Saturday, August 22, 2015

YESU NI UPENDO (SEHEMU YA TATU)

Yesu ni Mungu Aliye “Tayari Kukusamehe Dhambi”
Tunapofanya dhambi tunakuwa na hisia gani zenye kulemea, lakini tunaweza kunufaikaje na msamaha wa Yesu?

Tunapofanya dhambi, sisi huona aibu, hukata tamaa, na kuhisi hatia na huenda hali hiyo ikafanya tufikiri kwamba hatustahili kabisa kumtumikia Mungu. Hata hivyo, kumbuka kwamba Mungu ‘amekuwa tayari kusamehe.’ (Zaburi 86:5) Naam, Yesu anaweza kutusamehe dhambi zetu tunapotubu na kujitahidi kabisa kutozirudia. Ona jinsi Biblia inavyofafanua sehemu hiyo yenye kuvutia ya upendo wa Yehova.

Yesu Kristo anayo amri na mamlaka ya kusamehe dhambi

Kuna jambo lililowahi kutokea hadi likawashangaza watu; hebu fatilia kisa hiki. Biblia Takatifu inasema kwamba:

“Wakaja watu wakimleta mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne. Na walipokuwa hawawezi kumkaribia (Yesu) kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza. Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na baadhi ya waandishi waliokuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao, Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?

Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu? Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?

Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi – Akamwambia yule mwenye kupooza,

Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako.
Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe.” (Marko 2:3-12)

Kwa Wayahudi uponyaji haukuwa kitu kigeni kwao kwani hata manabii enzi za Agano la Kale nao walitumia nguvu za Mungu kuponya wagonjwa; lakini, jambo lililoonekana geni kwa Wayahudi ni kusikia Yesu amesema 
“...Umesamehewa dhambi zako...” (Marko 2:5) Kauli hiyo ya Yesu iliwafanya waone kwamba Yesu AMEKUFURU kwa maana mwenye mamlaka ya kusamehe dhambi ni Mungu pekee. Watu hao walidhani Yesu amekufuru kwa sababu hawakujua kuwa Yesu ni Mungu ingawa alikuwa ameuvaa mwili wa kibinadamu kama sisi.

Ukimpokea Yesu; anakusamehe dhambi zako zote. Haijalishi umetenda dhambi nyingi kiasi gani; haijalishi hali uliyonayo hivi sasa. Fahamu kwamba Yesu anakupenda. Neno la Mungu linasema kwamba:

“...asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji...” (Isaya 1:18)

Mungu huweka dhambi zetu mbali nasi kadiri gani?
Mtunga-Zaburi Daudi alitumia usemi mwingine ulio wazi zaidi kufafanua msamaha wa Mungu: “Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.” (Zaburi 103:12, italiki ni zetu.) Mashariki ni mbali kadiri gani kutoka magharibi? Katika maana fulani, sikuzote mashariki huwa mbali kabisa na magharibi; pande hizo mbili haziwezi kamwe kukutana. Msomi mmoja anasema kwamba usemi huo unamaanisha “mbali iwezekanavyo; mbali kabisa.” Maneno ya Daudi yaliyoongozwa na Roho ya Mungu yanatuambia kwamba Mungu anapotusamehe, anaweka dhambi zetu mbali kabisa nasi.

Kwa nini tunaweza kuwa na hakika kwamba Mungu hutuona kuwa safi baada ya kutusamehe dhambi zetu?
Je, umewahi kujaribu kuondoa doa katika nguo nyeupe? Huenda hukufaulu kuondoa doa hilo ingawa ulijitahidi kadiri unavyoweza. Ona jinsi Mungu anavyoeleza msamaha wake: “Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” (Isaya 1:18, italiki ni zetu.) Usemi “nyekundu sana” unaonyesha kwamba rangi hiyo ni nyangavu.* Rangi “nyekundu” ilikuwa mojawapo ya rangi zilizotiwa kwenye nguo. Hatuwezi kamwe kuondoa doa la dhambi kwa jitihada zetu. Lakini Yesu anaweza kuondoa dhambi ambazo ni nyekundu sana na kuzifanya kuwa nyeupe kama theluji au sufu isiyotiwa rangi. Kwa hiyo, Yesu anapotusamehe dhambi zetu, hatupaswi kuhisi kwamba tuna hatia ya dhambi hizo maisha yetu yote.

Ni katika maana gani Mungu hutupa dhambi zetu nyuma yake?
Hezekia alimwambia Mungu hivi katika wimbo wa shukrani wenye kugusa moyo ambao alitunga baada ya kuponywa ugonjwa wa kufisha: “Umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako.” (Isaya 38:17, italiki ni zetu.) Ni kana kwamba Mungu anachukua dhambi za mtenda-dhambi mwenye kutubu na kuzitupa nyuma Yake ambako Hawezi tena kuziona wala kuzikazia fikira. Kichapo kimoja cha kitaalamu kinasema kwamba andiko hilo linaweza kuelezwa hivi: ‘Umefanya iwe ni kana kwamba sikufanya dhambi.’ Je, hilo si jambo lenye kufariji?

Nabii Mika anaonyeshaje kwamba Mungu anapotusamehe Anafutilia mbali dhambi zetu daima dawamu?
Katika ahadi ya urudisho, nabii Mika alieleza usadikisho wake kwamba Mungu Yehova angewasamehe watu wake wenye kutubu: “Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye . . . kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? . . . Nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari.” (Mika 7:18, 19, italiki ni zetu.) Hebu fikiria maana ya maneno hayo kwa watu walioishi nyakati za Biblia. Haingewezekana kupata tena kitu kilichotupwa “katika vilindi vya bahari.” Kwa hiyo maneno ya Mika yanamaanisha kwamba Yesu anapotusamehe, anafutilia mbali dhambi zetu daima dawamu.

Yesu ni Mungu, endapo ukimpokea atakusamehe dhambi zote ulizozitenda. Yesu anakupenda sana. Hebu leo mpe Yesu maisha yako ayatawale; Yesu ataiondoa kiu hiyo ya kutenda dhambi ikufanyayo ushindwe kujizuia kuwaka tamaa mbaya za mwili wako; Yesu atakupatia ulinzi ambao utazuia pepo wachafu wasiingilie maisha yako; Yesu atakubariki na kufungua tumbo lako lililokosa mtoto kwa muda mrefu wote huo unaotaabika hata sasa; Yesu atawarejesha kwako watoto wako ambao wamekataa kukutii hata wametoweka kwako; Yesu atakupatia uzima na kuyaondoa magonjwa yote hayo yanayokutesa hata sasa; Yesu atakubariki na kukupatia uzima wa milele.

Kwa kweli nashindwa kuuelezea kwa ufasaha zaidi upendo wa Yesu juu yako kwa maana wewe ni wathamani kubwa sana mbele za Mungu. Mimi nachoweza kukwambia ni kwamba: Yesu anakupenda tena hataki upotee. Mpe Yesu maisha yako sasa ili ufurahie uzuri wa pendo Lake.

Damu ya Yesu inamamlaka ya kusafisha dhambi zako zote.

Mpokee Yesu sasa na upate msamaha wa dhambi.

Yesu anakupenda.

Max Shimba

Max Shimba Ministries @2015.

No comments:

WHY CHRISTIANITY IS BETTER THAN ISLAM?

Has Islam Improved to Become Better Than Christianity? Does Muhammad fulfill and complete the mission and purpose of Christ? Muhammad emphat...

TRENDING NOW