Ndugu msomaji,
Hebu tuangalie mifano kadhaa hapa:
MFANO WA KWANZA
Yesu alipomponya mtu ambaye alikuwa hawezi kwa muda wa miaka 38, alimwambia ‘jitwike godoro lako, uende.’ (Yohana 58). Hii ilikuwa ni siku ya sabato.
Lakini tunaona kwamba Wayahudi walipomwona mtu huyo walimwambia, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. (Yohana 5:10). Bila shaka walisema hivi kwa kuwa walifahamu fika jinsi sabato inavyotakiwa kutunzwa.
Hii ni kusema kwamba, kwa kadiri ya kanuni za utekelezaji wa sabato, hili lilikuwa ni kosa. Sasa, swali ni kwamba, kwa nini Yesu alivunja sabato kwa kumruhusu yule mtu abebe godoro?
MFANO WA PILI
Wayahudi walipomkasirikia Yesu kwa sababu ya kumruhusu yule mtu kubeba godoro siku ya sabato, Bwana Yesu aliwajibu kwamba: Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. (Yohana 5:17). Haya ni maneno ya ajabu sana. Wewe uliye Mungu ulituambia kwamba siku ya sabato tusifanye kazi bali tupumzike; tumemwona mtu anafanya kazi ya kubeba godoro, tumekuja kwako, lakini wewe si tu kwamba hukumkemea, bali unasema tena kwamba na wewe unafanya kazi hata sasa (siku ya sabato)!
Kama sabato hasa ni kuacha kufanya kazi, iweje tena Yesu atamke jambo ambalo ni wazi kabisa linavunja sheria aliyoiweka mwenyewe ya kutofanya kazi; yaani aseme kuwa hata sasa yeye anafanya kazi?
MFANO WA TATU
Siku moja Yesu aliingia kwenye sinagogi ambamo mlikuwamo mwanamke mwenye pepo wa udhaifu. Yesu alimponya mama yule.
Hata hivyo, Biblia inasema: Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. (Luka. 13:14).
Maneno haya ya mkuu wa sinagogi yanatuonyesha kwamba, jambo alilofanya Yesu lilikuwa ni kuvunja sabato. Swali ni lilelile, kwa nini Yesu alivunja sabato?
Tunafahamu kuwa maandiko yanasema kwamba kuvunja sabato ni dhambi, tena ambayo iliadhibiwa vikali sana. Na katika mifano hiyo hapo juu, tunaona kwamba Yesu alivunja sabato kwa kufanya mambo ambayo jamii nzima ilikuwa haiyafanyi siku ya sabato. Kwa harakaharaka, mtu anaweza kusema kwamba, Yesu alitenda dhambi.
Lakini wakati huohuo, maandiko yanasema kwamba, katika kuishi kwake kote hapa duniani, Bwana Yesu hakuwahi kutenda dhambi. (Waebrania 4:15).
Swali la kujiuliza hapa ni kwamba, iweje uvunje sabato, jambo ambalo ni dhambi, halafu uhesabiwe kuwa hujatenda dhambi? Pili, iweje wewe ambaye ndiye ulisema watu wapumzike siku ya sabato, ndio uwe wa kufanya kinyume na agizo lako mwenyewe? (Maana Yesu ndiye Mungu aliyeagiza sheria ya sabato ifuatwe). Iweje hapa yeye ndiye awe wa kuivunja?