Marehemu Ahmed Deedat
Waislamu wanashikilia kwamba Muhammad alitabiriwa kwenye Biblia. Andiko lao kuu wanalotumia kutetea hoja hii ni Kumbukumbu la Torati 18:18. Andiko hilo linasema:
Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.
Haya ni maneno ambayo aliambiwa Musa na Yehova.
Mmojawapo wa watu ambao walijaribu sana kuonyesha kuwa andiko hili lilimhusu Muhammad, alikuwa ni mwanaharakati wa Kiislamu, marehemu Ahmed Deedat wa Afrika Kusini.
Unaposoma au kusikiliza sababu wanazotoa ili kuthibitisha madai yao hayo, kwa kweli ni sababu zenye nguvu sana (kwa mtu ambaye haelewi Biblia); ingawaje hazina uzito hata chembe ukijua Biblia inasema nini katika ujumla wake na ni nini makusudi na malengo ya Mungu kwa uzao mzima wa Adamu.
Siku moja Ahmed Deedat alimkaba mchungaji mmoja kwa maswali kuhusu mstari huu wa Kumbukumbu 18:18 kiasi kwamba, kwa maneno yake, Deedat anasema kuwa mchungaji yule alikosa cha kusema.
Deedat alimpomsomea mstari huo, alimwuliza, “Unabii huu unamhusu nani?”
“Unamhusu Yesu,” mchungaji alijibu.
“Unajua,” alisema Deedat, “Maneno ya msingi kabisa kwenye unabii huu ni ‘mfano wako’. Sasa, ni kwa vipi Yesu ni mfano wa Musa?”
“Musa alikuwa Myahudi na Yesu alikuwa Myahudi. Pili, Musa alikuwa nabii na Yesu alikuwa nabii,” alijibu mchungaji.
Deedat anaendelea kusema, “Kama hizi ndizo sababu mbili pekee zinazotuwezesha kumtambua mhusika wa unabii huu wa Kumbukumbu 18:18, basi unabii huu unaweza kumhusu yeyote kati ya wafuatao baada ya Musa: Sulemani, Isaya, Ezekieli, Danieli, Hosea, Yoeli, Malaki, Yohana Mbatizaji, n.k. maana hawa wote nao walikuwa Wayahudi na pia manabii. Kwa nini basi useme kuwa unabii huu unamhusu Yesu na si hawa wengine?”