Kwanza nakukaribisha katika somo hili kuhusu ngono na picha za ngono na au ponografia. Ni somo la muhimu sana, maana labda kwenye Kanisa lenu au Msikini wenu au Sinagogi lenu hamjawai fundishwa hili so. Basi ni vema leo tujifunze kwa kutumia misingi ya NENO LA MUNGU.
Kufika sasa, jambo ambalo limefanyiwa utafiti wa mara nyingi sana kwa maneno katika mitandao linahusiana na ponografia. Kutokana utafiti ulio fanywa na “google” unasema kuwa neno “sex” “ngono kwa kiswahili” linaangaliwa mara milioni 506 kila mwezi.
Maana ya ngono:
Ngono ni kitendo cha mtu au watu kufanya kitendo cha kujamiana (Tendo la Ndoa) na pia ni ile hali ya kuwa uchi wa mnyama.
Maana ya picha:
Neno picha ni kivuli cha mtu, watu, kitu n.k. Picha si kitu halisi bali ni kivuli chake. Unaweza ukapewa picha ya mtu lakini usifahamu urefu wake au ni mfupi kiasi gani lakini sura yake ukawa umeiweka katika kumbukumbu yako ya fahamu.
Ponografia imeenea sana katika ulimwengu wa leo. Ingawa zaidi ya kitu cho chote, shetani amefaulu katika kugeuza na kupotosha jinsia. Amechukua jambo ambalo ni jema na zuri (mapenzi kati ya mume na mke) na kubadilisha na tamaa, ponografia, uzinzi, ubakaji, na ushoga.
Kwa ujumla picha za ngono ni dhambi kwa kuwa kuangalia picha za ngono ni kufanya zinaa. Hata kama ninyi ni wanandoa, bado kuangalia picha za ngono ni dhambi.
UTHIBITISHO WA AYA:
Bwana Yesu anasema katika Mathayo 5:28, “lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.”
Hakuna anayeangalia picha za ngono aidha mwanaume au mwanamke alafu asiwake tamaa. Na tamaa hiyo haiwaki kwa sababu ya mwenzi unayeangalia naye, bali inawaka kwa sababu ya wale mnaotazama picha zao, nikiwa na maana kwamba chanzo cha tamaa yako hapo ni utupu wa yule mwanaume na mwanamke wanaofanya ngono na si mwenzi wako. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo, tayari ninyi wanandoa wote mnaingia kwenye mtego wa kuwa wazinzi.
Picha za ngono ni mtego wa shetani katika kukiweka kizazi cha sasa kiweze kila wakati kutafakari mambo ya ngono na sio kumtafakari Mungu. Mtu aliyeathirika na picha za ngono kwenye mitandano kamwe hawezi kuwa na mahusiano ya kweli na Mungu.
UTHIBITISHO WA AYA:
Neno la Mungu linasema katika Wafilipi 4:8, “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, YATAFAKARINI HAYO.”
Picha za ngono zinamfanya mtu awe mateka wa ngono, na ni ngumu kwa mtu aliyeathirika na picha za ngono kujinasua kwenye mtego huo. Kila wakati hujisikia nguvu fulani inamvuta kutazama picha hizo. Kila akiingia kwenye mtandao kuna kitu kinamsukuma kutazama picha hizo. Hizo ni dalili za mtu kuwa mateka na mtumwa wa ngono. Tayari mtu huyo yupo kwenye gereza la shetani la ngono.