipandio, Kis-wa (nguo) ya Msimu wa Kusi na Kaskazi, Alhamisi ya Adasi na Siku ya Ubatizo” (Al-Khutwat, Mj. 1, uk. 490 na baada yake). na amesema tena katika kitabu chengine: “Na katika mwezi wa Rabi’ul Awwal walijilazimisha watu kuwasha kandili usiku katika njia zote na vichochoro vyake huko Misri”.
Na amesema tena al-Maqriiziy katika maudhui nyengine: “Shughuli za Mawlid ya Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilikuwa zikifanyika rasmi kama desturi yake katika mwezi wa Rabi’ul Awwal”. Kila mmoja anatakiwa azingatie jinsi gani Mawlid yalivyoanzishwa pamoja na uzushi mkubwa mfano: Uzushi wa kukataa na kuchupa mipaka juu ya familia ya Mtume kwa kusimamisha mawlid ya ‘Aliy, Faatwimah, Hasan na Husayn.