Na Mchungaji Josephat Gwajima 16.9.2012
Utangulizi:
Biblia imeeleza kuhusu nyota ya Yesu ilivyoonekana kutoka mashariki,(Mathayo2:1); Hii inadhihirisha wazi kuwa kila mtu ana nyota yake. Hivyo katika mfulilizo wa somo hili tutaona maana ya nyota, kazi ya nyota, nyota yaweza kufunikwa kichawi, madhara ya kuishi bila nyota, dalili za kuchukuliwa nyota, nyota yaweza kurudishwa na namna ya kutambua nyota yako. Hapa hatuzungumzii kuhusu kusoma nyota au utabiri wa nyota bali tunaangalia nyota kama ilivyo katika Biblia.
MAANA YA NYOTA:
Nyota katika Biblia inawakilisha kipawa, hatma ya mtu, lengo lililomfanya Mungu akulete hapa duniani na kusudi lako la maisha. Hivyo tunaposema nyota yako ipo au imechukuliwa maana yake hayo mambo yamechukuliwa au yapo. Kimsingi hakuna mtu asiye na maana tangu kuzaliwa kwake, kwasababu kila mtu aliye duniani amekuja kwa kusudi lake.
Kuna tofauti kati ya elimu na nyota; elimu sio nyota lakini elimu yaweza kunoa nyota. Na si kwamba kujifunza kunaleta nyota bali nyota ipo kwa wote lakini elimu inainoa nyota; na ndio maana ni rahisi kumwona mtu hana elimu lakini anamafanikio mahali fulani. Ukisoma Mhubiri 9:11 Biblia inasema wakati na bahati huwapata wote na sio swala la elimu au ujuzi tu.
KAZI YA NYOTA:
- Nyota humfanya mtu kuwa mahiri katika utendaji kazi wake. (Effectiveness)
- Nyota huleta ubunifu katika maisha ya kila siku (Creativity)
- Nyota inamfanya mtu anatenda kwa ufanisi (Efficiency)
- Nyota huleta mvuto kwa watu kutoka mbali ili kuleta vitu kwa ajili yako. (Attraction)
- Nyota humfanya mtu awe na maisha yenye mwelekeo na kibali mbele za watu. (Acceptance and Favor)
- Nyota humfanya mtu kusikilizwa katika jamii.
Kuna vitu ambavyo mtu anaweza kuvipata kwasababu nyota yake imeonekana. Nyota yaweza kuvuta zawadi yaani vile vitu ambavyo hujavitaabikia, na ndio maana Yesu alipokuwa mdogo aliletewa zawadi na mamajusi wa mashariki. (Mathayo 2:11) kwahiyo nyota ikichukuliwa maana sahihi ni kwamba hayo mambo hapo juu yote hayapo.
Mathayo 2:1-2; Wakati Yesu anazaliwa kulikuwa na watu wanaitwa mamajusi, ambao walikuwa na uwezo wa kusoma nyota. Hivyo katika ulimwengu wa roho waweza kuona watawala wajao, maisha yajayo au yale yatarajiwayo. Na ndio maana Mamajusi wa mashariki ya mbali waliweza kuifuata nyota ya Yesu.
Nyota inapoonekana inaweza kufuatwa, yaani watu waona zile kazi zake na kumfuata mtu. Kimsingi tunaposema mtu hana nyota maana yake umahiri, ufanisi na kibali vimechukuliwa. Lakini nyota ikionekana maana yake haya mambo yote yamerudishwa na hapo utamwona mtu anafanikiwa hata kama elimu yake sio kubwa.

















