Wednesday, October 26, 2016

NENO LA MUNGU LINASEMA NINI KUHUSU SABATO? (SEHEMU YA SABA)


Msomaji wangu,

Tumesha zisoma aina tatu za Sabato katika Sehemu Ya Sita, sasa, tuangalie malengo ya Sabato.
Wanao jiita Wasabato wa karne hii, hawafamu lengo la kushika sabato kwa wana wa Israeli. Kwa kifupi, lengo la kushika Sabato kwa Wana wa Israeli lilikuwa ni kupumzika kazi na kustarehe tu na wala si vinginevyo.
Kitu cha kushanganza, wanaojiita Wasabato katika karne ya leo, wameigeuza sheria aliyo pewa Musa na wana Waisraeli ya kushika sabato kama ni siku ambayo Mungu ameamuru wafanye ibada, kinyume kabisa na kusudi zima na maana halisi ya neno sabato. Watu hawa wamekuwa na tabia ya kuwashutumu wakristo wengine na kusema kuwa, Jumamosi ndiyo siku halali ya kufanya ibada, lakini Jumapili, ni siku ambayo haikuamriwa na Mungu, watu kukusanyika kufanya ibada. Zaidi ya hapo, wanasema kuwa eti Jumapili ni siku ya kipagani. Wasabato hawa wanaihusisha siku ya Jumapili na waabudu JUA, kwa kufanya tafsiri ya neno la Kiingereza ‘Sunday’ – WANALIGAWA NENO “SUNDAY” KWA KUTENGANISHA SUN AND DAY, SUN = JUA NA DAY = SIKU Na kuja na jibu kuwa wale wote wanao abudu Jumapili basi wao wanamwabudu Mungu JUA, ingawa tuna uthibitisho tosha kuwa Wakristo wa kwanza walimwabudu Yesu ambaye alikufa kwa ajili ya dhambi zetu na SIO MUNGU JUA kama wanavyo dai. Ili kufahamu kwanini kuna siku hizi za wiki na maana yake, ni vyema kuangalia msingi wa hizi siku na jinsi walivyo ziweka. MFANO: Tuiangalie siku ya JUMAMOSI ambayo kwa Kiingereza ni SATURDAY, je, hili jina walilipataje? Kutokana na Warumi siku hii ya SATURDAY iliitwa kutokana na SAYARI YA ZOHALI yaani (dies Saturni) kwa sababu Warumi wa wakati huo waliheshimu sayari Zohali. SASA KAMA TUKITUMIA UTAALAMU HUO HUO WA KUHUSISHA SIKU NA IMANI AU DINI, JE, INAMAANISHA KUWA WASABATO “SDA” WAO WANAAMINI NA AU ABUDU SAYARI YA ZOHALI?
Kitu ambacho hawa Wasabato hawakifahamu ni hiki: Agizo la kushika sabato na siku ya kukusanyika ni vitu viwili tofauti na ni maagizo mawili tofauti ambayo wana wa Israeli walipewa kuyatekeleza.
AGIZO LA KUKUSANYIKA KUFANYA IBADA:
Katika agizo la kukusanyika kwa wana wa Israeli, Mungu alitoa siku mbili yaani Jumapili na Jumamosi, ingawa wasabato karibu wote hawalijui jambo hili, maana hao wamekaririshwa siku ya sabato tu yaani Jumamosi.

UTHIBITISHO:
Tunaweza kuthibitisha ukweli huu katika kitabu cha Kutoka 12:16 Biblia inasema, “SIKU YA KWANZA kutakuwa kwenu na kusanyiko takatifu, na SIKU YA SABA kutakuwa na kusanyiko takatifu, haitafanywa kazi yoyote katika SIKU HIZO, isipokuwa kwa hiyo ambayo kila mtu hana budi kula, hiyo tu ifanyike kwenu.”

Mungu aliwaamuru wana wa Israeli wakusanyike siku ya kwanza ya juma yaani Jumapili na siku ya saba yaani Jumamosi kwa kalenda ya kwetu. Pia Mungu hakuwaagiza kukusanyika tu, bali aliwaagiza wasifanye kazi pia. Lakini wanaojiita wasabato nyakati za leo, wanapinga kukusanyika Jumapili sawasawa na maagizo ya torati wanayodai kuifuata.
1. Swali ni kwamba, mafundisho yao ya kukusanyika siku ya sabato yametoka wapi?
2. Kama ni kwenye Biblia mbona siku moja hii wameiacha?
3. Je aliyetoa agizo la siku ya sabato ni Mungu mwingine na aliyetoa agizo katika kitabu cha Kutoka 12:16 (yaani kukusanyka siku ya Jumapili) ni Mungu mwingine?

Mtume Paulo anafundisha kuwa ni jambo la udanganyifu kuwafundisha watu washike siku ya Sabato. Kwa sababu ya wokovu wetu ndani ya Kristo (Wakolosai 2:11-15) Paulo anasema, “Basi, MTU ASIWAHUKUMU ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” (mstari wa 16).
Kwa hiyo agizo la kukusanyika lilikuwa ni siku mbili, imetajwa ya kwanza ni Jumapili (siku ya kwanza ya juma) na ya pili ni Jumamosi (siku ya saba) kwa kalenda yetu, kama tulivyoona katika kitabu cha Kutoka 12:16. Sasa tukija kwenye agizo la kushika sabato halikuwa ni siku ya kukusanayika, bali ni pumziko la kazi tu na kustarehe kama tunavyoweza kuona katika kitabu cha Kutoka 31:14-15, “Basi mtaishika hiyo sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake. Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa Bwana, kila mtu atakayefanya kazi yoyote katika siku ya sabato, hakika yake atauawa.”
Mungu hapa anasema kila mtu atakayefanya kazi siku hiyo atauawa, hajasema kila mtu atakaye kosa kwenda kwenye kusanyiko atauawa. Na ndiyo maana kwenye Biblia, inapotaja neno sabato ina maana ya kupumzika kazi na siyo kufanya kusanyiko la kuabudu kama wafanyavyo wanaojiita wasabato wa leo.
Pia Kutoka 35:2 Biblia inasema, “Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni sabato ya kustarehe kabisa kwa Bwana; mtu awaye yote atakayefanya kazi yoyote katika siku hiyo atauawa.”
Tunaona tena hapa, Mungu anasisitiza kwamba, atakayeuawa, ni yule atakayefanya kazi siku ya sabato, na hakusema atakayekosa kwenda kukusanyika kwa ajili ya ibada, kwani agizo hili lilihusiana na kupumzika kufanya tu. Kimsingi unaposema sabato, siyo dhehebu, wala siyo siku ya kuabudu, bali ni pumziko la kazi. Nyakati za leo, wanaojiita wasabato, wanachanganya siku ya kusanyiko na siku ya pumziko la kazi.
Paulo alihuzunishwa sana, kwa sababu anasema wazi hivi “…..sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini KUYAREJEA TENA MAFUNDISHO YA KWANZA yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? MNASHIKA SIKU, na miezi, na nyakati, na miaka.”(Wagalatia 4:9,10).
“Maana yale YASIYOWEZEKANA kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa DHAIFU kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma “YESU KRISTO” Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ILI HAKI YA TORATI YATIMIZWE NDANI YETU sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.” (Warumi 8:3,4).
Kwa hiyo, mtume Paulo anasisitiza, “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO.”
Tukiangalia tena maandiko katika kitabu cha Kumbukumbu la torati 5:14 kwenye ile amri ya nne ya kushika sabato, Biblia inasema, “Lakini siku ya saba ni sabato ya Bwana, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng’ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe.”
Kadhalika na hapa Mungu anaifafanua kwa uzuri kabisa, maana ya sabato na lengo lake. Lengo lilikuwa watu wapumzike, wanyama wapumzike, wafanyakazi wapumzike na kustarehe, kwa sababu hiyo, sabato iliwagusa mpaka wanyama. Kama ingekuwa kwamba sabato ilimaanisha siku ya kuabudu basi wanyama wasingetajwa kupumzika.
Mtu aliyepigwa mawe hata kufa nyakati za Musa jangwani, hakuuawa kwa sababu hakwenda kuabudu siku ya sabato, bali aliuawa kwa sababu alifanya kazi (Hesabu 15:32-36). Hii inathibitisha kwamba agizo la kushika sabato lililenga pumziko la kazi tu na si agizo la kukusanyika kama wanavyodai wasabato wa leo. Wana wa Israeli walikusanyika siku ya saba (Jumamosi) na siku ya kwanza ya juma (Jumapili) kwa agizo la Mungu mwenyewe katika Kutoka 12:16, kama tulivyokwisha kuona hapo nyuma. Kimsingi ni kwamba, katika amri kumi (Kumbukumbu 5:12-15), amri ya nne inazungumzia kupumzika kazi tu. NaKutoka 12:16 Mungu anatoa mwongozo wa siku za kukusanyika kwa ibada. Swali ni kwamba, wasabato wa leo wanakusanyika Jumamosi kwa msingi wa andiko lipi kati ya hayo? Kama kwa msingi wa amri ya nne ya kushika sabato (Kumbukumbu 5:12-15), basi watakuwa wamepotea, maana pale haikuzungumziwa siku ya kukusanyika kwa ajili ya ibada, bali ni pumziko la kazi tu. Lakini kama wana kusanyika Jumamosi, kwa msingi wa andiko la Kutoka 12:16, kadhalika watakuwa wamepotea, maana, katika siku za kukusanyika, katika andiko hili, Mungu ametoa siku mbili yaani siku ya kwanza ya juma (Jumapili) na siku ya saba ya juma (Jumamosi), sasa mbona siku ya kwanza ya Juma (Jumapili) wanaipinga? Ni wazi kabisa wanampinga Mungu.
ANGALIZO: 
Ili kupata pumziko vizuri siku ya sabato, wana wa Israeli waliagizwa na Mungu, wasitoke mahali pao; Kutoka 16:29 Biblia inasema, “Angalieni, kwa kuwa BWANA amewapa ninyi hiyo sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba. Basi hao watu wakapumzika siku ya saba.” Kwa hiyo, nyakati zile, ilikuwa ni sheria kwa wana wa Israeli, kutotembea mwendo mrefu siku ya sabato. Walitembea mahali pafupi sana, na hatimaye urefu ule wakauita mwendo wa sabato (Matendo 1:12). Wanaojiita wasabato wa leo, siku ya Jumamosi, wanatembea mwendo zaidi ya kilometa moja, kwenda kanisani, je hii ni kweli sabato ya kweli (pumziko la kweli)?
Ndugu msomaji ambaye wewe ni Msabato, umesha jiuliza swali hili? Kwanini mnachagua kutunza siku tu na mengine ya Sheria za Musa hamyafuati? Watunza Sheria wakati wa mtume Paulo waliotetea sheria na waliojitahidi sana kwa ajili ya torati ya Musa, walitoa hukumu kubwa sana kwa Wakristo walio fuata mafunzo ya Yesu. Wasabato wa wakati huo/MAFARISAYO walimshitaki mtume Paulo kwa kufundisha kinyume na sheria za Musa, eti, wanadai kuwa Mtume Paulo alifundisha uongo na au alifundisha kuvunja sheria za Musa. Je, haya madai ni kweli?

Tumefika mwisho wa Sehemu ya Saba, na sasa tutaenda SEHEMU YA NANE.
JE, UNAZIFAHAMU SABABU ZILIZOMFANYA BWANA YESU KUINGIA HEKALUNI SIKU YA SABATO?
**********USIKOSE SEHEMU YA NANE***********
Ni mimi Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo.
© Copyright 1998-2016 Max Shimba Ministries - All Rights Reserved.

No comments:

JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD "

 JESUS DECLARES THAT "HE IS THE LORD JEHOVAH GOD " Author: Dr. Maxwell Shimba  Jesus Declares, “I am the Alap and the Tau” – Under...

TRENDING NOW