Saturday, November 28, 2015

NINI NI MAPENZI YA MUNGU KWA MWANADAMU?

Mathayo 7:21 inasema “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana atakayeingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”
Naamini kabisa kama kweli wewe unahamu ya kuingia katika ufalme wa Mungu basi ni lazima utataka kujifunza yapi ni mapenzi ya Mungu kwako ili uyatende na uweze kuurithi uzima wa milele. Yesu anasema si kila mtu, sio watu, bali mtu aniambiaye Bwana, Bwana atakayeingia katika ufalme wa Baba.…………kwa lugha nyepesi maana yake wapo wengi wenye kusema Bwana Bwana lakini hawataurithi ufalme wa milele kwa sababu ya kutotenda mapenzi ya Mungu.
Hivyo basi kwa sababu si kila mtu, aniambiaye………….., maana yake kwa kila mtu chini ya jua kuna mapenzi ya Mungu ya kutekeleza, na mapenzi ya Mungu maana yake ni yale ambayo Mungu anataka watu wake wayatende . Sasa lengo au shabaha ya ujumbe huu ni kujibu swali letu kwamba nini ni mapenzi ya Mungu kwa mwanadamu na hivyo kukupa maarifa yatakayokusaidia kuyajua mapenzi ya Mungu katika maisha yako .
Baada ya kuwa nimemuomba Mungu anijulishe na kujifunza zaidi kuhusu mapenzi ya Mungu nilipata maarifa yafuatayo kuhusu mapenzi ya Mungu, Mapenzi ya Mungu unaweza kuyagawanya katika makundi makubwa mawili kama ifuatavyo;
(a) Ni mapenzi ya Mungu uongozwe na Roho Mtakatifu.
Ukisoma 1Wakorinto 12:3 Biblia inasema “kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema Yesu amelaaniwa wala hawezi mtu kusema Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu sasa ili uelewe vizuri soma kwanza mistari hii katika Isaya 46:9-10 ; “ Kumbukeni mambo ya zamani za kale, maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado nikisema , shauri langu litasimama , nami nitatenda mapenzi yangu yote” unaweza ukarudia tena kusoma hiyo mistari ndiyo tuendelee.
Mungu anasema yeye ndiye autangazaye mwisho tangia mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka. Maana yake ni hii Mungu anakujua vizuri kuliko unavyojijua. Pia tayari Mungu anayo ratiba kamili ya maisha yako tangia ulipozaliwa. Na anajua kwa nini alikuumba na anao wajibu au kusudi ambalo anataka ulitekeleze, na hii ina maana haukuzaliwa kwa bahati mbaya.
Sasa ili uweze kulitumikia kusudi/shauri la Bwana katika kizazi chako unatakiwa uongozwe na Roho Mtakatifu. Maana katika zaburi 32:8 anasema “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, nitakushauri jicho langu likikutazama’.
Mimi sijui kusudi la Mungu kwako ni nini?, ila ninachojua kwa mujibu wa Biblia kila mmoja ana wajibu wa kuutekeleza. Na Roho Mtakatifu ndiye mwezeshaji wa wewe kutekeleza huo wajibu uliopewa na Mungu chini ya jua. Ikiwa ni huduma, siasa, utawala, ofisi, biashara n.k. Anaposema nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea maana yake katika mambo ya rohoni na hata ya mwilini, Roho Mtakatifu atakuongoza kuyatenda yale ambayo ni mapenzi ya Mungu. Maana katika warumi 8:14 anasema ” kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho Mtakatifu hao ndio wana wa Mungu”.
Sasa kama hauongozwi na Roho Mtakatifu katika kulitumikia shauri / kusudi la Bwana katika maisha yako ya kiroho au kimwili maana yake unaongozwa na roho nyingine ya dunia hii ambayo nia yake ni mauti. Na mtu wa namna hii hata akitoa unabii au pepo kwa jina la Yesu atakataliwa maana anafanya hayo kwa kujikinai siyo Mungu Roho Mtakatifu anayemuongoza.
(b) Ni mapenzi ya Mungu ulitendee kazi neno lake.
, Warumi 2:13 inasema “Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki“. Tazama, haki ya kuurithi ufalme wa Mungu haiko kwa wale waliosikia au kusoma kwamba tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu kwa maana hapana mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao.Bali haki ipo kwa wale ambao siku zote wanatafuta kuwa na amani na watu wote na pia wale ambao wanaishi maisha ya utakatifu . Yakobo 1:22 inasema “Lakini iweni watendaji wa Neno wala si wasikilizaji tu, hali mkijidangaya nafsi zenu”. Neno la Mungu ni jumla ya mawazo na njia za Mungu kwa wanadamu za kuwasaidia kuishi katika mpango wa Mungu.
Limebeba mapenzi ya Mungu, hukumu, amri, mafunuo na maagizo ya Mungu kwa mwanadamu. Sasa kwa mfano imeandikwa usiue, usizini sasa si yule anayesikia kwamba usiue,au usizini ndiye anayehesabiwa haki bali ni yule asiyeua wala kuzini. Kushindwa kulitendea kazi Neno la Mungu ni kushindwa kuyatenda mapenzi yake maana hayo mapenzi yake yamebebwa kwenye neno la Mungu.
Anaposema enendeni kwa Roho, halafu wewe unaendenda kwa mwili na unajua nia ya mwili ni mauti ,Je unategemea kuurithi uzima wa milele? Kwa lugha nyingine na nyepesi maana yake ni mapenzi ya Mungu tuwe na imani yenye matendo. Ukisema nakiri na kuamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka ili niokolewe, maana yake unatakiwa kutekeleza yale ambayo Yesu anakuagiza maana Imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa Neno la Kristo.
Hebu soma habari hii. Yakobo 2:14 –26 Mstari wa 14 unasema “Ndugu zangu yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je ile imani yaweza kumwokoa? Na ule wa 24 unasema “Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa na haki kwa matendo yake, si kwa Imani peke yake”.
Kumbuka imani inafanya kazi pamoja na matendo yake, yaani kwa kushirikiana na matendo yake. Uzao wa Imani ni – kile ulichosikia (ulichoamini) + matendo yake.
Imani yeyote ile, iwe ni ya Mungu kukuagiza kufanya jambo fulani au iwe ya wewe kuiumba ina matendo yake. “Yakobo 2:22” . Ukitenda kinyume cha hayo matendo yake hautafanikiwa. Mfano:- kama Ibrahimu angemtoa sara kuwa dhabihu kwa Mungu asingehesabiwa haki na kuwa rafiki wa Mungu . Tendo la Imani ya Ibrahimu ilikuwa ni kumtoa Isaka. Ndiyo maana Mungu alimhesabia haki.
Mapenzi ya aina yeyote ile ya Mungu kwako yamebebwa katika makundi mawili niliyokutajia. Hivyo jifunze kutulia na kusikiliza uongozi wa Roho Mtakatifu na kisha pili ujifunze kutendea kazi yale ambayo Mungu amesema katika neno lake.
Mtu afanyaye hayo hakika hatakosa kuurithi uzima wa milele. Maana yeye mwenyewe amesema katika Zaburi 32:8 kwamba “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, nitakushauri jicho langu likikutazama”. Sasa akikufundisha na kukuonyesha njia Yesu maana yake anakuongoza katika njia ya uzima maana yeye alikuja ili uwe na uzima, kisha uwe nao tele Yohana 10:10.
Neema ya Bwana Yesu na iwe nawe siku zote.
Na;Patrick Samson Sanga.

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW