Sharoni hakuwa Mkristo bali alikuwa ni binti wa Kiislamu. Na wala hakuwa amewahi kujifunza habari za Yesu na Ukristo. Lakini Bwana Yesu mwenyewe alimfuata na kujidhihirisha kwake. Je, ilikuwaje, na nini kilitokea baada ya hapo? Tafadhali fuatilia ushuhuda huu wenye nguvu na unaodhihirisha upendo na uweza na uungu wa Bwana Yesu.
……………………………….
Jina langu ni Sharoni Sabina Natrajan. Kwa sehemu kubwa ya maisha yangu nilikulia Bombay. Familia yangu si Wakristo. Kwa hiyo sikuwahi kupata mafundisho yoyote ya Kikristo. Natokea kwenye familia ambayo inathamini sana elimu, na kila mtu ana elimu ya kutosha. Upande wa mama yangu, anatokea kwenye ukoo wa Zaminda. Na hata nyakati zile, wavulana na wasichana walikuwa na elimu kubwa.
Baba yangu ni injinia ambaye amesoma kwenye chuo kinachoheshimika sana, na anashikilia cheo kikubwa kwenye makampuni ya kimataifa hapo Bombay.
Sisi ni familia ndogo tu yenye mimi, dada yangu, baba na mama. Tangu nikiwa mdogo, nilikuwa ni mtu ninayependa masuala sanaa (creative arts). Nilisomea na kuhitimu katika sanaa za maonyesho na pia uchoraji. Kwa hiyo, maisha yangu yote ya utotoni yalikuwa yamejikita kwenye mambo haya.
Wazazi wangu walikuwa na upendo sana na nilipata kila nilichohitaji. Sikupungukiwa na chochote maishani mwangu.
Baba yangu alipenda sana nisomee uinjinia, licha ya kuwa wakati nikiwa sekondari ya juu nilikuwa tayari nikifanya sanaa za maonyesho kote nchini – kucheza ngoma, maigizo,n.k. Sasa, kwa kuwa alitaka niwe injinia, nilituma maombi na kupata nafasi kwenye chuo kizuri sana. Uinjinia haukuwahi kuwa jambo la moyoni mwangu, lakini nilifanya hivyo ili tu kuwafurahisha wazazi wangu. Kwa hiyo, nilienda Puna kusomea uinjinia lakini wakati huohuo nilikuwa nikifanya sanaa za maonyesho.