Siku hizi tunaishi katika enzi za sayansi, teknolojia na maendeleo makubwa ya kompyuta. Ni wakati ambao sayansi inaenea kupita kiasi katika pande zote. Katika kipindi tulicho nacho mwanadamu anaweza kuchambua muundo na umbile la ‘molekuli’ na kufanya utafiti kuhusu asili yake. Kupitia njia ya teknolojia ya vinasaba mwanadamu anaweza kuchagua aina ya mnyama au mmea anaotaka kuukuza. Maendeleo haya ya kisayansi yanatufanya tujiulize ikiwa uvumbuzi huu unapingana na ukweli wa Biblia au ikiwa sayansi inakanusha Biblia. Ukweli ni kuwa tunaweza kuiamini sayansi, kuitegemea na kuitumia kuthibitisha kweli zinazopatikana katika Biblia. Mara nyingi watu wasio na elimu ya kutosha na wanaoegemea upande mmoja ndio wanaofikiria kuwa Biblia na sayansi ni vitu viwili vinavyopingana. Misimamo inayofuatwa na baadhi ya watu ya kuwa na imani inayokataa kufikiri na kufikiri kunakokataa imani, ni misimamo hatari isiyotupeleka kwenye ukweli.
Ili tupate jibu kuhusu swali letu lililohoji ikiwa maelezo yaliyoko ndani ya Biblia ni ya kuaminika yakilinganishwa na maelezo ya sayansi, inatubidi kulinganisha maelezo ya pande mbili. Kwa kuwa hatuna muda wa kutosha kujibu swali hili kwa undani, nitazungumzia mifano michache tu inayohusu tafiti na chunguzi za kisayansi zinazohusu elimu ya mambo ya kale, elimu ya sayansi ya mazingira, historia, jiografia, fizikia ya uchunguzi wa miamba, sayansi ya kompyuta na sayansi ya utabibu. Hata maelezo yanayotokana na sayansi ya fizikia na elimu ya uchunguzi wa miamba kuhusu mwenendo na umbile la dunia yanapatana kabisa na maelezo ya Biblia. Mifano ya maelezo haya ni pamoja na yale yanayohusu gharika, utumwa katika nchi ya Misri, kushambuliwa kwa mji wa Yerusalemu, ustaarabu wa miji ya kale kama vile Babeli, Tiro, Sodoma na Gomora. Habari zilizoandikwa katika Biblia kuhusu mifano hii zinaweza kuhakikishwa kwa ushahidi ulioandikwa.
Kwa kuwa matokeo ya tafiti za kisayansi yanathibitisha habari zinazopatikana katika Biblia, inaonyesha wazi kuwa sayansi, inathibitisha kuwa habari zinazopatikana katika Biblia ni za kweli. Ukweli huu unatupa kuamini habari zote tunazokutana nazo katika Biblia. Tunapotafakari upekee wa Biblia, tunaweza kuelewa sababu zinazowafanya watu mashuhuri kuiheshimu na kuipenda, kuliko vitabu vingine vilivyoko chini ya jua. Yafuatayo ni maelezo mafupi ya mtu aliyeipenda Biblia licha umashuhuri aliokuwa nao katika ulimwengu wa sayansi.
“Siku moja mwaka 1890, wanaume wawili walikuwa wakisafiri kwa treni kutoka mji wa Lyon kwenda Paris. Mmoja alikuwa mzee mwenye ndevu nyingi na mvi anayekadriwa kuwa na umri wa miaka 65. Msafiri wa pili alikuwa kijana aliyejulikana kwa jina la Gaston Leroux, mwenye umri wa miaka 25 hivi. Kijana huyu alikuwa anakwenda kuhudhuria semina katika asasi ya Profesa mashuhuri nchini Ufaransa ndugu Louis Pasteur. Katika kusafiri kwao walijikuta katika mazungumzo yaliyokuwa na shabaha ya kufahamiana. Baada ya yule kijana kueleza dhumuni la safari yake, yule mzee alimjibu na kusema. “Ndugu nimefurahi kusikia kuwa unataka kuendeleza kiwango chako cha elimu, sayansi unayotaka kujifunza ni muhimu kutokana na ukweli kuwa itakusaidia kuthibitishia ukuu wa kipekee unaohusu uumbaji. Bila shaka wewe ni mwamini.”
Yule kijana alimwangalia yule mzee kwa macho ya dharau na kusema, “kuamini maana yake ni nini? Ninachojua ni kuwa sayansi inaweza kujitegemea bila huyo Mungu mwenye upendo unayemzungumzia.” Yule mzee kwa heshima na unyenyekevu huku akiwa ameshikwa na butwaa, alimjibu kwa kusema: “Ndugu yangu huo ni mtizamo wako na baadhi ya wasomi wana mtizamo unaofanana huo ila ukweli ni kuwa, sayansi ya kweli ….” Kufikia hapo yule kijana aliingilia kati huku akiwa amekasirika na kusema, “ninafikiri tofauti kabisa na vile unavyofikiri; sayansi unayoizungumzia ni ya zamani na haifanyi kazi katika siku tulizo nazo. Sayansi ya leo ni ya tofauti kabisa na imepiga hatua kiasi cha kutomhitaji Mungu wala usaidizi wowote kutoka kwake.”
.jpg)





