Wednesday, October 26, 2016

NENO LA MUNGU LINASEMA NINI KUHUSU SABATO? (SEHEMU YA SITA)


Baada ya kusoma kwa undani Sehemu ya Tano kuhusu aina ya mavazi ya kisabato na au ya kitorati, hebu tuangalie aina za Sabato ambazo wana wa Israeli walipewa.
Sasa nitaanza kuelezea kuhusu mwanzo wa hii Sabato na Mungu alitoa hili agiza kwa nani. Kwa mara ya kwanza kabisa, Mwenyezi Mungu anatoa agizo kwa wanadamu, la kushika sheria kuhusu siku ya sabato, lilitolewa kwa Wana wa Israeli tu, na kwa mkono wa Nabii Musa. Hivyo basi, sio kosa nikisema kuwa hata Israeli mwenyewe yaani Yakobo alipo kuwa hai, hakuwai sikia habari ya kupumzika siku ya saba (sabato) na au Mungu hakuwai mwambia kuwa ashike Sabato.
Agizo hili la kuhusu siku ya saba, “Sabato” halikutolewa kwa mataifa mengine, bali kwa wana wa Israeli tu, na sababu kuu ya kupewa wana wa Israeli peke yao ni kwamba, katika karne hiyo, ni wana wa Israeli peke yao ndiyo waliokuwa wanamjua Mungu wa kweli yaani Yehova. Ni kwa sababu hiyo ya kumjua Mungu wa Kweli kabla ya mataifa mengine, Mungu aliwapa sheria (Torati), yaani Amri kumi “Ndio maana huwa nasema Amri kumi hazikuwa kwa Mataifa yote” ingawa si kosa kuzifuata.
Zaidi ya hapo, Mungu alitoa kwa wana wa Israeli sheria nyingine 613 na Hukumu zake.
UTHIBITISHO: Kumbukumbu la Torati 4:7-8 Biblia inasema, “Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.” Sasa tumsikilize Musa: Musa mwenyewe alithibisha kwamba, sheria ya kushika siku ya sabato na sheria nyingine haikuanza na baba zao, bali ilianza na wao wenyewe yaani wana wa Israeli.
UTHIBITISHO: Kumbukumbu la torati 5:1-3 Biblia inasema, “Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na hukumu ninenazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuangalia kuzitenda. Bwana Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu. Bwana hakufanya agano hili na baba zetu, bali na sisi, yaani sisi sote tulio hapa, tu hai.”
Musa anathibitisha kwa kutumia aya hapo juu kuwa hata baba zao hawakupewa Sheria. Sasa, Wasabato wanapo sema kuwa eti Adam alipewa sheria ya kutunza Sabato wanatoa wapi haya madai yao yasio na uthibitisho wa aya?
Kigezo ambacho Wasabato wa leo wanachotumia, ni kwamba Mungu alipumzika siku ya saba, hivyo husema kwamba, Adamu naye alipumzika ingawa Biblia haituambii kama Adamu alipumzika na hakuna kabisa uthibitisho wa aya Zaidi ya madai hewa. Sasa tuwaulize Wasabato, kama Adam alipumzika, alipumzika kwa sababu ya kazi ipi aliyoifanya? Musa ambaye ndiye aliyekuwa msabato halisi, anaipinga hoja hii katika mistari tuliyosoma hapo juu kwa kusema kwamba, Mungu hakufanya agano la zile sheria na baba zao, bali wao wenyewe. Kwa hiyo ni wazi kabisa, kuanzia Adamu mpaka Yakobo hawakuwahi kuambiwa na Mungu juu ya sheria ya kushika siku ya sabato.
JE, UNAZIFAHAMU IDADI YA SABATO AMBAZO WANA WA ISRAELI WALIAMRIWA KUZISHIKA NA MALENGO YAKE?

Wana wa Israeli katika sheria ya kushika sabato, hawakupewa sheria moja tu, yaani sabato ya siku, kama wanavyofanya wanaojiita Wasabato wa leo. Kwa mtu mwenye ufahamu sahihi wa maandiko na au anaye taka kuelewa maandiko, anaweza akahoji maswali mengi, na ya msingi sana dhidi ya Wasabato wa leo.
Hebu sasa tuangalie idadi ya sabato ambazo wana wa Israeli waliamriwa kuzishika.
UTHIBITISHO: Walawi 26:2 Neno la Mungu linasema, “Zishikeni SABATO ZANGU, na kupastahi patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.” Tunaona hapa Mungu anatumia WINGI ‘sabato zangu’ na siyo ‘sabato yangu’. Tukiangalia katika Ezekieli 20:20 Biblia inasema, “Zitakaseni SABATO ZANGU; nazo zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.” Tunaona na hapa Mungu anasema ZITAKASENI NA SIO ITAKASENI, na anatumia tena neno ‘sabato zangu’ na siyo ‘sabato yangu’.
UTHIBITISHO: Kutoka 31:13 inasema, “Kisha, nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika SABATO ZANGU, kwa kuwa ni ISHARA kati ya mimi na ninyi, katika vizazi vyenu vyote, ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.” Kadhalika na hapa Mungu anatumia neno ‘sabato zangu’na siyo ‘sabato yangu’.
UTHIBITISHO: Walawi 19:30 Biblia inasema, “Zishikeni SABATO ZANGU, mpaheshimu patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana.” Na hapa pia tunaona Mungu anatumia neno ‘sabato zangu’ na siyo ‘sabato yangu’. Kwa hiyo, hii inatuthibitishia wazi kabisa kwamba, Mungu hakuawaagiza wana wa Israeli kushika sabato moja ya siku kama wanavyofanya wanaojiita wasabato wa leo.
Kulingana na maandiko tuliyoyasoma hapo juu, yanathibitisha kuwa wana wa Israeli walipewa sabato zaidi ya moja, na baadhi ya sabato hizo ni kama zifuatazo;
USHAHIDI WA KWANZA:
SABATO YA SIKU.
Sabato ya siku ya saba, ni pumziko ambalo lilifanywa baada ya siku sita za kazi, hivyo siku ya saba, wana wa Israeli walipewa amri ya kupumzika, kama tunavyoweza kuiona katika amri ya nne miongoni mwa amri kumi.
Uthibitisho wa Sabato hii upo katika kitabu cha Kutoka 35:2 Biblia inasema, “Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni sabato ya kustarehe kabisa kwa Bwana, mtu awaye yote atakayefanya kazi yoyote katika siku atauawa.” (Soma pia Kutoka 31:14-15; Kumbukumbu 5:14).
Hii ndio Sabato ambayo wengi wanaipigania na kusahau Sabato zingine.
USHAHIDI WA PILI:
SABATO YA MWAKA.
Sabato ya mwaka wa saba, ni pumziko ambalo lilifanywa baada ya miaka sita ya kazi, hivyo mwaka wa saba, wana wa Israeli walipewa amri ya kupumzika mwaka mzima.
Uthibitisho wa sabato hii upo katika kitabu cha Walawi 25:1-5, “Kisha Bwana akanena na Musa katika mlima wa Sinai, na kumwambia. Nena na wana wa Israeli, hapo mtakapoingia katika nchi niwapayo, ndipo hiyo nchi itashika sabato kwa ajili ya Bwana. Panda shamba lako miaka sita, na miaka sita lipalie shamba lako la mizabibu, na kuyachuma matunda yake; lakini katika mwaka wa saba itakuwa ni sabato ya kustarehe kwa ajili ya hiyo nchi, ni sabato kwa Bwana; usipande shamba lako wala usipalie shamba lako la mizabibu. Hicho kimeacho chenyewe katika mavuno yako, usikivune, wala zabibu za mizabibu isiyopelewa usizitunde, UTAKUWA MWAKA WA KUSTAREHE KABISA KWA AJILI YA NCHI HIYO. Na hiyo sabato ya nchi itakuwa chakula kwenu; kwako wewe, na kwa mtumwa wako, na kwa mjakazi wako, na kwa mtumishi aliyeajiriwa, na kwa mgeni wako akaaye pamoja nawe.”
Je, wewe unaye fuata Sabato ulisha wai pumzika kwa mwaka mzima bila ya kufanya kazi?
USHAHIDI WA TATU:
SABATO YA SABATO SABA ZA MIAKA (YUBILEE)
Sabato hii ni pumziko ambalo lilifanywa baada ya sabato saba za miaka yaani miaka saba mara saba unapata miaka 49, hivyo mwaka wa hamsini, wana wa Israeli waliamriwa kupumzika. Kwa jina lingine iliitwa Yubile.
Uthibitisho wa Sabato hii tunaweza kuiona katika kitabu cha Walawi 25:8-11, “Nawe utajihesabia sabato saba za miaka, maana, miaka saba mara saba; zitakuwa ni siku za sabato saba za miaka kwenu, maana miaka arobaini na kenda (49).Ndipo utakapoipeleka pande zote hiyo baragumu, yenye sauti kuu, siku ya kumi ya mwezi wa saba; katika siku hiyo ya upatanisho mtaipeleka baragumu katika nchi yenu yote. NA MWAKA WA HAMSINI MTAUTAKASA, na kupigwa mbiu ya kuachwa mahuru katika nchi yote kwa watu wote waiketio, itakuwa ni yubile kwenu; nanyi kila mtu atairudia milki yake mwenyewe, nanyi mtarejea kila mtu kwa jamaa yake. Mwaka huo wa hamsini utakuwa ni yubile kwenu; MSIPANDE MBEGU, WALA MSIVUNE, KITU HICHO KIMEACHO CHENYEWE, WALA MSIZITUNDE ZABIBU YA MIZABIBU ISIYOPELEWA.”
SASA TUJIULIZE MASWALI MACHACHE:
1. Kama kweli Wasabato wa leo wako sahihi kushika Sabato, kwa nini wanashika sabato ya siku peke yake?
2. Je mbona hizi nyingine zimewashinda?
3. Kama sabato inayoshikwa leo na wasabato, msingi wake ni Biblia, mbona hizi Sabato nyingine wameziacha na wakati zote ziliamriwa na Mungu mwenyewe?
Sasa tuangalie neno la Mungu linasema nini hukusu washika sheria/sabato.
Yakobo 2:10 inasema, “Maana mtu awaye yote atakaye ishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote.”
Umesoma mwenyewe kuhusu kushika sheria na tatizo la kuto shika sheria zote. Inamaanisha kuwa wamekosea juu ya sheria zote. Sasa kuna faida gani kushika sheria moja na kuvunja zote?
Tumefika mwisho wa sehemu ya Sita, na sasa tutaenda SEHEMU YA SABA
JE, UNAJUA MALENGO YA KUSHIKA SABATO KWA WANA WA ISRAELI?
**********USIKOSE SEHEMU YA SABA***********
Ni mimi Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.
© Copyright 1998-2016 Max Shimba Ministries - All Rights Reserved.

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW