Sunday, October 16, 2016

KUSHEREKEA MAULID YA MTUME MUHAMMAD NI UPAGANI NA HAIKUTAJWA KWENYE QURAN


Natanguliza maswali kwa waislam:
(a)Aya gani ya quran inawaagiza kufanya sikukuu au sherehe ya Maulid ya Mtume?
(b)Waislam nini/nani mnafuata, Allah au Muhammad au Quran au Sahihi Hadith au Nguzo au Sharia?
UTANGULIZI
Upagani wa maulid unadhihirika kwa kuangalia maeneo makubwa matatu:
(a) Historia ya Maulid.
(b) Kutokuwepo kwa uhakika wa tarehe aliyozaliwa mtume Muhammad kutoka kwenye quran au hadithi
(c) Ushahidi wa wanazuoni juu ya upagani wa maulid.
(a) HISTORIA YA MAULID
Historia hii inatuonesha vitu vitatu vya msingi:
(i) Si Muhammad wala maswahaba walisherekea Maulid
(ii) Maulid ilianza miaka zaidi ya mia tatu baada ya mtume.
(iii) Waanzilishi wa Maulid wana nasibishwa na kizazi cha wakanaji Mungu (Wapagani na makafiri).
Yeyote mwenye kutazama maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na historia ya Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum), Taabi‘iyna na waliowafuata kwa wema mpaka kufikia zaidi ya mwaka wa 350 Hijri hatumuoni hata mwanachuoni mmoja wala mahakimu (viongozi) na wala watu wa kawaida waliokuwa wakifanya mawlid au wakaamrisha au wakahimiza au wakazungumza juu yake. Amesema al-Haafidh as-Sakhawiy: “Shughuli za kufanya Mawlid matukufu hayakupokelewa na watangu wema (Salafus Swaalih) wa karne tatu bora za mwanzo. Kwa hakika jambo hili lilizuliwa baada yake” (Imenukuliwa kutoka kwa Subulul Hudaa war Rashaad cha As-Salihiy, Mj. 1, uk. 439).
Suala la sisi kujiuliza ni kuwa; Je, haya Mawlid yalianza lini? Jawabu ya suala hili kwa mwanachuoni wa Ki-Sunnah, Al-Imaam al-Maqriiziyni:

“Katika kipindi cha uongozi wa Faatwimiyyuun (hawa walikuwa ni Rawaafidh (Mashia) katika kipote cha Ismailiyyah [Makoja] katika nchi ya Misri) walikuwa wanachukuwa hii ni misimu ya sherehe ambapo walikuwa wakiwakunjulia hali za raia zao na kuwakithirishia neema. Na walikuwa hawa watawala wa Faatwimiyyuun katika mwaka mzima wana misimu ya sherehe na Idi zao nazo ni kama zifuatazo: Msimu wa kichwa cha mwaka, Msimu wa mwanzo wa mwaka, Sherehe za ‘Aashuraa, na Mawlid ya Nabii (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Mawlid ya ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu), na Mawlid ya Hasan na Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhuma), na Mawlid ya Faatwimah az-Zahraa (Radhiya Allaahu ‘anha), na Mawlid ya kiongozi wao aliye hai kwa wakati ule, usiku wa kwanza wa Rajab, na usiku wa kati ya Rajab, na Mawlid ya usiku wa Ramadhaan na mwisho wa Ramadhaan na Msimu wa ‘Iydul Fitwr na Msimu wa ‘Iydul Adh-ha na Idi ya Ghaadir, Msimu wa ufunguzi wa Ghuba na Siku ya Nairuuz na Siku ya Ghatas na Siku ya Mazazi, na Siku ya Vipandio, Kis-wa (nguo) ya Msimu wa Kusi na Kaskazi, Alhamisi ya Adasi na Siku ya Ubatizo” (Al-Khutwat, Mj. 1, uk. 490 na baada yake). na amesema tena katika kitabu chengine: “Na katika mwezi wa Rabi’ul Awwal walijilazimisha watu kuwasha kandili usiku katika njia zote na vichochoro vyake huko Misri”.
Na amesema tena al-Maqriiziy katika maudhui nyengine: “Shughuli za Mawlid ya Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilikuwa zikifanyika rasmi kama desturi yake katika mwezi wa Rabi’ul Awwal”. Kila mmoja anatakiwa azingatie jinsi gani Mawlid yalivyoanzishwa pamoja na uzushi mkubwa mfano: Uzushi wa kukataa na kuchupa mipaka juu ya familia ya Mtume kwa kusimamisha mawlid ya ‘Aliy, Faatwimah, Hasan na Husayn.
Watu wa kwanza kuzua kile kinachoitwa Mawlid ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Bani ‘Ubayd ambao walikuwa wakijulikana kama Faatwimiyyuun. Haya yametajwa na wanazuoni wengi mfano Mufti wa Misri wa zamani, Shaykh Muhammad Bakhiit al-Mutii‘y katika kitabu chake Ahsanul Kalaam Fi maa Yata‘alaq Bis Sunnah wal Bid‘ah Minal Ahkaam; Shaykh ‘Ali Mahfuudh katika kitabu chake Al-Ibda‘ Fii Madh-har al-Ibtidaa‘; Shaykh Isma‘iyl al-Answaariy katika kitabu chake Al-Qawlul Fasl Fiy Hukmil Ihtifaal Bi Mawlid Khayrir Rasuul.
“Wa mwanzo walioyazua Mawlid huko Cairo ni watawala wa Kifaatwimiyyah (Mashia) katika karne ya nne. Walizua Mawlid aina sita: Mawlid ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Mawlid ya Imam ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu), Mawlid ya Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha), Mawlid ya Hasan (Radhiya Allaahu ‘anhu), Mawlid ya Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) na Mawlid ya Khalifa aliyekuwepo” (‘Ali Mahfuudh katika kitabu chake al-Ibda‘ Fii Madh-har al-Ibtidaa‘, uk. 251).
Je, wanazuoni wamesema nini kuhusu hii Dola ya Faatwimiyyuun ‘Ubaydiyyah ambayo imeanzisha jambo hili (Mawlid ya Mtume)? Amesema Imaam Shaamah, mwana-historia na Muhaddith (aliyeboboea katika mas-ala ya Hadithi za Mtume [Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam]), mwandishi wa kitabu ar-Rawdhatayn Fiy Akhbaar Dawlatayn, uk. 200 – 202 kuhusu Faatwimiyyuun ‘Ubaydiyyah: “Wao walijidhihirisha kwa watu kuwa wao ni masharifu (watukufu) kutoka kwa Faatwimah hivyo wakamiliki na kutawala ardhi na kuwatendesha nguvu waja. Na wametaja kipote cha wanazuoni wakubwa kuwa wao hawakustahiki hilo na nasaba yao si sahihi bali walikuwa wanajulikana zaidi kwa banu ‘Ubayd. Na baba wa ‘Ubayd alikuwa ni katika kizazi cha wakanaji Mungu na Mmajusi na inasemekana kuwa babake alikuwa Myahudi mfua vyuma kutoka Shaam. Jina la huyu ‘Ubayd lilikuwa ni Sa‘iyd, lakini alipofika Morocco alijiita ‘Ubaydullah na akajidai kuwa yeye ni katika ukoo wa ‘Alawi Faatwimiy na madai yake ya nasaba hiyo siyo sahihi. Yeye hakutajwa na yeyote miongoni mwa wajuzi wa nasaba za ‘Alawi, kipote kikubwa cha wanavyuoni wametaja kinyume cha hayo. Alijinasibisha na Bani Mahdiyyah wa Morocco, naye alikuwa Zindiyq muovu, adui wa Uislamu na alijidhihirisha Ushia wake. Alikuwa na hima ya kuiondoa mila ya Kiislamu pamoja na kuwaua mafaqihi wengi pamoja na wanavyuoni wa Hadiyth. Kusudio lake kubwa lilikuwa kuwaondosha kabisa ili dunia ibaki na wanyama pekee na hivyo kumakinika katika kuleta uharibifu katika itikadi zao na kuwapoteza lakini Allaah Anaitimiza nuru Yake japokuwa watachukia makafiri”.
Kizazi chake kiliinukia katika hilo huku wakijitokeza wakati kukiwa na fursa na isipokuwa hivyo walikuwa wakijificha na kufanya vituko vyao kwa siri. Walinganizi wake walitumwa katika nchi yote huku wakiwapoteza wale wanaoweza miongoni mwa waja. Balaa hii ilibakia kwa Uislamu kuanzia mwanzo wa Dola yao mpaka mwisho wake yaani Dhul-Hijjah 299 hadi 567 Hijri.
Katika siku zao za utawala hawa Rawaafidh (Mashia) waliongezeka sana na hivyo wakawa wanahukumu watu kwa kuwawekea vikwazo na wakaweza kuharibu itikadi za mapote ya watu waliokuwa wakiishi katika majabali na mapango ya Shaam kama Nusayriyyah, Druze na Hashashiyyun (Assassins), wote wakiwa aina moja na wao wenyewe. Waliweza kuwatumia kwa sababu ya udhaifu wa akili zao na ujinga wao, hivyo kuwapatia fursa Wazungu (Crusaders – watu wa msalaba) kuziteka ardhi za Shaam na Bara Arabu mpaka Allaah Alipowapatia Waislamu ushindi chini ya uongozi wa Swalaah ud Diyn Hasan al-Ayyubi ambaye aliweza kuzirudisha nchi hizo kwa Waislamu.
Makhalifa 14 walipita, ambao walikuwa wanajiita masharifu na nasaba yao ni kutokana na Majusi au Mayahudi mpaka likawa maarufu baina ya watu wa kawaida hivyo kuiita dola hiyo, Dola ya Faatwimah na Dola ya ‘Alawi na ilihali uhakika ni Dola ya Kimajusi au ya Kiyahudi wakanaji Mungu.
Na miongoni mwa uovu wao ni kuwa walikuwa wakiwaamrisha makhatibu kwa hilo (yaani wao ni Alawiyyah Faatwimiyyuun) na hayo yalikuwa yakisemwa juu ya minbar na wakiandika katika kuta za Misikiti na sehemu nyinginezo. Na alihutubu yeye mwenyewe mtumishi wao kwa jina Jawhar, aliyeteka nchi ya Misri na kujenga mji wa Cairo. Alisema ndani yake: “Ewe Mola mswalie mja wako na rafiki yako tunda la Unabii na dhuria wako mwenye kuongoza muongofu anayepelekesha mambo. Naye ni Abi Tamiym Imam Mu‘iz-ud-Diinil Llah, Amiri wa Waumini kama ulivyowaswalia baba zake walio tohara na waliomtangulia kwa kuchaguliwa, maimamu waongofu”. Amesema uongo adui wa Allaah, hakuna kheri kwake wala kwa watangu wake wote wala kwa dhuria wake waliobakia na kizazi cha Unabii tohara miongoni mwao.
Na yule mwenye lakabu ya Mahdi, laana ya Allaah iwe juu yake aliwachukuwa wajinga na kuwasalitisha kwao wale wenye fadhila. Alikuwa akiwatuma kwenda kuwachinja mafakihi na wanavyuoni katika firasha zao. Na akawasaliti Waislamu kwa Warumi na alikuwa na ujeuri mwingi na kuchezea mali na kuwaua watu. Alikuwa na kipote cha walinganizi (ma-Du‘aat) wake waliokuwa wakifanya kazi ya kuwapoteza watu kwa uwezo wao wote. Wao walikuwa wakiwaambia baadhi ya watu: “Huyo ni Mahdi mtoto wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na dalili (huja) ya Allaah kwa viumbe vyake”. Na kwa wengine: “Huyu ni Mtume wa Allaah na dalili ya Allaah”. Na kwa wengine: “Yeye ni Allaah, Muumbaji, Mwenye kuruzuku”. Hapana Mola muabudiwa wa haki ila Allaah tu, Naye Hana mshirika, Ametukuka na Hana upungufu wala kasoro aina yoyote kwa yale wanayoyasema madhalimu kwa kiburi kikuu. Alipoangamia alichukua hatamu za uongozi mtoto wake anayeitwa, Qa’im, naye alizidisha shari yake juu ya uovu wa babake maradufu. Akatoka na kuwatusi Manabii na alikuwa akinadi masokoni na sehemu nyenginezo: “Mlaanini ‘Aishah na mumewe. Mlaanini pango na vinavyounganishwa”.
Ewe Allaah! Mswalie Nabii Wako na Maswahaba zake na wakeze walio twahara na uwalaani hawa makafiri walioasi na kuvuka mipaka katika ukanaji wa Allaah na Uwarehemu waliopambana nao na ikawa ndio sababu ya kuing’oa mizizi na utawala wao. Waislamu katika zama za utawala wao walipata dhiki na shida kubwa kwa ukatili, kiburi na ujeuri wao uliochupa mipaka.
Naye Shaykh ‘Abdulla Saleh Farsy (Allaah Amrehemu) katika kuelezea yalivyoanza Mawlid anasema:
“Walioanza Mawlid ni watu wenye Madhehebu za Kishia, hawa Shia Ismailiya walizitawala nchi za Kisuni tangu mwaka 297 A.H. (909) mpaka 567 A.H. (1171) (muda wa miaka 270).
Walipotoka katika nchi hizo waliacha hiyo ada yao ya kumsomea Mawlid Mtume na Maimamu zao. Basi Suni wakaendeleza Mawlid ya Mtume, wakayawacha yote mengine.
Mawlid ya Mwanzo Rasmi Kusomwa na Suni:
Mawlid ya mwanzo Rasmi yalisomwa na Suni ni Mawlid aliyokuwa akiyasoma Mfalme Mudhaffar Din- Mfalme wa kaskazi ya Iraq ambaye alikuwa shemeji wa mfalme mkubwa wa Kiislamu, Mfalme Salahud Din (Saladin – maarufu). Mawlid makubwa kabisa hayo. Yalikuwa yanahudhuriwa na watu wa pande zote zilizokuwa karibu na hapo, kwa shangwe kubwa kabisa lisilokuwa na mfano.
Mfalme huyo alizaliwa mwaka 549 A.H. (1154 wa kizungu); na akatawala hapo mwaka 586 A.H. (1190) na akafa 630 A.H. (1233) – miaka mia saba na khamsini na sita (756) kwa tarikhi ya kiislamu, na miaka mia saba na thalathini na tatu kwa tarikhi ya Kizungu. Basi ada ya kusoma Mawlid haikuanza miaka mingi sana. (Tafsiri ya Mawlid BARZANJI – KADHI SHEIKH ABDULLA SALEH FARSY, ZANZIBAR, Uk.(iv) )
(b)KUTOKUWEPO KWA USHAHIDI WA QURAN AU HADITHI KUHUSU TAREHE YA KUZALIWA MTUME.
Tarehe halisi aliyozaliwa mtume haijulikana kwa usahihi. Tarehehiyo haikutajwa si tu kwenye quran bali pia hakuna hadithi saheeh inayotaja tarehe ya kuzaliwa mtume. Hivyo wanazuoni wengi wamejaribu kubashiri tu tarehe ya kuzaliwa mtume.
Wana-taariykh wametofautiana kuhusu mwaka na mwezi aliozaliwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Safi-ur-Rahmaan Mubarakpuri, mwanachuoni aliyepata zawadi ya kwanza katika mashindano ya kuandika historia ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameandika yafuatayo katika kitabu chake: “Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), bwana wa Mitume, alizaliwa katika mtaa wa Bani Haashim katika mji wa Makkah, Jumatatu, tarehe 9 Rabi’ul Awwal, mwaka ule ule wa ndovu na miaka arobaini baada ya utawala wa Kisra (Khsru Nushirwan) yaani tarehe 20 au 22 Aprili 571 BI (Baada ya kuzaliwa ‘Iysa), kulingana na alivyohakikisha mwanachuoni mkubwa Muhammad Sulayman al-Mansourpuri na mwana-falaki Mahmud Pasha” (Ar-Rahiyqul Makhtuum, uk. 62).
Sirajur Rahmaan katika kitabu chake amesema: “Tukio hili la ndovu lilitokea mwezi wa Muharram kabla ya kuzaliwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa siku hamsini na tano, kama wanavyothibitisha wanavyuoni wengi. Nayo inawafiki mwisho wa mwezi wa Februari au mwanzo wa Machi mwaka 571 BI” (Al-Mustafa, nakala ya Ansaar Muslim Youth Organisation, 1993, uk. 11). Kutokana na mapokezi hayo mawili tunaweza kuiweka tarehe ya kuzaliwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baina ya tarehe 25 Swafar na tarehe 25 Rabi’ul Awwal na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anajua zaidi.
(c) USHAHIDI WA WANAZUONI KUHUSU UPAGANI WA MAULID:
Wanazuoni mbali mbali wamethibitisha jinsi waislam wanavyojiingiza katika uovu wa kusherekea maulidi. Imaam Ash-Shaatwibiy ndani ya kitabu chake cha Al-I’tiswaam (1/34) ambapo alitaja ndani ya kurasa zake za mwanzo baadhi ya aina za uzushi, akihusisha sherehe ya kuzaliwa Mtume kuwa miongoni mwao, akakemea sana kitendo hicho.
Imaam Al-Faakihaaniy kakemea sana kitendo cha Mawlid katika Risaalah yake maalum. 8/9.
Imaam Al-Haj Al-Maaliky kakemea naye Mawlid na kasema bid’ah katika kitabu Al-Mudkhal, 2, 11/12.
Mwanachuoni wa India, Abu Atw-Twayyib Shamsul-Haq Al-Adhwiym Abaadiy, naye kasema Mawlid ni bid’ah, na
Shaykh wake; Bashiyrud-Diyn Qannuujiy, ambaye ameandika kitabu kwa lengo hilo, alichokiita “Ghaayatul Kalaam fiy Ibtwaal ‘amal Al-Mawlid wal-Qiyaam”. Angalia sharh yake ya Hadiyth sahihi: “Yeyote anayezua katika Dini yetu katika yale ambayo sio (asili) katika hiyo (Diyn), halitakubaliwa”, Iliyopo katika Sunan Ad-Daaraqutwniy.
Mwanachuoni Abu ‘Abdillaah Al-Haffaar Al-Maalikiy kutoka Morocco amesema kwamba: (Sherehe ya kuzaliwa Mtume haikuwahi kufanywa na kizazi cha wamchao Allaah baada ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambao ni Maswahaba wake. Hawakupatapo kuitofautisha na nyakati nyengine za usiku kwa kazi nyengine yoyote. Kwamba wamejifunza kutoka kwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambaye hakupatapo kufanya ibada kwa Mola wake isipokuwa tu kwa yale Aliyomshushia.) [Al-Mi’yaar Al-Mu’arab. 7/99].
MASWALI:
1. Wapi katika Quran pamewaruhusu kusherekea Maulid ya kuzaliwa Muhammad?
2. Wapi katika Quran panasema Muhammad alizaliwa na aliishi?
3. Kwanini Waislam wanasherekea Maulid ya Muhammad ambayo haipo kwenye Quran?
4. Waislam nini mnafuata, Allah au Muhammad au Quran au Sahihi Hadith au Nguzo au Sharia?
Kumbe Maulidi ya Mtume Muhammad ni Sherehe ya Kipagani.
Max Shimba Ministries Org.

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW