Mutee'a Al-Fadi alikuwa ni Mwislamu mwenye msimamo mkali wa Wahabbi ambao alisomea kule Saudi Arabia. Lakini baada ya kukutana na upendo wa Yesu, moyo wake uligeuka kabisa na akaanza kuitafuta kweli iliko. Hatimaye alitambua kuwa Yesu ndiye Njia, Kweli na Uzima. Ufuatao ndio ushuhuda wake:
****************
Mimi nilikuwa Muislamu wa Wahabbi ambaye nilizaliwa na kulelewa kama Mwislamu nchini Saudi Arabia. Katika maisha yangu yote nilikuwa mfuasi mwaminifu wa Kiislamu ambaye nilifuata na kuishi mafundisho ya Uislamu katika kila eneo la maisha yangu. Mafundisho haya yalikuwa ni pamoja na imani:
- kwamba Uislamu ndio dini ya mwisho duniani;
- kwamba ndiyo dini pekee inayokubalika kwa Mungu;
- kwamba ndiyo njia ya kwenda Mbinguni;
- kwamba wale wasioukubali Uislamu wanakwenda jehanamu na kwamba matendo na ibada zao hazitawaokoa hadi watakapomkubali Allah kama Mungu wao na Muhammad kama mtume wake;
- kwamba wokovu kwa Mwislamu ni kwa njia ya matendo mema na hauna uhakika isipokuwa kwa wale walio tayari kufa kwa jina la Allah;
- kwamba Waislamu ni watu bora kuliko wengine;
- kwamba watu wote wasio Waislamu ni makafiri, ikiwa ni pamoja na Wakristo;
- kwamba Kristo alikuwa ni mwanadamu tu na nabii aliyetumwa na Allah;
- kwamba yeye si Mungu au Mwana wa Mungu;
- kwamba hakuwahi kusulubiwa, kufa msalabani au kufufuka kutoka kwa wafu;
- kwamba Yesu alipaishwa Mbinguni ili kuokolewa dhidi ya waliotaka kumuua na
- kwamba Yesu atakuja tena siku za mwisho ili kuujenga upya Uislamu kama dini ya kweli ya Allah, kuharibu msalaba, kumuua mpinga-Kristo, na kuwafanya Wakristo wawe Waislamu.
Lakini jambo lenye nguvu zaidi ambalo nilijifunza katika makuzi yangu ni kuwa na CHUKI dhidi ya wale wote wasiomwabudu Allah; wasiomfuata Muhammad; wasioamini Uislamu – ikiwa ni pamoja na Wakristo na Wayahudi. Kwa lugha rahisi ni kwamba, nilikuwa adui wa Kristo.
Katika umri wa miaka 12, nilikuwa nimeshakariri nusu ya Qur’an. Lengo langu lilikuwa kukariri kitabu chote; maana huwa tunafundishwa kwamba kukariri Qur’an kunasaidia kufunika baadhi ya dhambi zako na kuboresha matendo yako mema Siku ya Hukumu; pia kunakupandisha daraja mbinguni.


