Saturday, March 12, 2016

DINI NA MADHEHEBU NI MZIGO USIO WA LAZIMA


MAANA YA DINI
Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford: 2004) inaeleza neno ‘dini’ kama mfumo fulani wa imani inayohusiana na mambo ya kiroho na njia ya kuabudu, kusali au kuheshimu/kutii Muumba.

Kwa hiyo tunaweza kusema kwa kifupi kwamba, dini ni utaratibu anaotumia mwanadamu katika kumwabudu Mungu.

Zipo dini mbalimbali duniani. Japokuwa zote zinaweza kusema zinamwabudu Mungu aliyeumba vitu vyote, lakini kile kinachozitofautisha ni “utaratibu” zinazotumia katika huko kumwabudu Mungu – ndiyo sababu zikawa ni dini au madhehebu mbalimbali.

Utaratibu maana yake ni kanuni mahususi zinazotakiwa kufuatwa katika kufanya jambo fulani. Mathalani, unapotaka kujiunga na chuo, utatakiwa kulipa gharama za usajili, kujaza fomu, kufanya hivyo katika muda maalum, kuwasilisha maombi yako kwenye ofisi maalum, nk. Hali kadhalika kwa upande wa dini, ili muumini ahesabike kuwa ametekeleza ibada kwa Mungu, upo utaratibu au kanuni mbalimbali zinazotakiwa kufuatwa. Kanuni hizo ni pamoja na:
Kusema sala maalum;
Kusema sala mara idadi maalum;
Kusimama au kukaa kwa wakati maalum;
Kuvaa mavazi maalum;
Kutazama welekeo maalum; n.k.

YESU ALIANZISHA DINI GANI?
Ukisoma Biblia kwa makini, utagundua kwamba Yesu Kristo hakuanzisha Ukristo kama dini au madhehebu. Wakati Bwana Yesu alipokuja, kulikuwa na dini ya Kiyahudi (Judaism). Hii ni dini ambayo ilikuwa na utaratibu wake wa kumwabudu Mungu kama ilivyo kawaida ya dini yoyote kuwa na utaratibu.

Lakini ni wazi kwamba, Bwana Yesu hakukubalika kabisa ndani ya dini hii. Walikuwa ni wakuu wa dini hiyohiyo ndio waliomshitaki Bwana na kuwachochoea watu wa kawaida waanze kupiga kelele za kusema: asulubiwe, asulubiwe! Kati ya mashtaka yao, walisema: Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono. (Mk. 14:58).

Lakini ni kwa nini walikuwa hawamtaki? Ni kwa sababu alikuwa anaonekana anavunja utaratibu wa dini. Pia ni kwa sababu alionekana kujizolea umaarufu mwingi kuliko wakuu wa dini. Kwa hiyo, waliona kwamba nafasi zao ziko hatarini. Kwa hiyo, walimchukia na kumtungia hila nyingi ili waweze kupata sababu ya kumwua.

Tunaona jambo hilohilo hata baadaye katika huduma ya mtume Paulo. Kabla ya kuokoka, Paulo alikuwa ni mshika dini ya Kiyahudi. Yeye mwenyewe anasema kwamba: Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. (Gal. 1:14).

Lakini pale alipoitwa na Bwana Yesu kwenye huduma, mambo yaligeuka kabisa. Wayahudi walitafuta kumwua Paulo kwa sababu waliona kwamba tayari yuko kinyume na dini yao. Mathalani, Paulo alipokuwa ameshikiliwa na utawala wa Kirumi, mjomba wa Paulo alienda kumwambia jemadari wa Kirumi kwamba: ...Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paulo chini kesho, ukamweke mbele ya baraza, kana kwamba wanataka kupata habari zake kwa usahihi zaidi. Basi wewe usikubali; kwa maana watu zaidi ya arobaini wanamwotea, wamejifunga kwa kiapo wasile wala wasinywe hata watakapomwua; nao sasa wako tayari wakitazamia ahadi kwako. (Mdo. 23:20-21).

Na ndiyo maana baadaye Paulo anasema: Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumwa wa Kristo. (Gal. 1:10).

Hapa Paulo anamaanisha kwamba, kabla ya kumjua Kristo alikuwa ni mshika dini tu ambapo wakati huo uhusiano wake na washika dini ulikuwa wa amani kabisa. Lakini baada ya kuachana na dini, ndio maana wakamchukia. Na anasema sasa, kama angekuwa bado anawapendeza wanadamu wale washika dini, basi asingekuwa anateseka hivyo kwa ajili ya Kristo.

Mtume Paulo anaonyesha kwamba kutoka kwenye dini kwa ajili ya Kristo kuna neema kubwa. Anasema: Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri mataifa habari zake. (Gal. 1:15-16).

Kumbe Mungu anaita dini kuwa ni mapokeo ya mababa (Gal. 1:14). Na kumbe, alipomwita Paulo katika huduma, hakutaka Paulo abakie tena humo ndani ya dini. Na kwa kuwa sasa Paulo alitoka nje ya dini, alijikuta akizalisha maadui wengi sana.

Watu waliokuwa wakimpinga Bwana Yesu na wale waliompinga Paulo hawakuwa wakitetea maslahi ya kisiasa, bali walikuwa wakitetea dini yao.



Hata hivyo, sote tunafahamu kwamba Mungu alikuwa anawaridhia kikamilifu Bwana Yesu na Paulo. Swali la muhimu la kujiuliza ni kwamba, ndani ya dini kuna nini ambacho hakimpendezi Mungu; na nje ya dini kuna nini ambacho ndicho anaonekana kutaka sisi tukiendee?

JE, WATAKATIFU WOTE WALIKUWA NA DINI KAMA ZETU?
Ni muhimu kukumbuka kwamba, wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiendesha huduma yake hapa duniani, hakukuwako na Ukristo kama dini. Maana maandiko yanasema: Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia. (Mdo. 11:26).

Sasa swali ni kwamba kama Yesu na mitume wake hawakukubalika katika dini ya Kiyahudi na wakati huohuo Ukristo kama dini haukuwapo, je, Yesu pamoja na mitume wake waliokufa kabla ya kuanza kwa Ukristo kama dini walikuwa watu wa dini gani? Maana wangekuwa ni wa dini ya Kiyahudi kama Wayahudi wengine, wasingechukiwa wala kuuawa. Lakini hapohapo hawakuwa na dini ya Kikristo, maana dini hiyo haikuwapo!

Swali jingine ni kwamba, mababa wa zamani kabla ya Musa, yaani akina Ibrahimu, Isaka na Yakobo, ambao leo wako mbinguni, walikuwa wa dini gani; maana dini ya Kiyahudi ilianza na Musa pale kwenye mlima wa Sinai? Je, watakatifu hao walienda mbinguni kwa tiketi gani?

NINI KINACHOTAKIWA?
Ni jambo gani ambalo Mungu anataka tufahamu kuhusiana na dini na madhehebu? Je, vitu hivyo vina nafasi gani katika uhusiano wetu na Mungu?

Jibu ni kwamba, Bwana Yesu hakuja kuleta dini. Mbele za Mungu dini ni aina ya maisha ndani ya mtu yaliyotawaliwa na utii wa sheria za Mungu; na sio kuitwa mshirika wa madhehebu fulani. Maandiko yanasema: Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa. (Yak. 1:27).

Je, ni lazima uwe mshirika wa madhehebu fulani ili ufanye mambo haya? Bila shaka jibu ni hapana! Kinachotakiwa ni kuwa tu na Neno la Kristo moyoni, kisha unalitii. Dini kwa maana ya madhehebu zilianzishwa na wanadamu.Lakini mbele za Mungu, dini ni aina ya maisha yanayompendeza Mungu na si kuwa mshirika wa kundi lenye jina na taratibu fulani.

Yesu anaita kwa nguvu akisema: Njoni kwangu ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. (Mt. 11.28). kwa nini anasema hivyo? Anasema: Mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. (Yoh. 10:10).

Tunatakiwa kukimbilia kwa Bwana Yesu mwenyewe; si kwenye dini. Je, hakuna watu wa dini wanaoingia motoni? Jibu ni kwamba wapo. Kwa nini waende motoni na huku wana dini? Ni kwa sababu unaweza kuwa na dini lakini ukawa huna Yesu. Na hiki ndicho kinachotokea kwa watu wengi. Wengi wameridhika na kuwa na dini wasijue kwamba hilo si hasa kusudi la kuishi kwetu hapa duniani.

Lakini hakuna mtu aliye na Yesu ambaye anakwenda motoni! Bwana mwenyewe anaahidi wazi kabisa: Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. (Yoh. 10:27). Haleluya!

Dini ni mzigo juu ya mabega ya watu. Ni taratibu zilizoanzishwa na wanadamu na kuendelea kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Mojawapo ya washika dini wazuri sana walikuwa ni mafarisayo. Kwa mfano, walikuwa wakishika kwa uaminifu sana utaratibu wa kutokula bila kunawa mikono. Kwa hiyo, siku moja walimkabili Bwana Yesu na kumwambia: Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula. (Mt. 15:1).

Kumbuka kwamba hapa hawaongei juu ya kanuni za afya bora, la hasha! Wanaongelea utaratibu wa kidini. Bwana akasema: Mbona ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu? (Mt. 15:3). Unsona? Haya mapokeo ni yao; si ya kutoka kwa Mungu! Ukiendelea kusoma, utaona kwamba hatimaye Bwana anawaambia hawa washika dini: Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, Watu hawa huniheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu. (Mt. 15:7-9).

Kumbe tunaweza tukawa tunaenda kwenye nyumba za ibada, lakini tukawa tunafundishwa maagizo ya wanadamu!! Na kwa kuyafuata hayo tunaweza kuwa tunamwabudu Mungu bure! Inatisha kama nini! Ukisikia kazi ya hasara, basi ni pamoja na hii!

Rafiki, kwenye dini kumejaa maagizo ya wanadamu. Tena msisitizo mwingi umo kwenye hayo maagizo badala ya kuwa kwenye maagizo ya Mungu.

YESU KRISTO NDIO ANATAKIWA AWE NAMBA MOJA KWENYE MAISHA YAKO
Yesu Kristo ndiye anayetakiwa kuwa namba moja katika maisha yetu kabla ya vitu vyote. Kama dini hainiwezeshi kufikia lengo hilo, basi kuna haja gani ya kushikilia taratibu ambazo hazinisaidii; ambazo mwisho wa siku nitaingia upotevuni?

Kumbuka siku zote kwamba, wito wa Bwana Yesu ni: Njoni kwangu ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. (Mt. 11.28). Sio nendeni kwenye dini!

Utajuaje kwamba dini haikusaidii? Angalia matunda maishani mwako. Unazaa matunda gani katika maisha yako.

Imeandikwa: Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. (Mt. 7:16-18).

Matunda mabaya ni yapi? Imeandikwa: Kwa maana, ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi. (Mt. 7:20-23).

Pia imeandikwa: Basi matendo ya mwilini dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo ... (Gal. 5:19-21).

Jichunguze maisha yako na kujipima wewe binafsi. Je, dini uliyonayo imeweza kukutoa katika mambo hayo? Kama sivyo, utaponaje? Kama sivyo, mwisho wake ni nini?

HITIMISHO

Kila mwanadamu anamhitaji Yesu Kristo maishani mwake. Yeye anakupatia Roho wake Mtakatifu. Na Roho Mtakatifu anapokuja ndani ya maisha ya mtu, maandiko yanasema: Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi, ... (Gal. 5:22).

Ukiwa na Yesu maishani mwako kibinafsi, ndipo dini yako itakuwa na maana. Bila Yesu, dini ni mzigo usio na maana wala msaada wowote kwake yeye aliye nayo. Unakuwa unafanya kazi tu ya kutekeleza maagizo ya wanadamu; na mwisho wa yote ni kuingia upotevuni. Dini haiwezi kubadili maisha yako na kukufikisha kwenye utakatifu anaotaka Mungu. Maana imeandikwa: Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao. (Ebr. 12:14).

Kwa lugha rahisi, utakatifu ni kitokuwa na dhambi. Dini haiwezi kukupa huo utakatifu. Kilichozaliwa na mwili ni mwili na kilichozaliwa na Roho ni roho. (Yoh. 3:6). Mpokee Yesu kama Bwana na Mwokozi wako ili uzaliwe katika Roho. Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. (Yoh. 3:3). Kwa lugha ya iliyozoeleka, kuzaliwa mara ya pili ni kuokoka. Pokea wokovu wa Kristo leo. Ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. (Rum. 10:9).

Labda unasema, “Si imeandikwa ‘utaokoka’, yaani baadaye?” Maandiko yanasema: ... wakati uliokubalika nalikusikia, siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa. (2 Kor. 6:2).

Amka leo. Njoo kwa Yesu upokee wokovu. Hatujaitwa kutumikia dini; tumeitwa kumtumikia Bwana Yesu!

By permission: Ijili ya Kweli, King James Version Bible,

Mungu awabarikisana,

Ni mimi Max Shimba, mtumwa wa Yesu Kristo,

For Max Shimba Ministries Org,

MAX SHIMBA MINISTRIES ORG ©2016. ALL RIGHTS RESERVED
Everyone is permitted to copy and distribute verbatim copies of this license document, but changing it is not allowed.
March 12, 2016

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW