Ndugu Msomaji: Leo ningependa tujikumbushe jambo Fulani kuhusu maisha yetu ya kila siku.
Hebu kwanza tusome neno la Mungu kama lilivyo andikwa katika Isaya:
Isaya 42:22‘Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.’
Inawezekana kabisa labda huelewi kuwa, shida zako zote zimesemwa katika hii aya hapo juu. Labda hufahamu kuwa wewe ni tajiri na Shetani amekuwa akikuibia mali zako. Labda hufahamu kuwa wewe ni Msomi na ulitakiwa uwe na Madigirii kadhaa. Labda hufahamu kuwa wewe ni Kiongozi Fulani ambae ameibiwa uongozi wake, “nyota yako”.
Leo ningependa ufahamu kuwa Shetani ni Mwizi na anaweza kukuibia wewe unae soma huu ujumbe. Ningependa ujiulize, hivi, Je, huyu Shetani alikuibiaje wakati wewe ni mtoto wa Mungu na umeokoka?
Katika Injili kutokana na Yohana 10:10 inasema kuwa: Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.
Mpendwa katika Bwana. Ningependa ufahamu kuwa, hiyo ndio kazi kuu ya Shetani katika Maisha ya Mkristo. Shetani amekuja kukuibia mali zako, labda amekuja kukuibia amani yako ya wewe na familia yako. Labda amekuja kukuharibia watoto wako. Ndugu msomaji, jibu tunalo na tumekuwa nalo kila siku, lakini tumeshindwa kulitumia. Isaya anasema kwenye aya hiyo hiyo kuwa “wala hapana asemaye, rudisha”
Je, wewe umesha wai mwambia Shetani arudishe mali zako? Labda kwasababu hukuwai ziona na aliziiba kabla ya wewe kuzishika, haimaanishi kuwa wewe sio tajiri. Baba yetu aliye Mbinguni ni Tajiri Mkuu, hivyo elewa kuwa, wewe kama motto wake ni Tajiri vile vile. Hebu jisifie kidogo kuwa, wewe ni motto wa tajiri. Sema hivyo na anza kukiri kuwa wewe ni tajiri na sio maskini.
Biblia inasema katika Isaya 42:18 kuwa, tutoke kwenye upofu, tumebaki kuridhika na hali mbaya tuliyonayo tukiona amani tu! Kumbe tuko vipofu! Hatuoni uhalisia.
Leo ningependa ufungue macho yako ya Kiroho na uelewe kuwa, Mungu anakupenda na anataka utoke kwenye upofu. Mungu anataka usiridhike na kidogo ulicho nacho. Mungu anataka usikubali kuwa hali mbaya ni ya kwako. Leo nakuomba ufumbue macho yako na umwambie Shetani rudisha mali zangu zote ulizo ziiba katika jina la Yesu. Mwambie Shetani akurudishie fedha zako zote alizo ziiba ukiwa na ufahamu na au bila ya ufahamu. Mpendwa katika Bwana. Mungu wetu ni Upendo na anatupenda ndio maana alimtoa Mwana wake wa pekee ali aje na afe kwa ajili ya matatizo yetu yote. Matatizo ya Kifedha, matatizo ya magonjwa. Matatizo ya kifamilia. Kikazi, kishule. Kila aina ya matatizo Yesu aliyamaliza pale Msalabani. Ndio maana Yesu alisema kabla ya kukata roho kuwa “IMEKWISHA”.
Sasa anza kumwabia Shetani kuwa ameshindwa kwa Jina la Yesu. Mwambie kuwa leo unafahamu kuwa wewe ni mtoto wa Mungu na umebarikiwa na Mungu aliye juu. Mwabie Shetani kuwa kuanzia leo, hana mamlaka na mali zako zote. Mwambie kuwa kuanzia leo, hana mamlaka na familia yako katika Jina la Yesu. Mwambie kuwa Ushindi ni wako katika Jina la Yesu. Mkumbushe Shetani kuwa aliye ndani yako ni Mkuu kuliko yeye aliye nje. Mwambie kuwa Damu ya Yesu imekuzingira na mteketeza na msambaratishe kwa kutumia Damu ya Yesu. Vunja uovu wake wote alio ufanya katika maisha yao. Vunja uchawi wote alio ufanya katika maisha yako kwa kutumia Damu ya Mwana Kondoo katika Jina la Yesu. Vunja hila zote alizo zifanya kwako kwa kutumia Damu ya Yesu. Vunja kila aina ya uovu, wizi, uchawi, uongo alio ufanya kwako kwa kutumia Damu ya Yesu.
Mambo yanaweza kufichwa machoni pako usiyaone, na inakuwa hasara kubwa sana lakini kama ungeona, ungetengeneza. Tunatakiwa tutambue majira ya kujiliwa kwetu. Haya ndio yale majira Yesu anataka kurudisha heshima ya jina lake, majira ambayo Yesu anataka kufanya falme za dunia ziwe zake.
Isaya anasema unaona mambo mengi lakini huyatii moyoni, kwanini inakuwa hivyo ndo linapokuja swala la Isaya 42:22 kwamba huyu mtu anakuwa ameibiwa moyo, macho ndo mana anaona lakini hatii moyoni nk.
Akina Daudi walivyorudi na kukuta mji wao umechomwa moto na kila kitu kimeibiwa hadi wakeze. Wanaume wakaanza kulia hadi wakaishiwa nguvu lakini haikuwa suluhisho! Daudi akaona hili jambo suluhisho si kulia bali ni kuingia mbele za BWANA, kutafuta suluhisho, hata wewe ndugu yangu haijalishi una tatizo kiasi gani, wazazi , ndugu , marafiki , bunge na vyote hapa duniani haviwezi kukusaidia, muige Daudi kwa kumwangalia Yesu maana yeye ndiye mwenye funguo za mauti na kuzimu. Daudi akaruhusiwa na BWANA aende na atarudisha vyote ndipo Daudi alipowaongoza wenzie na kwenda na hakika walirudisha vyote.
1Sam 30:1 ‘Basi Daudi na watu wake walipoufikilia mji, tazama, ulikuwa umechomwa moto; na wake zao, na watoto wao, waume kwa wake, wamechukuliwa mateka. ………………. Basi Daudi na watu wake walipoufikilia mji, tazama, ulikuwa umechomwa moto; na wake zao, na watoto wao, waume kwa wake, wamechukuliwa mateka……… Daudi akauliza kwa Bwana, akasema, Je! Nikiwafuata jeshi hili, nitawapata? Naye akamjibu, Fuata; kwa kuwa hakika utawapata, nawe hukosi utawapokonya wote. Basi Daudi akaenda, yeye na wale watu mia sita waliokuwa pamoja naye……. Naye Daudi akawapiga tangu ukungu wa jioni hata jioni ya siku ya pili; hakuna aliyeokoka, ila vijana mia nne waliopanda ngamia na kukimbia.
18 Daudi akawapokonya wote waliokuwa wamechukuliwa na Waamaleki; naye Daudi akawaokoa wakeze wawili.
19 Wala hawakupotewa na kitu, mdogo wala mkubwa, wana wala binti, nyara wala cho chote walichojitwalia hao; Daudi akavirudisha vyote. ….’
Leo tunaenda kulifuatilia jeshi la shetani na kurudisha vyote, kwa msaada wa BWANA itawezekana.2 Samw 22:30 ‘Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi; Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta.
31 Mungu njia yake ni kamilifu; Ahadi ya Bwana imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia..’.
Yoh 5:28 ‘..msistaajabie maneno haya kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.
29 Nao watatoka; ..’
yaani haijalishi shetani aliwapataje pataje, iwe kiuhalali au vinginevyo, mimi najua neno moja tu ‘NAO WATATOKA’
Isaya 49:24 ‘ Je! Aliye hodari aweza kunyang'anywa mateka yake, au jeshi lao waliofungwa halali wataokoka? 25 Naam, Bwana asema hivi, Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka;……’
Isaya 14:17 ‘ Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao? 17 Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao? ’
SASA FANYA MAOMBI HAYA HAPA CHINI NA AMINI KUWA USHINDI NI WAKO







