Thursday, September 22, 2016

OMBA KWA JINA LA YESU KRISTO

KILA mkristo anapenda awe na maisha ya maombi yaliyo na mafanikio – anapenda akiomba kitu kwa Mungu ajibiwe. Lakini mara nyingi nimewasikia wakristo kadhaa wakisema wameomba jambo Fulani kwa Mungu lakini hawajajibiwa. Wengine wanapofikia hali ya namna hii, hukata tama – hata wokovu unaanza kupoa utamu wake.
Image result for jina la yesu kristo
Kuna sababu nyingi ambazo zimeandikwa ndani ya Biblia zinazoeleza chanzo cha kutijibiwa maombi ya watu. Sababu mojawapo ni kutokuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu – au kwa tafsiri nyingine kuomba kinyume na maagizo ya Mungu (Yohana 5:14-15)
Yesu Kristo alituachia maagizo mbalimbali juu ya maombi katika kulitumia Jina lake – mojawapo ni hili;

                        Tumuombe Baba kwa jina la Yesu Kristo.
Katika kitabu cha Yohana 16:23-24; Yesu Kristo alisema;  “Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.”
Wazo la kwanza tunalopata katika agizo hili ni kuelekeza mawazo na maombi yetu kwa baba Yetu aliye mbinguni wala si kwa malaika wala kwa wanadamu. Ndiyo maana imeandikwa; “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” (Waebrania 11:6)
Yesu Kristo alipokuwa anawafundisha kuomba alisema; “basi ninyi saline hivi; Baba yetu uliye mbinguni….” Jambo kubwa alilotaka wanafunzi waone ni umuhimu wa kujua na kuelekeza mawazo na maombi yao kwa BABA MUNGU. Watu wengi wamekwama kwenye maombi kwa kuwa katika mawazo yao wamewategemea sana watu katika kupata majibu ya maombi yao badala ya kumtegemea Baba Mungu.
Sisemi ni vibaya kushirikiana na watu wengine katika maombi – hapana. Bali nataka ujue kuwa hata ukiwashirikisha watu wakusaidie kuomba – wewe elekeza mawazo yako kwa Baba Mungu na kumtegemea Yeye kukujibu.
Wazo la pili tunalolipata katika maagizo ya Yesu Kristo juu ya maombi yaliyoandikwa katika (yohana 16:23-24) ni tuombe kwa Jina lake. Hakusema tuombe kwa ajili yake au kwa niaba yake, bali alisema tuombe kwa jina lake.
Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.” (yohana 16:23-24)
Mara kwa mara utawasikia watu wakimaliza maombi yao kwa kusema “kwa ajili ya Yesu Kristo, amina”. Lakini sioni mahali ambapo Yesu Kristo alisema tuombe kwa ajili yake. Hebu fikiri mtu anaomba uponyaji wa tumbo halafu aombe akisema “Naomba tumbo langu lipone kwa ajili ya Yesu Kristo”. Je! Ni Yesu Kristo anayehitaji uponyaji au ni wewe?
Yesu Kristo alisema tuombe kwa Jina lake na siyo tuombe kwa ajili yake wala kwa niaba yake – kumbuka hilo kila wakati unapolitumia jina la Yesu Kristo katika maombi. Lakini kama unataka mtu apone kwa ajili ya Yesu Kristo, basi omba kwa jina la Yesu Kristo – ili Jina hili litukuzwe.
           
     
                        Maombi ya mapatano kwa Jina la Yesu Kristo.

“Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.” (Mathayo 18:19-20)
Maombi ya mapatano kwa Jina la Yesu Kristo yana uwezo wa ajabu. Yesu Kristo alisema watu waliokusanyika kwa jina lake wakipatana kuomba JAMBO LOLOTE watafanyiwa na baba yetu aliye mbinguni.
Kwa nini iwe hivyo? Yesu Kristo alisema, “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.” Kwa maneno mengine tunaweza kusema jina la yesu Kristo limebeba uwepo wa Yesu Kristo. Palipo na Jina la Yesu Kristo, Yeye mwenyewe Yesu Kristo yupo – na atahakikisha mnaloliomba linapatikana. Unapoliitia jina la Bwana mahali popote ulipo, Yesu Kristo anatokea hatakama humuono kwa macho ya kimwili.
Kuna wakati Fulani mwaka 1986, watu Fulani walifika nyumbani kuambia kuwa matokeo ya mitihani waliyofanya mwishoni mwa mwaka wa kwanza katika chuo walichokuwa wanasoma yametoka, na kwamba mwenzao mmoja ameshindwa masomo matatu kwa hataendelea na masomo tena. Kwa hiyo kwa kufika nyumbani kwangu, walikuwa wamemsindikiza mwenzao kuniaga.
Habari hizo nilipozisikia sikuzipenda kwa kuwa nilifahamu kuwa watu hao walikuwa wacha Mungu, wameokoka na wanampenda Yesu Kristo sana. Na biblia imesema wazi kabisa kuwa Bwana atawafanya watu wake, “kuwa kichwa, wala si mkia” (kumb. La torati 28:13). Bwana atawafanya kuwa juu tu, wala siyo chini.
Kwa hiyo nilijua hakika haukuwa mpango wa Munguhuyo mmojawao ashindwe mitihani. Ndipo nilipoanza kumwuliza maswali huyu kijana; “je umefeli mtihani au umefelishwa”?
Yeye akajibu kwa mshangao akasema; “matokeo ya mitihani yametoka na yanaonyesha kuwa nimeshindwa mitihani mitatu – ambayo kwa utaratibu wa chuo huwezi ukaendelea na masomo”.
Kwa jibu hili nilielewa kuwa alikuwa haaelewa kwa nini nilimuuliza swali hilo. Kwa hiyo nilimwuliza swali jingine, nikasema; “Je uliwahi, kushuhudiwa rohoni juu ya matatizo utakayokuwa nayo kimasomo?” Yule msichana akajibu, “ndiyo”, na niliomba sana hata kwa kufunga”.
“Je uliomba tu pamoja na kuomba ulofanya bidii ya kusoma? Mimi nilimuuliza. Nilimuuliza swali hili kwa kuwa kuna wanafunzi wengine wakiokoka wanadhani watafaulu mitihani kwa maombi tu bila kufanya bidii katika kusoma. Wamesahau Biblia imesema “…..ufanye bidii katika KUSOMA…”  (Timotheo 4:13)
Yule msichana akasema nilipokuwa naomba niliweka bidii pia katika kusoma masomo. Je ulipomaliza kufanya mitihani ya masomo yote, ni masomo mangapi ambayo ulikuwa huna uhakika wa kufaulu?” nilimuuliza tena.
“Masomo mawili tu – ambazo kufuatana na taratibu za chuo nisingefukuzwa bali ningerudia mwaka mmoja tena” alieleza yule msichana. Baada ya mazungumzo hayo nilifahamu moyoni mwangu ya kuwa Ibilisi alikuwa alikuwa amenuia kuharibu masomo ya kijana huyo. Ghafla wazo lilinijia moyoni mwangu, halafu nikamwuliza swali Yule msichana; “Je unataka kurudi nyumbani au unataka kuendelea na masomo?”
Yule msichana alishangaa nilipomwuliza swali hilo, lakini akanijivbu akasema; “napenda kuendelea na masomo, lakini wamekwisha sema nimeshindwa na matokeo yamekwisha kupelekwa makao makuu ya wizara.
            Ndipo nikamkumbusha nikasema; “Mungu tunayemtumikia na kumwabudu katika Kristo Yesu, ni Mungu yule yule wa Joshua aliyesimamisha jua na mwezi visisogee mpaka wana wa Israeli walipomaliza vita kwa ushindi”.
            Nikaendelea kusema kuwa; “zaidi ya hayo tunalo jina la Yesu Kristo ambalo linapita majina yote na lina mamlaka mbinguni, duniani, na chini ya nchi. Yesu Kristo alisema tukipatana lolote duniani na kuomba  kwa Jina lake tutafanyiwa na Baba Mungu. Kwa hiyo tunakwenda kupatana na kuomba kwa Mungu kuwa matokeo ya mitihani yabadilishwe na urudi chuoni uendelee na masomo. Je! Wote tunakubaliana na patano hili?”
                        “ndiyo!” walijibu wale vijana kwa pamoja.
            Halafu nikasema hivi ndivyo mtakavyofanya; “mtarudi chuoni na kuanza kumtafakari Mungu, uku wake na matendo yake yaliyoandikwa katika Biblia. Pia, mtafakarimambo ambayo amekwisha watendea ninyi binafsi. Baada ya muda mtaona ndani ya mioyo yenu uzito wa mawazo ya kushindwa mtihani yanatoweka; na badala yake mioyoni mwenu mtajaa imani ya kujua hakuna lisilowezekana kwa Mungu”
            “kwa maneno mengine nataka mumtafakari Mungu  na ukuu wake, kiasi ambacho mfikie ndani yenu anakuwa mkubwa kuliko tatizo mlilonalo”.
            “Mkiifikia hali hiyo, ingieni katika maombi kama tulivyokubaliana, bila kusahau kutubu kwa ajili ya kushindwa mitihani. Na mimi nitashirikiana nanyi katika maombi nikiwa hapa nyumbani. Halafu kesho asubuhi uende (nikimtazama yule msichana aliyeshindwa mtihani) kwa mwalimu wako umwombe uone alama za matokeo ya mitihani ya masomo wanayosema umeshindwa – mwambie ya kuwa wewe unaamini kuwa umefaulu.
            Kwa jinsi ya kibinadamu lilionekana kama ni jambo lisilowezekana – lakini wale vijana walilikubali na wakaondoka.  Kesho yake jioni walirudi nyumbani kwangu kwa furaha, na yule kijana akanieleza yafuatayo:- “tulifanya kama ulivyotuambia, tukaomba na asubuhi leo nilikwenda kumwona mwalimu. Akanionyesha alama za mitihani yangu, na wakagundua kuwa kulikuwa na makosa kwa upande wao katika kuandika alama katika somo moja – badala ya kuandika maksi 19 waliandika 9. Wakaniambia nandike barua kwa mkuu wa chuo, na nikafanya hivyo, na mkuu wa chuo akasema niendelee na masomo.
            Yule kijana aliendelea na masomo vizuri, sasa amemaliza na anafanya kazi! Jina la Bwana libarikiwe!
            Mafanikio haya tuliyapata kwa sababu tulipatana na kuomba kwa JINA LA YESU KRISTO !
            Naamini wakristo wengi waliowahi kufanya maombi ya mapatano namna hii kwa Jina la Yesu Kristo, wanakubaliana name nikisema maombi ya jinsi hii yana mafanikio makubwa.
            Mke wangu, Diana, alikuwa ananishuhudia siku moja juu ya matendo makuu ya Jina La Yesu Kristo yaliyofanyika kwa mama mmoja aliyekuwa mjamzito. Alisema, mama huyo alikuwa amefanyiwa operesheni alipojifungua mtoto wa kwanza, lakini kwa mimba ya pili alitaka asijifungue kwa operesheni, bali ajifungue kwa njia ya kawaida.
             Mke wangu alisema, katika kikundi chao cha maombi cha akina mama walipatana kama alivyosema huyo mama kuwa wamuombe Mungu kwa Jina la Yesu Kristo ili (huyo mama) ajifungue kwa njia ya kawaida. Kwa hiyo wakaomba hivyo.
            Siku za kujifungua zilipowadia yule mama likwenda hospitalini na akalazwa kwa muda usiopungua wiki mbili bila kupata uchungu wowote wa kuzaa. Mara kwa mara daktari alimwambia kuwa anataka kumfanyia operesheni, lakini mara zote aliahirisha bila kutoa sababu za kuridhisha. Lakini yule mama alijua ni sababu ya maombi – maana walipoomba walikataa asifanyiwe operesheni.
            Baada ya wiki mbili hizo kupita siku moja ghafla alianza kusikia uchungu wa kuzaa na kisha akajifungua mtoto kwa njia ya kawaida kama walivyopatana katika maombi yao! Jina la Bwana libarikiwe kwa uweza wake mkuu. Lakini nataka ujue ya kuwa kufanyiwa operesheni si upungufu wa imani, na wala sina maana hiyo. Ila  yule mama alitaka ajifungue kwa njia ya kawaida! Na akapata alichoomba!
            Siku zote ukiomba, omba kwa jina la Yesu Kristo ukiwa na uhakika ya kuwa uatpewa ulichoomba. Ukiweza kumpata mkristo mwenzako wa kupatana naye kwenye maombi hayo ni vizuri pia.
            Kumbuka Yesu Kristo alisema,  “Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba,  watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao. ” (mathayo 18:19-20)

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW