Muda Unaisha Haraka!
Huu ni ufupisho wa ushuhuda wa Victoria Nehale

Nilizaliwa na kuishi Namibia maisha yangu yote; na niliyatoa maisha yangu kwa Yesu tarehe 06 Februari 2005. Bwana Yesu Kristo ameshanifunulia mambo mengi katika ulimwengu wa roho ikiwa ni pamoja na safari za kuzimu. Bwana alinipa maelekezo kwamba niwashirikishe watu uzoefu wangu; pia alinionya kuwa nisiongeze wala kupunguza chochote katika vile alivyonionyesha na kuniambia. Wakati nikiandika kitabu hiki, mwishoni mwa 2006, nilishatembelewa mara 33 na Bwana Yesu Kristo. Kila aliponitembelea, Bwana alikuwa akiniambia kabla ya kuondoka: MUDA UNAISHA HARAKA!
Safari ya kwanza kuzimu
Katika wikiendi ya tarehe 23 Julai 2005, nilipanda taksi kwa ajili ya safari ya dakika thelathini kutokea mji wa Ondangwa ambako ndiko ninakofanya kazi na kuishi, hadi kijijini kwetu, kwa lengo la kwenda kuwa na wazazi wangu wakati wa wikiendi ile. Wakati nikielekea nyumbani, nilipata hisia kwamba kuna jambo lisilo la kawaida ambalo lingetokea jioni ile. Nilifika nyumbani kwenye saa 12 jioni; na hapo watu walikuwa wanaandaa chakula cha jioni. Nilikuwa jikoni pamoja na familia yetu, huku nikiwa nimelala kwenye mkeka. Watoto wa hapo nyumbani walikuwa wakiimba nyimbo zao za Shule ya Jumapili. Ghafla nilijisikia upako mzito ukinishukia; mwili wangu ukawa dhaifu sana; na nikawa nimetoka kwenye mwili kutokana na nguvu za Mungu. Nilimwona mwanamume amevaa joho jeupe refu likiwa limefungwa kwa kamba ya rangi ileile; akiwa anatembea kuelekea pale nilikokuwa nimelala. Kulikuwa na nuru imemzunguka kana kwamba ilikuwa ikitokea kwake. Alikuwa amevaa viatu vya wazi vya kahawia. Mwonekano wake ulikuwa kama wa watu wa Mashariki ya Kati, huku akiwa na ngozi nzuri ya hudhurungi. Uso wake ulikuwa mpole sana na umejaa utukufu lakini sikuweza kumtazama machoni. Alipoongea, sauti yake ilikuwa ya upole, na upendo, lakini pia yenye mamlaka; mawimbi ya upendo yalikuwa yakitoka kwake.
Alinyoosha mkono wake kwangu na kuninyanyua kutokea pale nilipolala. Ghafla nilijiona nikiwa nina mwili mzuri sana. Nilijiona niko kama nilivyokuwa ningali na miaka kumi na nane. Nilikuwa nimevaa joho jeupe na kamba nyeupe. Japokuwa joho langu lilikuwa jeupe, lilitengenezwa kwa matirio tofauti na ya joho la yule mwanamume. Joho lake lilikuwa la hariri huku liking’aa kiasi kwamba hata nashindwa namna ya kuelezea.
Alisema, kwa sauti ya upendo na upole sana: “Victoria, nataka uende nami; nitakuonyesha mambo ya kuogopesha na ninakupekela mahali ambako haujawahi kufika katika maisha yako.” Alinishika mkono wa kulia na tukaondoka. Nilijiona kama vile tunatembea hewani na muda wote tulikuwa tukielekea tu juu. Baada ya muda, nikawa nimechoka sana, na nikamwambia kuwa nisingeweza kuendelea na safari. Hivyo nikamsihi aniruhusu nirudi. Hata hivyo, alinitazama kwa upendo na kusema, “Haujachoka – uko sawa tu. Kama ukichoka, nitakubeba, lakini kwa hivi sasa uko tu sawa. Amani iwe kwako. Tuendelee.”
Tulifika mahali ambako ni pakavu sana; pakavu kuliko jangwa lolote analojua binadamu; hakukuwa na dalili zozote za uhai. Hakukuwa hata na mti mmoja au hata jani au kiumbe chochote hai. Lilikuwa ni eneo linalofadhaisha sana.

