Sunday, November 20, 2016

KURUDI KWA MASIHI NA DALILI ZAKE


Namshukuru Mungu kwa mara nyingine tena kukuletea mfululizo wa pili wa somo la 'NI MUHIMU KUJUA MAJIRA NA NYAKATI UNAZOISHI'. Ni matumaini yangu kuwa kama unafuatilia vizuri masomo ninayokutumia unabarikiwa na unajifunza kitu kwa namna moja ama nyingine. Sasa naomba jifunze sehemu hii ya pili ambayo nimelenga kukueleza machache tu kwa habari ya kurudi kwa Bwana Yesu kulichukua kanisa, dalili zake na mambo yatakayojili baada ya hapo.
Nikueleze tu kwamba siku za mwisho zilianza mara tu baada ya Yesu kupaa.
Yesu hakuweka wazi kuwa ni lini atarudi kulichukuwa kanisa, lakini aliweka wazi mambo kadha wa kadha juu ya kuja kwake. Alisema katika Mathayo 24:36, kwa habari ya siku ya kurudi hata malaika hawajui ila baba mwenyewe.
Mathayo 24.
Kitabu hiki kinaeleza kwa ufupi, ila kwa umakini wa hali ya juu sana kwa kile kitakachotokea. Nia na madhumuni ya kitabu hiki ni kukujulisha kwa habari za siku za mwisho, dalili zake na kurudi kwa masihi wa Bwana. Maana yake ni kwamba matukio ndiyo yatakayoeleza nyakati. Natamani uone jambo hili kwamba majira na nyakati za kurudi kwa Bwana huelezwa na matukio yanayojili, na ndio maana kila wakati Yesu alisema, "...mkiona...mjue..." Sasa naamini unaelewa namaanisha nini. Natamani sasa niweke kile kitakachotokea kwa mfululizo wake, moja baada ya jingine;
Kupaa kwa Bwana Yesu kwenda mbinguni.
· Jambo hili lilishatokea tayari, hata wewe ni shahidi wa hili na ndio maana umeokoka unasubiri kwenda mbinguni. Soma Mdo 1:9-11; Luka 24:51; Marko 16:19
Dalili za siku za mwisho.
· Kubomolewa kwa hekalu: Yesu alisema katika Mathayo 24:2, "...amin, amin nawaambieni, halitasalia hapa jiwe ambalo halitabomoshwa". Hii ni baada ya wanafunzi wake kumuonesha mawe ya hekalu na misingi yake ilivyo imara.Hekalu lilikuja kubomolewa miaka 70 AD. Na sasa eneo hilo lilipokuwepo hekalu limejengwa msikiti.

· Dalili nyingine nyingi: Soma hiyo mathayo kuanzia mst wa 4 utaona dalili nyingi ambazo nyingi zimeshatimia hadi sasa; mfano, vita, matetemeko ya ardhi, magonjwa ya kutisha, maarifa kuongezeka (angalia teknolojia ilivyo juu sasa hivi), n.k
Kurudi kwa Yesu mara ya pili (unyakuo).
Hili ndilo subirio kubwa la watakatifu wa Mungu. Siku moja nikawaambia watu kwamba kama mimi ningeulizwa Yesu arudi sasa ama la, ningesema asirudi kwanza, watu walinishangaa, labda na wengine kuniona natania. Pengine nawe waweza kunishangaa, lakini ngoja nikwambie, nilisema hivyo kwani nilikuwa nikiangalia kiwango nilichotumika, nikaona bado sijafanya kazi ya kuridhisha. Sijafika sehemu ya kusimama kama Paulo na kusema, "...kazi nimeimaliza, vita nimevipiga, imani nimeilinda..." Nasema hivyo kwani tukifika mbinguni tutapewa taji, na 'size' ya taji itategemea kazi uliyofanya! Sasa nafikiri unaelewa kwa nini nilisema vile.
· Mathayo 24:27,28,40,41. "Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adamu. Kwa kuwa popote ulipo mzoga ndipo wakutanikapo tai...Wakati ule watu wawili watakuwepo kondeni, mmoja atwaliwa mmoja aachwa;wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa."
· 1 Thesalonike 4:16,17. "Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele..."
· 1Kor 15:52,53. "Kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uhalibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti huu (mwili) uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa." Ieleweke kwamba wakati parapanda itakapolia, wafu waliolala katika Kristo, yaani waliookoka peke yao ndio watakaofufuka. Watakaomwona Kristo kwa wakati huu ni watakatifu peke yao. Kristo hataigusa ardhi kwa wakati huu, na badala yake tutamlaki mawinguni. Shughuli za dunia hii zitaendelea kama kawaida. Pia uelewe kwamba mbinguni hatutakaa milele. Huko tutaimba wimbo wa mwana-kondoo, tutakula karamu ya mwana-kondoo na kuvikwa taji za ushindi, KWA KADRI YA KAZI TULIZOFANYA. Tutakaa huko kwa miaka saba kisha tutashuka duniani na Bwana (Nitatoa somo hili la 'badget' ya miaka kulingana na matukio kwa kutumia kitabu cha Daniel 9:24-27) na ndipo tutatawala na Bwana kwa miaka elfu duniani.
Dhiki kuu.
· Jambo hili, niaminivyo mimi kulingana na maandiko, litatokea huku duniani wakati sisi watakatifu tukiwa mbinguni. Huu ndio wakati ambao mpinga Kristo atafanya kazi. Kinachomzuia sasa ni kanisa. 2Thes 2:6,7. "Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa kwa wakati wake. Maana ile siri ya kuasi sasa inatenda kazi; lakini yupo azuiaye(kanisa) sasa, hata atakapoondolewa."
· Ukisoma kitabu cha ufunuo kuanzia sura ya nne utaelewa ninachosema. Ile sura ya tisa anaeleza baadhi tu ya dhiki hizo.
· Chapa ya mpinga Kristo itafanyakazi wakati huu. Ufunuo 13:18. "Yeye mwenye akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita."
· Wengi watakufa kwa makali ya upanga. Lakini pia watu watatafuta mauti, haitakuwepo. Yaani mtu anatafuta kufa lakini hafi! Ufunuo 9:5,6. "Wakapewa amri kwamba wasiwaue, bali wateswe kwa miezi mitano...Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, mauti itawakimbia."
· Hii dhiki ni kubwa,kila atakayekuwepo atajuta kuwepo. Niliposoma kitabu hiki cha ufunuo nilishangaa, kuna watakatifu(waliookoka) watakuwepo. Nikajiuliuza kwa nini; lakini kumbe ni wale ambao hawakutenda kazi; yaani walikuwepo tu duniani wakisubiri kwenda mbinguni. Wakati mbinguni tunakwenda kupewa taji za kazi tulizofanya, wao hawakufanya kazi.
kurudi kwa Yesu mara ya tatu.
· Hapa tutarudi ama tutashuka pamoja na Bwana tukitokea mbinguni, tukiwa tumevaa taji zetu za ushindi. Tutakuja kuitawala dunia. Mathayo 24:30,31 anasema, "...ndipo itakapoonekana ishara yake mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza nao watamwona mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi." Kumbuka pale mwanzoni, akija mwana wa Adamu mara ya pili, watakatifu watamlaki mawinguni wakishangilia na kuondoka naye; hapa anasema anakuja na utukufu mwingi, badala ya watu kushangilia na kuondoka naye, wanaomboleza!
· Hapa ndipo pale Paulo anasema, kila jicho litamwona! Si kama mkombozi tena, ila kama mtawala, hakimu n.k.
· Tutakaa pamoja naye katika mlima wa mizeituni kule Israel, yaani pale ndipo itakapokuwepo Ikulu ya ufalme huo. Tena Biblia inasema itakuwepo kambi ama ngome ya watakatifu.
Kutawala na Bwana miaka elfu (Millenium of Peace) Ufunuo 20:1-6
· Tutawala na Kristo, shetani atafungwa kipindi chote hiki cha miaka 1000, mpinga Kristo atatupwa Jehanamu ya moto, pamoja na yule nabii wa uongo (kumbuka hawa watakuwa wanadamu wa kawaida tu, yaani mpinga Kristo na nabii wa uongo).
· Utakuwa ni wakati wa amani mno, nabii Isaya anasema, "...mwana-simba atacheza na mwana-kondoo..."
· Ufunuo 20:5,6. "Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa ukuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu."
Hukumu ya mwisho (The last judgement) Ufunuo 20:11-15
"Nikaona wafu wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawa sawa na matendo yao...na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto."
· Hapa ni baada ya ile miaka elfu, wale ambao hawakufufuka bado, yaani walikufa katika dhambi, watafufuliwa hapa ili wasomewe hukumu zao.
· Hukumu hii ni ukomo wa mambo ya zamani, mara baada ya hapo tutaanza kuona mambo mapya kabisa.
Mbingu mpya na nchi mpya. Ufunuo 21:1-7
"Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi za kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari...Tazama maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao,nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao...Tazama nayafanya yote kuwa mapya...Yeye ashindaye atayarithi haya, mimi nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu."
· Huu ndio mwisho uliokuwa ukisubiriwa kwa zaidi ya miaka 1000 baada ya unyakuo. Hapa ndipo tutaishi milele na milele.
· Huu mji mpya, Yerusalemu una sifa nyingi ambazo kwa namna ya kawaida hazielezeki, kila nikipiga picha, kila siku napata picha mpya. Njia zake ni dhahabu tupu, milango yake ni lulu safi, n.k. Soma mwenyewe Ufunuo 21:9-27.
· Biblia haisemi baada ya sisi kuingia mji huo utapaa kuelekea mbinguni kama ulivyoshuka, ila inasema tutaishi humo, tena tukiingia na kutoka kwani milango yake haitafungwa daima.
· Nionavyo mimi, wala si Roho sasa, ni mawazo na maoni yangu mimi, kwamba hatutaondoka kwenda mbinguni tena, ila tutakaa humo tukiingia na kutoka, yaani tutakuwa tukingia na kutoka ndani ya mji, ili kufurahia mji pamoja na hii mbingu na nchi mpya ambazo Mungu amezitengeneza. Maana kama tutaondoka tena, hii nchi mpya nani atakaa? Nawe waweza kuwa na mawazo yako. Biblia inasema tunajua kwa sehemu tu.
Nimalize kwa kukupa angalizo kwamba, kuna 'doctrines' nyingi sana kwa habari ya siku za mwisho, hivyo kile ninachokuletea ni kile ninachoamini mimi. Huwa napenda kuwaambia watu kwamba, ni muhimu sana kuweka machujio (filters) ya kiroho, kuchuja kila unachopokea, kwa kutumia maandiko na Roho mtakatifu ndani yako na ndipo uamini kwani kuna mafunuo mengi mno katika siku tunazoishi leo, hivyo kuwa makini!
Lakini pia, jiweke tayari muda wowote, ufaao na usiofaa, kwani huwezi kujua ni lini na saa ngapi Bwana wetu atarudi. Paulo alisema, "...tusije tukawa watu wa kukataliwa siku ile..."
Basi neema ya Kristo na ikutunze, zaidi sana Roho mtakatifu akuwezeshe kuyaelewa haya. Usisahau kuwatumia wengine. Ukilichukulia hilo kama wajibu, kwa namna ile ile mimi nilivyolichukulia kama wajibu wangu kukutumia wewe, tutafanikisha pamoja kuujenga mwili wa Kristo.
Kwa maswali,ushauri ama mawasiliano ya namna yoyote ile na saa yoyoye,
Ev. Azgard S. Chamulungwana
sheghwede@yahoo.com
+255713990607

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW