UTANGULIZI
Mwandishi mmoja alimwuliza Bwana Yesu: Katika amri zote ni ipi iliyo kuu? (Mk. 12:28).
Bwana alimjibu: Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. (Mk. 12:29-30). Hicho ndicho kipimo cha utimilifu wa utii.
Tunapoamua kumfuata Yesu, hata hivyo, hatukamiliki kwa siku moja. Maisha ya wokovu ni safari; ni mchakato wa kukua kuanzia uchanga, utu uzima, hadi utimilifu wa Kristo. (1 Pt. 2:2; Ebr. 5:12-14).
Mabadiliko ya ukuaji wetu kiroho hayafanyiki kwa juhudi zetu wenyewe – ni Roho Mtakatifu ndiye anayetubadilisha. Wajibu wetu ni kumpa nafasi ili aweze kufanya hivyo. Hiyo ni kusema kwamba, kazi ya Roho Mtakatifu ndani yetu inategemea mwenendo wetu na kiwango kile cha utayari tulio nao wa kutii neno lake; na pia bidii na shauku yetu ya kumtafuta Bwana. Yeye anasema: Nawapenda wale wanipendao na wale wanitafutao kwa bidii wataniona. (Mith. 8:17).
KABLA YA KUOKOLEWA
Kabla ya kuokolewa tunakuwa ni watu wa duniani. Mawazo, maneno, na matendo yetu yanakuwa ni ya kidunia; maana dunia ina kawaida zake ambazo ni tofauti kabisa na zile za kimbingu.
Maandiko yanasema: Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu. (1 Kor. 6:9-11).
Vilevile imeandikwa: Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo ... (Gal. 5:19-21).
Huko ndiko ambako tunakuwa kabla ya kuamua kumpokea Yesu mioyoni mwetu na kumwachia utawala wa maisha yetu. Wakati tungali kule, maandiko yanasema: Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nao tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. (Efe. 2:1-3).
BAADA YA KUOKOLEWA