Sunday, October 16, 2016

MAOMBI KUHUSU UCHUMI WA MAISHA YAKO


Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa #MATHAYO 6:33
Tumsifu Yesu Kristo mwana wa Mungu.
Ninamtukuza Mungu mkuu kwa neema zake nyingi zilizotufunika kwenye sherehe hizi za pasaka. Binafsi nimemuona Bwana kipekee.
Mwana wa Mungu, Kila eneo la maisha yetu tunavyoishi sote tunaomwamini Kristo ni sehemu ya utumishi wetu mbele za Mungu. Na Bwana anatamani sana aone namna gani kila mmoja wetu tunampa nafasi ya yeye kufanyika kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku kila jambo tulifanyalo. Mtume Paulo anasema kwa lolote tufanyayo kwa tendo au kwa neno tulifanye kwa jina la Yesu.
Hakika ni mapenzi ya Mungu kwamba tufanikiwe katika maisha yetu kwenye kipengele cha kiuchumi. Ni mapenzi yake. Na sio kwamba Bwana anatamani tuwe maskini. Hapana. Lakini bahati mbaya kwa sababu ya kuutafuta utajiri injili imegeuzwa na kuwa deal kwa baadhi yetu ‘watumishi’. Sasa Injili ya utajirisho imeziba msingi wa injili ambao ni toba na msamaha na kuwa utajiri na kufanikiwa. Mungu atusaidie sana sana.
Ni mapenzi ya Mungu tufanikie kiuchumi. Bwana anasema ‘NA ITAKUWA, KWA SABABU MWAZISIKILIZA HUKUMU HIZI, NA KUZISHIKA NA KUZITENDA, BASI BWANA, MUNGU WAKO, ATAKUTIMILIZIA AGANO NA REHEMA ALIYOWAAPIA BABA ZAKO; NAYE ATAKUPENDA NA KUKUBARIKIA NA KUKUONGEZA TENA ATAUBARIKIA UZAO WA TUMBO LAKO, NA UZAO WA NCHI YAKO, NAFAKA ZAKO NA DIVAI YAKO, NA MAFUTA YAKO, MAONGEO YA NG'OMBE ZAKO, NA WADOGO WA KONDOO ZAKO, KATIKA NCHI ALIYOWAAPIA BABA ZAKO KUWA ATAKUPA. UTABARIKIWA KULIKO MATAIFA YOTE’ #KUMBUKUMBU 7:12-14.
Hapa Bwana anazungumzia habari ya kufanikiwa kiuchumi. Kwetu Wakristo kufanikiwa kwetu msingi wake uko kiroho zaidi kuliko kimwili. Mungu anatamani tufanikiwe kiuchumi lakini kufanikiwa huku kuwe ndani ya mapenzi yake ili yeye awe sehemu ya furaha ya kufanikiwa kwako katika mali zako. Lakini pia anatamani kwanza roho zetu zianze kupona ndipo mambo mengine yote ya kimwili yapone na kufanikiwa. Anatamani hilo.

Mungu anataka ufanikiwe kwenye kazi yako, kwenye biashara zako, kwenye kila jambo jema unalolifanya kwa ajili ya uchumi. Na kwa sababu anatamani yeye awe sehemu ya mafanikio yako. Mungu ndiye anayetupa nguvu za kuwa na utajiri.
Ni mapenzi ya Mungu tufanikiwe wapenzi. Mungu alivyomuumba mwanadamu alimtaka afanikiwe kiuchumi. Maandiko yanasema ‘Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, MKAONGEZEKE, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi #MWANZO 1:27-28. Bwana alimtaka mwanadamu akaongezeke si tu kwa idadi lakini katika fedha na mali. Ibrahimu katika kufanikiwa na kubarikiwa kwake kuliendana sambamba na suala la uchumi. Uchumi ni wa msingi kwenye maisha ya kumtumikia Mungu.
Lakini liko tatizo la msingi kwenye utajiri ambao wengine tumekuwa tukiutamani kwa nguvu kubwa. Kwanza watu wamekosa hekima na maarifa ya Mungu katika uchumi wao. Wengine wamekuwa hawataki kabisa kumuhusisha Mungu kwenye kazi au biashara zao ili Bwana awe sehemu ya maisha yao ya kila siku. Na wengine yamkini wametamani fedha na mali hizo wazitumie pekee yako kuliko kuzitumia pamoja na Mungu.
Bwana aendelee kutupa nafasi nitayazungumza haya kwa upana wake kesho na kesho kutwa. Mungu anatamani aone kwanza akili zetu na fahamu zetu ziponywe na yeye. Tuutafute kwanza ufalme wake. Katika kila jambo tunalolifanya ni muhimu kujua ni nini yaliyo mapenzi ya Mungu katika jambo hilo. Lakini pia katika kazi unazozifanya ni lazima uzifanye kwa bidii. Ndugu zangu kwenye ufalme wa Mungu nimekuwa nikisema wazembe hatuwahitaji. Mtu ambaye hata hataki kutumia dakika 30 kuomba kwa ajili ya maisha yake, mtu ambaye hawezi kutumia dakika 5 tu kujifunza neno la Mungu limponye na kumsaidia, watu wa namna hii kwenye ufalme wa Mungu watachelewa sana. Hatuwataki. Watu ambao wako busy kuipendeza dunia kuliko kumpendeza Mungu. Imeandikwa ‘Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe.#MHUBIRI 9:10. Ndo maana hata mimi sifanyi makosa kuhubiri injili. Kwa nguvu zangu zote nitaihubiri injili. Nimedhamiria.
Sasa mpendwa wangu hebu tusimame pamoja sasa kwa maombi haya. Simama kusema jambo kuhusu uchumi wako na wa familia yako. Wewe ambaye huna kazi tuseme na Bwana akafungue milango ya kupata kazi. Wewe ambaye unatafuta mtaji tukaseme na Bwana akupe mtaji. Mwambie Bwana ni mapenzi yake wewe ufanikiwe.
Wewe ambaye yamkini unasumbuliwa na madeni sugu, nakusihi simama nami tumwambie Bwana akupe neema na kibali kuhusu madeni hayo. Najua madeni yanavyotesa. Wafanya biashara na hata wafanya kazi najua jinsi madeni yalivyo mzigo. Wengine kwa sababu ya madeni wamezalisha matatizo mengine ndani ya mioyo yao. Muombe Mungu akupe kibali na neema kuhusu madeni hayo. Uwe kulipa na ujipange upya namna ya kusonga mbele.
Barikiwa sana
Neno la Uzima Org.
For Max Shimba Ministries Org

1 comment:

Unknown said...

Asante mtumishi wa Mungu. Mimi. Nasumbuliwa sana na madeni na biashara imekataa kabisa. Naomba msaada wako.

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW