Sunday, September 10, 2017

WASABATO WANAPINGA AGIZO LA MUNGU LA KUFANYA IBADA SIKU YA JUMAPILI

No automatic alt text available.
Katika agizo la kukusanyika kwa wana wa Israeli, Mungu alitoa siku mbili yaani Jumapili na Jumamosi, ingawa wasabato karibu wote hawalijui jambo hili, maana hao wamekaririshwa siku ya sabato tu yaani Jumamosi.
UTHIBITISHO:
Tunaweza kuthibitisha ukweli huu katika kitabu cha Kutoka 12:16 Biblia inasema, “SIKU YA KWANZA kutakuwa kwenu na kusanyiko takatifu, na SIKU YA SABA kutakuwa na kusanyiko takatifu, haitafanywa kazi yoyote katika SIKU HIZO, isipokuwa kwa hiyo ambayo kila mtu hana budi kula, hiyo tu ifanyike kwenu.”
Mungu aliwaamuru wana wa Israeli wakusanyike siku ya kwanza ya juma yaani Jumapili na siku ya saba yaani Jumamosi kwa kalenda ya kwetu. Pia Mungu hakuwaagiza kukusanyika tu, bali aliwaagiza wasifanye kazi pia. Lakini wanaojiita wasabato nyakati za leo, wanapinga kukusanyika Jumapili sawasawa na maagizo ya torati wanayodai kuifuata.
1. Swali ni kwamba, mafundisho yao ya kukusanyika siku ya sabato yametoka wapi?
2. Kama ni kwenye Biblia mbona siku moja hii wameiacha?
3. Je aliyetoa agizo la siku ya sabato ni Mungu mwingine na aliyetoa agizo katika kitabu cha Kutoka 12:16 (yaani kukusanyka siku ya Jumapili) ni Mungu mwingine?
Mtume Paulo anafundisha kuwa ni jambo la udanganyifu kuwafundisha watu washike siku ya Sabato. Kwa sababu ya wokovu wetu ndani ya Kristo (Wakolosai 2:11-15) Paulo anasema, “Basi, MTU ASIWAHUKUMU ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” (mstari wa 16).
Kwa hiyo agizo la kukusanyika lilikuwa ni siku mbili, imetajwa ya kwanza ni Jumapili (siku ya kwanza ya juma) na ya pili ni Jumamosi (siku ya saba) kwa kalenda yetu, kama tulivyoona katika kitabu cha Kutoka 12:16. Sasa tukija kwenye agizo la kushika sabato halikuwa ni siku ya kukusanayika, bali ni pumziko la kazi tu na kustarehe kama tunavyoweza kuona katika kitabu cha Kutoka 31:14-15, “Basi mtaishika hiyo sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake. Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa Bwana, kila mtu atakayefanya kazi yoyote katika siku ya sabato, hakika yake atauawa.”
Mungu hapa anasema kila mtu atakayefanya kazi siku hiyo atauawa, hajasema kila mtu atakaye kosa kwenda kwenye kusanyiko atauawa. Na ndiyo maana kwenye Biblia, inapotaja neno sabato ina maana ya kupumzika kazi na siyo kufanya kusanyiko la kuabudu kama wafanyavyo wanaojiita wasabato wa leo.
Pia Kutoka 35:2 Biblia inasema, “Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni sabato ya kustarehe kabisa kwa Bwana; mtu awaye yote atakayefanya kazi yoyote katika siku hiyo atauawa.”
Tunaona tena hapa, Mungu anasisitiza kwamba, atakayeuawa, ni yule atakayefanya kazi siku ya sabato, na hakusema atakayekosa kwenda kukusanyika kwa ajili ya ibada, kwani agizo hili lilihusiana na kupumzika kufanya tu. Kimsingi unaposema sabato, siyo dhehebu, wala siyo siku ya kuabudu, bali ni pumziko la kazi. Nyakati za leo, wanaojiita wasabato, wanachanganya siku ya kusanyiko na siku ya pumziko la kazi.
Paulo alihuzunishwa sana, kwa sababu anasema wazi hivi “…..sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini KUYAREJEA TENA MAFUNDISHO YA KWANZA yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? MNASHIKA SIKU, na miezi, na nyakati, na miaka.”(Wagalatia 4:9,10).
“Maana yale YASIYOWEZEKANA kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa DHAIFU kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma “YESU KRISTO” Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ILI HAKI YA TORATI YATIMIZWE NDANI YETU sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.” (Warumi 8:3,4).
Kwa hiyo, mtume Paulo anasisitiza, “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au SABATO.”
Tukiangalia tena maandiko katika kitabu cha Kumbukumbu la torati 5:14 kwenye ile amri ya nne ya kushika sabato, Biblia inasema, “Lakini siku ya saba ni sabato ya Bwana, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng’ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe.”
Kadhalika na hapa Mungu anaifafanua kwa uzuri kabisa, maana ya sabato na lengo lake. Lengo lilikuwa watu wapumzike, wanyama wapumzike, wafanyakazi wapumzike na kustarehe, kwa sababu hiyo, sabato iliwagusa mpaka wanyama. Kama ingekuwa kwamba sabato ilimaanisha siku ya kuabudu basi wanyama wasingetajwa kupumzika.
Mtu aliyepigwa mawe hata kufa nyakati za Musa jangwani, hakuuawa kwa sababu hakwenda kuabudu siku ya sabato, bali aliuawa kwa sababu alifanya kazi (Hesabu 15:32-36). Hii inathibitisha kwamba agizo la kushika sabato lililenga pumziko la kazi tu na si agizo la kukusanyika kama wanavyodai wasabato wa leo. Wana wa Israeli walikusanyika siku ya saba (Jumamosi) na siku ya kwanza ya juma (Jumapili) kwa agizo la Mungu mwenyewe katika Kutoka 12:16, kama tulivyokwisha kuona hapo nyuma. Kimsingi ni kwamba, katika amri kumi (Kumbukumbu 5:12-15), amri ya nne inazungumzia kupumzika kazi tu. Na Kutoka 12:16 Mungu anatoa mwongozo wa siku za kukusanyika kwa ibada. Swali ni kwamba, wasabato wa leo wanakusanyika Jumamosi kwa msingi wa andiko lipi kati ya hayo? Kama kwa msingi wa amri ya nne ya kushika sabato (Kumbukumbu 5:12-15), basi watakuwa wamepotea, maana pale haikuzungumziwa siku ya kukusanyika kwa ajili ya ibada, bali ni pumziko la kazi tu. Lakini kama wana kusanyika Jumamosi, kwa msingi wa andiko la Kutoka 12:16, kadhalika watakuwa wamepotea, maana, katika siku za kukusanyika, katika andiko hili, Mungu ametoa siku mbili yaani siku ya kwanza ya juma (Jumapili) na siku ya saba ya juma (Jumamosi), sasa mbona siku ya kwanza ya Juma (Jumapili) wanaipinga? Ni wazi kabisa wanampinga Mungu.
Shalom
Max Shimba mtumwa wa Yesu Kristo Mungu Mkuu na mwokozi wetu.

No comments:

FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE

  **URGENT UPDATE**   **FORMER MUSLIM EVANGELIST MUSA BELLO ARRESTED BY NIGERIAN POLICE** Shimba TV, New York has received distressing news ...

TRENDING NOW