Saturday, February 3, 2018

YESU KRISTO ALIKUWA MASKINI ILI SISI TUWE MATAJIRI

No automatic alt text available.
“ Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake” (2 Wakorintho 8:9).
Je! unafahamu kwa nini Yesu Kristo aliamua kuwa maskini? Ni “…….. ili kwamba ninyi mpate kuwa MATAJIRI kwa umaskini wake”.
Najua kuna wengine watashangaa kuusoma mstari huu; lakini ndivyo ilivyo.
Nimewahi kusikia mkristo mmoja akisema: “ Mimi ni maskini kwa kuwa Yesu Kristo alikuwa maskini”.
Na mwingine alisema; “ Napenda kuwa maskini kwa kuwa Yesu Kristo alikuwa maskini”.
Nadhani kuwa kuna wakristo wengi ambao wana mawazo kama haya. Ni kweli kwamba Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini. Lakini hakuwa maskini ili sisi tuwe maskini; bali alikuwa maskini ili sisi tuwe matajiri! Kama alikuwa maskini ili sisi tuwe maskini kama wengine wanavyodhani, basi kazi hiyo haina faida kwetu. Lakini Yesu Kristo asifiwe kwa kuwa alikuwa maskini ili sisi tuwe MATAJIRI.
Na ndiyo maana alisema katika Luka 4:18a ya kuwa; “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri MASKINI habari njema.”
Je! kuna habari njema kwa maskini zaidi ya kumwondoa katika umaskini wake?
Injili ni habari njema. Na injili ni uweza wa Mungu uuletao wokovu kwa kila aaminiye (Warumi 1:16). Kuokoka si kuenda tu mbinguni; bali kuokoka maana yake ni uokolewe usiende motoni bali uende mbinguni ukifa, PAMOJA na kuokolewa kutoka kwenye matatizo ukiwa hapa duniani ambayo ni pamoja na umaskini.
Petro aliposema “Bwana niokoe” alipokuwa anazama katika maji unafikiri alikuwa anataka wakati huo aokoke aende mbinguni? La hasha! Yeye Petro alitaka aokoke ASIZAME KATIKA MAJI. Na Yesu akasikia kilio chake akamwokoa. Hivi leo kuna watu wengi mijini na vijijini wanalia Yesu awaokoe kutokana na njaa, kukosa mavazi, magonjwa, maonezi, nakadhalika. Kanisa kama mwili wa Kristo linatakiwa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia watu hao, kwa kuwa kazi hii ni sehemu ya utume wake.
Wakristo wengine utawasikia wakisema; hapa duniani hawahitaji kitu bali thawabu yao wataipata mbinguni. Lakini matamshi ya namna hii yanaeleza ukweli nusu na usiokamilika. Kuwa mkristo kuna thawabu duniani na kuna thawabu mbinguni.
Kama hakuna thawabu yoyote tunayoipata tukiwa hapa duniani kwa kumfuata Yesu Kristo; basi ukristo wetu hauna maana na hauna msaada wowote kwa mwanadamu. Ukristo usiotatua matatizo ya mwanadamu ya kila siku, ni ukristo usio na uhai.
Mtume Petro naye aliwahi kusumbuliwa sana na jambo hili, hata ikabidi amuulize Bwana Yesu.
“Ndipo Petro akajibu, akamwambia, tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata, TUTAPATA NINI BASI?” (Mathayo 19:27)
“Yesu akasema, Amini, nawaambiaeni, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa MARA MIA SASA WAKATI HUU, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele” (Marko 10:29,30).
Majibu haya ya Bwana Yesu, yanazidi kutudhihirishia ya kwamba si mapenzi ya Mungu tuwe maskini. Yesu Kristo ameeleza wazi kabisa ya kuwa atakayemwamini na kufuata maagizo hayo atapata MARA MIA SASA WAKATI HUU akiwa bado duniani. Na kati ya vitu atakavyopewa ni pamoja na nyumba na mashamba!
Ni kweli Bwana Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini, lakini baada ya kufufuka alirudishiwa utajiri wake. Ndiyo maana Mtume Paulo anazungumzia juu ya “….. utajiri wake Kristo usiopimika”. (Waefeso 3:8). Na katika Wafilipi 4:19 tunasoma hivi; “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu”.
Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na magonjwa yetu , na kwa kupigwa kwake sisi tumepona (Isaya 53:5; Mathayo 8:16,17; 1Petro 2:24). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na kuombea wagonjwa na kutoa huduma za afya kwa wagonjwa.
Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na akafanyika dhambi kwa ajili yetu, “ Ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye” (2Wakorintho 5:21). Na kwa kujua hili kanisa linahubiri habari za ondoleo la dhambi kwa yeyote atakayemwamini Kristo.
Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alikuwa maskini, ingawa alikuwa tajiri, ili kwa umaskini wake sisi tupate kuwa matajiri (2 Wakorintho 8:9). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili mtu aondokane na umaskini.
Shalom

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW