Katika makala yaliyopita tuliona hoja za ndugu wa Kiislamu wanavyojaribu kwa juhudi nyingi kuonyesha kwamba Muhammad ametabiriwa kwenye Biblia.
Katika makala hayo niliahidi kuwa nitaeleza jinsi ambavyo hoja zao hazina ukweli wowote. Licha ya kwamba Mungu wanayemwamini amewahakikishia kwamba Muhammad ametajwa kwenye Biblia, ukweli ni kwamba hajatajwa hata kidogo!
Katika sehemu ya kwanza ya mfululizo huu, nilimalizia kwa kunukuu kile ambacho Yehova, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, anasema juu ya Neno lake. Hebu tuangalie tena baadhi ya maneno hayo. Imeandikwa:
Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho,tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni.
Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu. (1 Wakorintho 2:12-15).
Tatizo mojawapo kubwa ninaloliona mara nyingi kwenye Uislamu na Waislamu ni kutazama mambo kwa jinsi ya mwili. Hapo ndipo penye shida kubwa yanapokuja masuala ya rohoni.
Kama uko kwenye safari ya kimaisha katika ulimwengu wa kimwili na unalenga kuishia kwenye ulimwengu wa kiroho (jambo ambalo ndilo linaloendelea kwa wanadamu wote), basi ni lazima utafute maana ya mambo ya ulimwengu wa mwilini kulingana na ulimwengu wa rohoni. Ukiishia tu kutazama mambo katika mwili, una hasara kubwa!!
Ni lazima kutambua kuwa Mungu hatupi ujumbe wake ili tuweze kuwa matajiri, maarufu na wenye vyeo wa hapa duniani. Kama hayo ndiyo malengo yako makuu katika maisha haya, basi wewe una hasara kuliko watu wote. Hayo si mambo ya msingi. Mungu ametuweka duniani kwa makusudi makubwa zaidi ya hayo. Yeye analenga mambo yadumuyo; si mambo ya kupita. Hivyo, kiini hasa cha ujumbe wa Mungu wa kweli ni maisha ya milele yajayo kwenye ulimwengu wa roho.
Sasa, kwa kuwa ndugu zangu hawa, wao wako zaidi katika mambo ya hapa duniani, ya kimwili, haishangazi basi kumwona Ahmed Deedat na wenzake wakiishia kuangalia tabia za kimwili za Musa na kuzilinganisha na tabia za kimwili za Muhammad na kusema kwamba eti, huo ndio uthibitisho kwamba maandiko ya Biblia wanayonukuu yanamzungumzia Muhammad.





