Wednesday, February 6, 2019

JE, MCHEZO WA “KU-BETI” NI DHAMBI?

Image may contain: 1 person, sitting and indoor
Na Pastor Zakayo Nzogere
JE, MCHEZO WA “KU-BETI” NI DHAMBI?
Kati ya mambo mapya na yenye mvuto usio wa kawaida kwa watu wa rika zote, ni mchezo wa KU-BETI. Kuna makampuni mengi ambayo yanasimamia mchezo wa KU-BETI kama vile BetWay, Bet365, BetOnline, SportPesa, na mengine mengi.
Swali kubwa ambalo WAPENDWA wengi wanajiuliza ni kama mchezo huu ni halali kwa Mkristo kuucheza?
Mimi sina majibu ya moja kwa moja, ila nitatoa mtazamo wangu binafsi kwa kutumia Maandiko. Pia ninaomba na wengine muwe huru kutoa MITAZAMO yenu CHANYA ili kwamba tuweze kuwa na UELEWA mpana wa jambo hili.
MASWALI YA MSINGI YA KUJIULIZA:
• Dhambi ni nini?
• Kuna tofauti gani kati ya ku-beti, kamari, na bahati nasibu?
• Je, Biblia inasemaje kuhusu michezo ya bahati nasibu? & Je, ku-beti kunawezaje kuathiri maisha ya Mkristo?
1. DHAMBI NI NINI?
Biblia inafafanua dhambi kama uasi au kutotii maagizo ya Mungu. Adamu na Hawa walifanya dhambi ya kutotii maagizo ya Mungu, matokeo yake ni kwamba mahusiano yao na Mungu yakaharibika. Dhambi ikawatenga mbali na uso wa Mungu na nguvu ya mauti ikaanza kutawala (Mwanzo 3).
DHAMBI ni kitu kinachomtenga mwanadamu na Mungu. Hata hivyo Mungu hakupenda kuwaacha wanadamu waangamie katika dhambi yao; akamtuma Yesu Kristo aje kutukomboa (Yohana 3:16). Dawa ya dhambi ni KUMWAMINI BWANA YESU KRISTO.
2. KUNA TOFAUTI GANI KATI YA KUBETI, KAMARI, NA BAHATI NASIBU?
Kwa mtazamo wangu, michezo hii yote ni michezo ya kubashiri au kutabiri nani atakae shinda au shindwa katika jambo fulani. Kwa hapa Tanzania, mchezo wa Ku-beti na Bahati Nasibu ni michezo ambayo imepewa vibali vya Serikali na ni michezo halali nchini. Kwa upande mwingine, KAMARI, ambayo kimsingi haina tofauti na hiyo mingine, yenyewe ni haramu kucheza. Kwangu mimi hii ni sawa na kuruhusu KONYAGI/WISKI na kukataza GONGO!!
3. JE, BIBLIA INASEMAJE KUHUSU MCHEZO WA KU-BETI AU BAHATI NASIBU; NA JE, INAWEZAJE KUATHIRI WOKOVU?
Biblia siyo kama MANUAL BOOK/KITABU CHA MAELEZO chenye mchanganuo wa kila kitu kinachohusu maisha ya wanadamu. Hata hivyo, Biblia kama Neno la Mungu, imejaa KANUNI ZA MSINGI (Principles) zinazoweza kutupa majibu na misimamo kuhusu mambo mbali mbali katika maisha yetu.
MFANO; hakuna mahali kwenye Biblia ambapo inakataza kuvuta sigara au kutumia madawa ya kulevya. Lakini Biblia inatoa kanuni ambayo imepelekea Kanisa kupiga marufuku matumizi ya vitu hivyo (1 Wakorintho 3:16-17; 6:19-20). Maandiko yanatuonyesha kuwa MIILI YETU NI HEKALU LA ROHO MTAKATIFU, pia Mungu atamhukumu yeye atakayeuharibu mwili wake.
Kwa upande mwingine WANASAYANSI wametuonyesha kwamba vileo na vitu kama bangi, madawa ya kulevya na sigara vina madhara makubwa sana kwa mwili wa mwanadamu. Hivyo basi KANISA linatumia KANUNI za Neno la Mungu kukataza matumizi ya vitu hivyo.
Vile vile Biblia inatupa kanuni nyingi zinazotuonya kuhusu kupenda pesa, tamaa, na kujilimbikizia mali kwa njia ambazo si halali.
JE, KU-BETI KUNAWEZA KUATHIRI WOKOVU?
Hili swali ni gumu sana. Kwa mtazamo wangu, mchezo wa ku-beti unaweza usiwe dhambi lakini ni kitu ambacho mazingira yake yanaweza kupelekea mtu kuuchafua Ukristo/wokovu wake. Siwezi sema kwa kucheza mchezo huo Mkristo ataikosa Mbingu, lakini anaweza kuharibu ushuhuda na maisha ya kiroho kwa namna mbalimbali kama:
• Itamfanya Mkristo asiweze kutuliza mawazo yake katika kumtafakari Mungu na Neno lake, badala yake atakuwa anawaza ni timu gani itashinda.
• Inaweza chochea UVIVU miongoni mwa Wakristo na jamii kwa ujumla.
• Inaweza athiri huduma na vipawa kwa sababu mchezo wa Ku-beti unachukua muda mwingi wa mtu.
• Itaharibu hata MAOMBI YA MKRISTO…. Yeye atakuwa anaomba MUNGU Team aliyoiwekea pesa ishinde. Endapo wapendwa wamebeti timu mbili tofauti, basi mmoja atashangilia kwamba maombi yake yamejibiwa na mwingine atajiona kana kwamba Mungu hajajibu. Kimsingi wote watakua wakiomba MAOMBI BATILI.
TUFUATE USHAURI WA MTUME PAULO:
1 WAKORINTHO 6:12 (BHN); “Mtu anaweza kusema: “Kwangu mimi kila kitu ni halali.” Sawa; lakini si kila kitu kinafaa. Nakubali kwamba kila kitu ni halali kwangu lakini sitaki kutawaliwa na kitu chochote.”
WARUMI 14:21 (BHN); “Afadhali kuacha kula nyama, kunywa divai, au kufanya chochote ambacho chaweza kumsababisha ndugu yako aanguke.”
1 WAKORINTHO 8:9,13 (BHN); “Lakini, jihadharini: Huu uhuru wenu usiwafanye walio na imani dhaifu waanguke katika dhambi… Kwa hiyo, ikiwa chakula husababisha kuanguka kwa ndugu yangu, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi.”
NB: KU-BETI KUNAWEZA KUWA KAMA ULEVI (ADDICTION) NA KUMFANYA MTU KUWA MTUMWA.
Shalom,

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW