Friday, August 26, 2016

Je, Nafsi tatu zaweza kuwa Mungu mmoja?

Hili ni swali nyeti sana na huenda ndilo msingi wa sababu hasa za baadhi ya watu katika ulimwengu wa dini kupinga fundisho hili la kweli la Kibiblia juu ya Utatu Mtakatifu na Uuungu wa Bwana Yesu. Hoja kubwa katika sehemu hii inaonekana kuwa ni ya kimahesabu zaidi ambapo jamii ya wale wanaopinga utatu mtakatifu hudai kuwa haiwezekeni Baba, Mwana na Roho mtakatifu yaani mamlaka tatu kuwa Mungu mmoja. Yaani hiyo ni sawa na kusema 1 + 1 + 1 = 3 na siyo 1’ kwa hiyo Baba + Mwana + Roho Mtakatifu = Miungu watatu. 

Kwa mtazamo huu ninalazimika katika sehemu hii kushughulika na dhana ya kimahesabu zaidi ili kuona kama madai hayo ni sahihi na kama yanaweza kupatiwa ufumbuzi wa kifarsafa katika maandiko. Katika kulipatia swala hili ufumbuzi ni vyema tukaongozwa na mtazamo wa kimaandiko kupitia fungu la kitabu cha ISaya… 

Isaya 55:8 Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana Hiyo ni tahadhari ya msingi sana katika kushughulika na mada hii, Mungu mwenyewe katika kitabu hicho cha Isaya anaweka bayana kuwa katika utendaji wake njia anazozitumia hutofautiana sana na njia zetu za kibinadamu na hata mawazo yetu yako tofauti na mawazo yake. Ukweli wa tamko hilo la Isaya tunaweza kushuhudia katika kipengele hiki cha uchambuzi ambapo kama utakumbuka hoja ya msingi ya upinzani juu ya Utatu mtakatifu imejengwa katika kile kinachoonekena kuwa nafsi tatu haziwezi kuwa Mungu mmoja kwa kuwa moja jumlisha moja jumlisha moja jumlisha moja ni sawa na tatu (1+1+1 = 3). 

‘Hebu tuichunguze hesabu hiyo (Nafsi tatu - Mungu Mmoja) katika maandiko’ Baba Mwana/Neno Roho Mtakatifu Mungu mmoja Elohim’ Mafundisho na mifano mbalimbali ya kimaandiko katika Biblia vinaweka bayana juu ya usahihi wa fundisho hili la kweli na la msingi katika Ulimwengu wa imani ambapo kama hatua ya juu zaidi ya uwazi wa fundisho hili maandiko ya Biblia yanaweka bayana usahihi wa jibu la Mungu mmoja toka katika hesabu ya nafsi tatu za Mungu . Fuatilia mifano na uchambuzi huu:

- Umoja katika wingi ‘A’ 
Ushahidi wa kwanza wa msingi juu ya Mungu mmoja katika nafsi tatu ni ule unaotoka katika kimya cha Mungu mwenyewe kama tunavyosoma katika andiko la kitabu cha Mwanzo;- Mwanzo 1:26-27 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. 


Sehemu hiyo ya kwanza ya andiko hilo Mungu kwa kutumia tamko la mfumo wa uwingi yaani utatu mtakatifu kama tulivyoona hapo awali anasema ‘Natuumbe mtu kwa mfano wetu’. Ni wazi kuwa tamko hilo linatoa taswira ya uwingi, lakini kile kinachoonyesha kuwa uwingi huo hubeba tu dhana ya upana wa utendaji wa Mungu mmoja katika nafsi tatu na si miungu watatu, ni tamko linalofuata katika aya ya 27 ya kitabu hicho cha Mwanzo..hebu tuisome:- 

(27 ) Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Haya hebu ona sasa’, tamko la awali lilibeba dhana ya wingi pale Mungu aliposema ‘Na tuumbe mtu kwa mfano wetu’ lakini tamko linalofuatia linarejesha dhana ya umoja wa Mungu kwa kusema ‘Mungu akaumba mtu kwa mfano wake’. 

Ni wazi kuwa kile kinachomaanishwa katika aya hizo mbili ni kuonyesha kuwa uwingi au upana huo wa otendaji wa Mungu uko ndani ya umoja wake na si badala yake kwamba nafsi tatu huzalisha aina nyingine ya miungu na kuongeza idadi toka ile ya Mungu mmoja na sasa kuwa miungu watatu. 


“Uelewa juu ya Mungu katika zama za Wayahudi - Israel” 
Ni vyema ikumbukwe kuwa tangu kipindi cha Wayahudi huo ndio ulikuwa uelewa wa Wayahudi (Israel) juu ya Mungu. Wayahudi walimtambua Mungu kwa jina la “Elohim” jina linaloonekana kutumika zaidi ya mara 2.602 katika maandiko ya Biblia ambapo jina hili ni la mfumo wa uwingi wa neno “Eli “(Mungu) hivyo neno Elohim linabeba dhana ya uwingi ndani ya umoja. (It has connotations of plurality). Pamoja na uelewa huo bado mtazamo wa Wayahudi ulikuwa ni juu ya ukweli wa Mungu mmoja tu na si zaidi, ambapo hapa tena Wayahudi walikuwa na fundisho lililotawala sana la “Monotheistic” – Mono kwa kiyunani humaanisha Moja’ na Theistic humaanisha Mungu. 

Dhana hii ya Mungu hujengwa katika Biblia kupitia fungu ambalo Wayahudi huliita Shema’ toka asili ya Kiebrania lenye maana Sikia” ambalo ni:- 

Kumbukumbu 6:4 Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja Kupitia andiko hilo jamii ya Wayahudi ilijenga msingi wa imani usiotikisika juu ya Mungu mmoja. Lakini pamoja na hayo ikumbukwe kuwa dhana hii ya Mungu mmoja pia ilizingatia asili ya Mungu katika utendaji wake wa nafsi tatu za  milele kama tulivyoona msingi wake. Na hata katika fungu hilo la shema’(kumb 6:4) tunaona dhana ya Mungu mmoja inatajwa kupitia tamko ….”Bwana ndiye mmoja” ambapo neno lililotumika kumaanisha ‘mmoja’ ni neno la lugha ya asili ya Kiebrania Echad’(mmoja). 

Neno hilo ‘Echad’yaani ‘mmoja’(muunganiko – to be united) bado hubeba dhana ileile ya umoja ndani ya uwingi kwa kile kinachoonekana kuwa neno hilo hilo Echad’ ndilo lililotumika kumaanisha umoja katika farsafa ya muunganiko wa wanandoa wa jinsia mbili yaani mume na mke kama tunavyosoma katika:- 

Mwanzo 2:24 Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja (echad’). Neno hilo’..watakuwa mwili “mmoja’ neno ‘mmoja’ hapo limetafsiriwa toka kwenye neno lilelile la Kiebrania lililotumika kueleza umoja wa Mungu (Echad), hivyo kwa mtazamo huo ni kumaanisha kuwa dhana ya umoja huu hujengwa katika matokeo ya muunganiko wa vitu zaidi ya kimoja na hivyo hueleza utendaji wa upana wa nafsi zaidi ya moja za Mungu. Katika kuendelea kujibu swali hili hebu tuone mifano mingine kadhaa juu ya uwezekano wa nafsi tatu kuwa Mungu mmoja, ambapo kama tulivyoona upande unaohoji swala hili umejikita kwenye dhana ya kimahesabu zaidi, kuwa je’ moja jumlisha moja jumlisha moja jumlisha moja yaweza kuwa moja?, hebu sasa twende mbele zaidi kwa kungalia ushahidi mwingine wa kimaandiko utakaotusaidia kwa uwazi kupata jibu la msingi juu ya umoja katika nafsi tatu. 


Umoja wa Mungu katika nafsi tatu ‘B’ 
2Petro 3:8 Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja 

Hili ni andiko muhimu sana katika mchakato wa kujibu hoja hii yenye sura ya kimahesabu, kama ilivyo hoja yenyewe andiko la Petro nalo linavunja dhana hiyo kwanza kwa kuonyesha kuwa mahesabu ya Mungu na ya mwanadamu ni tofauti sana, yani kile tunachoona kuwa ni wingi kwetu kama wanadamu kwa Mungu siyo wingi. Rejea upya sehemu ya kati hadi mwishoni ya andiko hilo la 2Petro 3:8‘…kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 

Ili kupata urahisi wa ufumbuzi wa hoja yetu tunaweza tukageuza kidogo maneno hayo kwa kusema’ “kwa Bwana’ Mungu mmoja ni kama na nafsi tatu, na nafsi tatu ni kama Mungu mmoja”. 

Ni imani yangu kwa mfano huo ndugu msomaji wangu umeanza kupata pambazuko la ufahamu juu ya hoja hii na kwa kadri tunavyoendelea na uchambuzi huu kupitia maandiko na mifano mbalimbali tutakayopitia ninaamini hutakuwa na shaka tena juu ya uelewa wa fundisho hili muhimu la imani. 

‘Muunganiko wa vitu zaidi ya kimoja unaozaa kimoja’(plurality in unity)

 Biblia inayo mifano mbalimbali juu ya uwezekano wa kuwepo kwa muunganiko wa vitu zaidi ya kimoja lakini vikatengeneza kitu kimoja kama tunavyoweza kuona katika aya zifuatazo:- 

Mwanzo 1:5 Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja Andiko hilo la Mwanzo linaeleza juu ya kanuni inayofanya kupatikana siku moja’ kuwa ni muunganiko baina ya usiku na mchana au kwa lugha nyingine nuru na giza ndivyo vinazaa siku inayoitwa siku moja na siyo siku mbili. 

Hivyo kwa maana nyingine haitakuwa sahihi kuchukulia kuwa muunganiko wa nafsi tatu za Mungu unafanya miungu watatu na huku tukikubali kuiita moja siku inayozaliwa na muunganiko wa hali mbili ya giza na nuru katika mzunguko wa majira. Hebu tufanye hesabu hii...,Usiku + Mchana = Siku moja’ (Mwanzo 1:5) Sasa tufanye nahii tena …. ,

Baba + Mwana +Roho = Mungu mmoja’(1Yoh 5:8) Nina amini kuwa sasa unaendelea kupata pambazuko juu ya mada hii na hivyo hofu na mashaka yako vinaanza kutoweka. Hebu tupitie andiko jingine kidogo;- Ezekieli 37:17 Ukaviunge pamoja kwa ajili yako hiki na hiki viwe kijiti kimoja, viwe kimoja katika mkono wako. 

Hilo ni agizo lililowahi kutolewa na Mungu kwa nabii Ezekieli ambapo Mungu anamwambia Ezekieli achukue vijiti viwili na kuviunganisha ili apate kijiti kimoja mkononi mwake. Hivyo kwa msingi wa maelekezo hayo tunaona Biblia ikiweka mkazo juu ya uwezekano wa kuzaliwa kitu kimoja au umoja toka kwenye muunganiko wa vitu zaidi ya kimoja lakini kile kinachozaliwa kikaitwa kimoja, hivyo dhana ya kutowezekana kwa nafsi tatu kumhusu Mungu mmoja inaondolewa kabisa na maandiko haya ya haki ya Biblia takatifu. Mifano rahisi Utatu katika Yai’ – endapo utachukua yai na kulichemsha na kisha baada ya hapo ukaanza kulimenya’ utagundua kuwa ndani yake kuna vitu zaidi ya vitatu yaani “Nganda gumu kiasi la nje, “Nyama laini nyeupe ya ndani na “Kiini ambavyo kimsingi havijawahi kupelekea mtu yeyote baada ya kumenya Yai hilo kudai kuwa hayo ni mayai matatu, badala yake wote tunakiri kuwa ni Yai moja tu pamoja na utatu uliyomo ndani yake. 

Hivyo mifano hiyo midogo itusaidie kurahisisha tafakuri zetu na ugumu wa kuamini katika fundisho hili sahihi na la kweli la Utatu Mtakatifu. 

Lenzi mbili toka chanzo kimoja cha Jicho’ Pamoja na mfano huo lakini mara kadhaa katika mahubiri yangu nimekuwa nikitumia pia mfano wa macho kufafanua dhana ya umoja katika katika wingi, katika mfano huu kwanza nimekuwa nikihoji watu kuwa uwezo wao wa kuona unatokana na asili ya macho mangapi! Ambapo wengi wao wamekuwa wakijibu kuwa wanaona kwa asili ya mambo mawili’ baada ya jibu hilo huwa ninawaomba wale wanaodai kuona kwa asili ya macho mawili watumie macho hayo mawili kuangalia kushoto na kulia kwa wakati mmoja’ tendo ambalo hushindakana. Kwa tafakari hiyo ndipo tunagundua kuwa mwanadamu yeyote ana asili moja ya jicho au chanzo kimoja lakini Mungu ametuwekea lenzi mbili ili kuwa na upana wa kuona lakini chanzo au kontroo ya jicho ni moja tu. 

Kwa hiyo Mungu mmoja anaweza kujifunua katika nafsi zaidi ya moja lakini bado hudumu kuwa Mungu mmoja lakini anayetenda katika wigo mpana zaidi wa mamlaka. 

Dunia ya Utatu’ 
Ni jambo linalonistua binafsi kwa jinsi Mwenyezi Mungu alivyoweka ushahidi mwingi wa utatu hata katika muundo wa Kisayansi na wa Kijografia wa Ulimwengu na hivyo ninachelea kwamba wale wanapinga fundisho hili huenda hata sayansi ikawahukumu katika siku ya kiyama juu ya mantiki ya upinzani huo. Hebu ona jinsi nyanja mbalimbali za kisayansi na kijografia zilivyotawaliwa viashiria au ushahidi wa kielelezo cha utatu:- 

 Ili kupata ’ World muungano wa Earth + Air + Sky 
 Ili kupata ’Universy muungano wa Mass + Space + Time 
Ili kupata ‘Atom muungano wa Proton + Electron + Neutron 
Ili kupata ‘Time muungano wa Present + Past + Future 
Ili kupata ‘Sphere muungano wa Lithosphere+Hydrosphere +Atmosphere 
Ili kupata ‘ Number muungano wa Positive + Zero + Negative 
Ili kupata ‘ Air muungano wa Nitrogen +Oxygen +Water 
Ili kupata ‘water muungano wa Hydrogen x2’ na + 0xygen 
Ili kupata ‘Music muungano wa Melody+ Harmon +Reazim 

Kwa hali hiyo kile kinachoonekana ni kuwa’ farsafa ya utatu imetawala sehemu kubwa ya jografia na uumbaji kwa jumla tendo ambalo binafsi ninaliona kama kielelezo cha ushahidi wa uhalisia wa fundisho hili la utatu mtakatifu,na kwa kwanamna nyingine ni jibu la vitendo dhidi ya hoja za mtazamo wa kutowekana kuzaliwa umoja toka kwenye wingi. 

 Utatu Mtakatifu katika ibada za viumbe wa mbinguni’ 
Ushahidi mwingine wenye nguvu ambao kimsingi ndiyo unaohitimisha kipengele hiki cha uchambuzi ni ule unaohusu mfumo wa ibada za mbinguni ambapo matamko yanayotolewa na viumbe hao wanaoabudu huko mbinguni yanaweka bayana juu ya msingi mzima wa Utatu wa Mungu hebu tusome katika andiko hili la Ufunuo wa Yohana”- Ufunuo 4:8 Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja. 

Hivyo ndivyo maandiko ya Biblia yanavyoweka wazi juu ya ibada hiyo ya mbinguni ambapo viumbe hao wanaoabudu mbele za Mungu hutoa matamko hayo yanayoweka uthibitisho na ushahidi wa wazi juu ya utatu wa Mungu kwa kusema mara tatu Mtakatifu,Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja. 

Licha tu ya kutamka Mtakatifu mara tatu, lakini pia viumbe hao wanaweka wazi sifa za walengwa wa utatu huo kwa kuwataja’ aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja. Kwa tafakari isiyo na ugumu wowote utagundua kuwa sifa hizo husimamia nafsi hizo za Mungu ambapo ile ya kwanza aliyekuwako – huonekana kumlenga Mungu Baba, aliyeko - humlenga Roho Mtakatifu ambaye kimsingi ndiye anayetawala sasa, atakayekuja - humlenga Yesu ambaye dunia inangoja kuja kwake mara ya pili na hata mbingu nayo inangoja kushuka kwake duniani baada ya kumaliza kazi yake ya ukuhani wa upatanisho katika hekalu la mbinguni na hatimaye kurejea na wateule aliowakomboa mbinguni. Mungu akubariki kwa kuanza upya kujenga ufahamu wako baada ya kupata ufafanuzi huu wa msingi toka katika ushahidi wa neno la Mungu. 

DARUBINI YA IMANI Na. Mchungaji Dominic Mapima

1 comment:

Unknown said...

Hii article ilikosa hata comments, maana kama ulitoka yumbishwa kiimani Unakuta umerud Tena na Imani thabiti

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW