
Baada ya kusoma kwa undani Sehemu ya Tano kuhusu aina ya mavazi ya kisabato na au ya kitorati, hebu tuangalie aina za Sabato ambazo wana wa Israeli walipewa.
Sasa nitaanza kuelezea kuhusu mwanzo wa hii Sabato na Mungu alitoa hili agiza kwa nani. Kwa mara ya kwanza kabisa, Mwenyezi Mungu anatoa agizo kwa wanadamu, la kushika sheria kuhusu siku ya sabato, lilitolewa kwa Wana wa Israeli tu, na kwa mkono wa Nabii Musa. Hivyo basi, sio kosa nikisema kuwa hata Israeli mwenyewe yaani Yakobo alipo kuwa hai, hakuwai sikia habari ya kupumzika siku ya saba (sabato) na au Mungu hakuwai mwambia kuwa ashike Sabato.
Agizo hili la kuhusu siku ya saba, “Sabato” halikutolewa kwa mataifa mengine, bali kwa wana wa Israeli tu, na sababu kuu ya kupewa wana wa Israeli peke yao ni kwamba, katika karne hiyo, ni wana wa Israeli peke yao ndiyo waliokuwa wanamjua Mungu wa kweli yaani Yehova. Ni kwa sababu hiyo ya kumjua Mungu wa Kweli kabla ya mataifa mengine, Mungu aliwapa sheria (Torati), yaani Amri kumi “Ndio maana huwa nasema Amri kumi hazikuwa kwa Mataifa yote” ingawa si kosa kuzifuata.
Zaidi ya hapo, Mungu alitoa kwa wana wa Israeli sheria nyingine 613 na Hukumu zake.
UTHIBITISHO: Kumbukumbu la Torati 4:7-8 Biblia inasema, “Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.” Sasa tumsikilize Musa: Musa mwenyewe alithibisha kwamba, sheria ya kushika siku ya sabato na sheria nyingine haikuanza na baba zao, bali ilianza na wao wenyewe yaani wana wa Israeli.
UTHIBITISHO: Kumbukumbu la torati 5:1-3 Biblia inasema, “Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na hukumu ninenazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuangalia kuzitenda. Bwana Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu. Bwana hakufanya agano hili na baba zetu, bali na sisi, yaani sisi sote tulio hapa, tu hai.”
Musa anathibitisha kwa kutumia aya hapo juu kuwa hata baba zao hawakupewa Sheria. Sasa, Wasabato wanapo sema kuwa eti Adam alipewa sheria ya kutunza Sabato wanatoa wapi haya madai yao yasio na uthibitisho wa aya?
Kigezo ambacho Wasabato wa leo wanachotumia, ni kwamba Mungu alipumzika siku ya saba, hivyo husema kwamba, Adamu naye alipumzika ingawa Biblia haituambii kama Adamu alipumzika na hakuna kabisa uthibitisho wa aya Zaidi ya madai hewa. Sasa tuwaulize Wasabato, kama Adam alipumzika, alipumzika kwa sababu ya kazi ipi aliyoifanya? Musa ambaye ndiye aliyekuwa msabato halisi, anaipinga hoja hii katika mistari tuliyosoma hapo juu kwa kusema kwamba, Mungu hakufanya agano la zile sheria na baba zao, bali wao wenyewe. Kwa hiyo ni wazi kabisa, kuanzia Adamu mpaka Yakobo hawakuwahi kuambiwa na Mungu juu ya sheria ya kushika siku ya sabato.
JE, UNAZIFAHAMU IDADI YA SABATO AMBAZO WANA WA ISRAELI WALIAMRIWA KUZISHIKA NA MALENGO YAKE?









