Katika sehemu ya kwanza ya ushuhuda huu wa Nabeel, aliyekuwa Mwislamu kisha akakutana na Bwana Yesu na kupokea wokovu, tuliona jinsi ambavyo alimwomba Mungu ampe maono yatakayomwonyesha imani ya kweli. Alionyeshwa misalaba kwenye maono lakini yeye akasema labda ni macho yake tu yamemchezea mchezo. Kwa hiyo, alimwomba tena Mungu kwamba, kama yale maono yalitoka kwake, basi ayathibitishe kwa ndoto. Je, Mungu alifanya nini? Tafadhali endelea kusoma sehemu hii ya pili.
…………………………………
Mungu alinipatia ndoto ile kwa uwazi sana kiasi kwamba sikuwa na ulazima wa kuitafsiri. Lakini ilikuwa wazi hata zaidi kuliko nilivyotarajia. Saa chache baadaye niliwasiliana na David na kumwambia kuwa nimeota hivi na hivi.
David aliniambia, “Sina ulazima wa kutoa maoni yangu juu ya hilo. Kila kitu kiko kwenye Biblia.”
Nikasema, “Unasemaje?”
Akasema, “Nenda kwenye Luka 13.”
Nilienda kwenye Luka 13 mstari wa 22 hadi 29. Niliposoma nikakuta kumeandikwa kuhusu kuingia kwenye Ufalme wa Mungu, na Kristo akasema kwamba, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza. Jitahidini kuingia kupitia mlango mwembamba. Na watu watakuwa wamesimama kwenye mlango huo wakibisha hodi.
Na hicho hasa ndicho kilichotokea kwenye ndoto yangu. Nilikuwa kwenye huo mlango ambao ulikuwa haujafungwa bado. Fursa ya mimi kuingia humo kwenye kushiriki sherehe ile ilikuwa bado ipo. Nilichotakiwa tu kufanya ni kukubali mwito.